WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amepata wadhamini zaidi ya 7000 katika mikoa ya Katavi na Rukwa, ambako ni nyumbani kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye naye anawania urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Akiwa mkoani Katavi ambao ni mkoa mpya alikozaliwa Waziri Mkuu Pinda, alipata wadhamini 3,450 huku Rukwa akipata wadhamini zaidi ya 4000.
Mkoa wa Katavi kabla ya kuwagawanywa ulikuwa unaunda mkoa wa Rukwa.
Lowassa aliwasili jana mchana mkoani Katavi akitokea Mkoa wa Kigoma na kupokewa na umati mkubwa wa wananchi wa Mpanda huku msafara wake ukipambwa na pikipiki kutoka Uwanja wa Ndege wa Mpanda hadi Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi.
Baada ya msafara wake huo kutoka kwenye ofisi za CCM mkoa ulielekea kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Mpanda ambako ulikuwapo umati mkubwa wa watu waliokuwa na shauku ya kumsikiliza.
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli mkoani Arusha alipofika katika Ofisi za CCM alisaini kitabu cha wageni.
Baada ya kusaini kitabu hicho, Katibu wa CCM Wilaya ya Mpanda, Elizebeth Kashili, alimkabidhi fomu za wana CCM waliomdhamini akisema waliomdhamini ni wanachama 3,450.
Akizungumza baada ya kukabidhi fomu na katibu wa CCM wilaya, Lowassa aliwashukuru wana CCM waliojitokeza kwa wingi kumdhamini katika safari yake ya matumani pamoja na kupata mapokezi makubwa mjini Mpanda.
Bada ya kumaliza na wana CCM wa Mkoa wa Katavi, Lowassa alikwenda mkoani Rukwa ambako alipata wadhamini zaidi ya 4000.
Akizungumza na wananchi mjini Sumbawanga jana, Lowassa alisema amezunguka kidogo lakini kila siku amekuwa akishuhudia mapokezi makubwa ambayo yanampa nguvu.
“Nimezunguka kidogo lakini kila siku kuna jipya mapokezi yenu yamenipa nguvu, huu ni mwanzo tu … je, nikiungwa mkono itakuwaje?
“Nawashukuru mlionidhamini mmenipa heshima ya kuniamini na mimi sitawaangusha, siri ya uchaguzi ni kupiga kura kuna watu wanapita wanasema CCM wanakataza kupiga kura ni uongo. CCM mtaji wake ni kura za wananchi naomba Mungu katika watu mtakaowapigia kura niwe mmoja wao,” alisema Lowassa.
Alisema anataka spidi ya maendeleo na ambaye hatataka spidi yake atamweka pembeni.
“Wale wanaosemasema waambieni yule jamaa ajenda yake ni kuondoa umaskini, usiwaseme watu, tushindane kuondoa umaskini kwa Watanzania,” alisema.