NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba amesema anatosha kugombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iwapo atapewa nafasi hiyo na vyama washirika.
Amesema anawania nafasi hiyo huku kujiona ni mgombea pekee anayeweza kuwaunganisha Watanzania na kwamba ndiye aliasisi jina la Ukawa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza Dar es Salaam jana baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kwa muhula wa tano, Profesa Lipumba alisema uamuzi wake wa kuwania urais unatokana na kiu yake ya kutafuta utatuzi wa masuala ya ufisadi na upatikanaji wa Katiba Mpya.
Kingine kilichomsukuma, alisema, ni kukuza uchumi, kushughulikia tatizo la ajira na lishe bora kwa watoto.
Profesa Lipumba ambaye amebobea katika masuala ya uchumi, alisema iwapo atapewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya Ukawa atahakikisha anawaletea Watanzania Katiba (iliyoshindwa kukamilika katika Bunge Maalumu la Katiba) itakayotatua kero za Muungano, itakayosimamia haki na uwajibikaji kazi.
“Kunyongwa kwa maoni ya wananchi katika Bunge Maalumu la Katiba ndicho kilichangia kwa kiasi kikubwa kuanza Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jina amabalo nililiasisi mimi, hivyo inaonyesha jinsi gani nilivyo mstari wa mbele kusimamia matatizo ya wananchi,” alisema.
Lipumba alisema iwapo atachaguliwa na Ukawa atahakikisha anaunda Serikali makini, yenye uadilifu na ambayo itatumia maliasili ya wananchi kwa masilahi ya wananchi wote na si kiongozi kujinufaisha mwenyewe.
Alisema ameamua kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia CUF ili baadaye aweze kuomba nafasi ya kuwania nafasi hiyo kupitia Ukawa kama walivyokubalina katika vikao vyao kwa kila chama washirika.
“Nachukua fomu hiyo kwa sababu naamini nina sifa, uwezo, uadilifu, uwazi na uwajibikaji wa kuweza kuwaunganisha watanzania kwa kuwawezesha kuepukana na rushwa na vitendo vya ufisadi,” alisema.
Alisema kutokana na historia yake ya uongozi na ushauri wa uchumi nchini na nje ya nchi anaamini anatosha kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Ukawa.
Profesa Lipumba alisema kama atachaguliwa atahakikisha anaandika historia ya kuwa rais wa kwanza kupata tuzo ya Mo Ibrahim kutokana na jinsi atakavyoiongoza Serikali itakayowaunganisha wananchi kwa rasilimali zilizopo.
Alisema atahakikisha anatoa motisha kwa wananchi watakaowafichua wezi wa mali za umma katika rasilimali za gesi na madini.
“Ukitoa motisha itasaidia kila mwananchi kuhusika katika kulinda rasilimali za nchi na hivyo kuwezesha nchi kupata faida kutokana na rasilimali hizo,” alisema.
AFYA
Profesa Lipumba alisema akipata nafasi ya kuwa Rais atahakikisha watoto wa maskini wanapata lishe bora kama ilivyo kwa watoto wa matajiri kuondoa wingi wa watoto wenye utapiamlo ambao utafiti wa afya duniani unaonyesha kwamba kila kwenye watoto 100 nchini, 42 wana utapiamlo.
“Tajiri wa Marekani Bill Gates alipotembelea Tanzania na kutakiwa kukadilia umri wa mtoto wa miaka 13 alisema ana miaka saba. Kama mjamzito hatopewa lishe anakuwa katika hatari ya kujifungua mtoto asiyekuwa na kinga hali inayomfanya baadaye kukosa afya na kuangukia katika umaskini,” alisema.
Kuhusu suala la afya kwa wazee, Lipumba alisema kuna wazee milioni 1.5 ambao wameshindwa kutengenezewa namna bora ya kuhudumiwa na kuenziwa.
“Nikichaguliwa katika nafasi hiyo nitahakikisha nawashughulikia wezi watakaobainika katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).
“Sitavumilia kuwaona wezi wa mali ya umma wakipita kifua mbele kutafuta wadhamini wa kuwawezesha kuwania urais, ila nitahakikisha nawashughulikia,” alisema.
AJIRA
Katika suala la ajira alisema ukosefu wa ajira umekuwa mkubwa na ndiyo sababu ya kuibuka kwa makundi ya uhalifu ya vijana kama Panya road, hivyo serikali yake itajenga mazingira mazuri ya kuwatengenezea ajira za kutosha wananchi.
“Tuna bandari ambazo zinaweza kututengenezea ajira kwa mfano Mtwara, tuna bandari ambayo ina kina kirefu cha asili ambacho tunaweza kutengeneza kituo cha viwanda na biashara ukizingatia ugunduzi wa gesi uliofanyika, hivyo wananchi wa Mtwara hawatakuwa na sababu ya kwenda mikoa mingine kutafuta ajira,” alisema.
Profesa Lipumba alisema kama Tanzania itajipanga katika miaka 10 ijayo inaweza kufaidika na ajira milioni 90 zinazotarajiwa kuondoka China kwenda nchi mbalimbali kutokana gharama za uzalishaji nchini humo kuwa juu hivyo zinaweza kusaidia sekta ya viwanda.
UJENZI WA MIUNDO MBINU
Alisema ujenzi wa miundombinu utasaidia kuunganisha nchi jirani za Rwanda Burundi, Congo DRC, Malawi na Zambia kwa kupitisha mizigo, jambo ambalo litasaidia kuongezeka ajira na usalama wa nchi kutokana na msaada huo.
Maalim Seif
Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Watanzania wamechoshwa kungozwa na utawala aliouiita kandamizi pamoja na viongozi wasio na maadili waliokubuhu kwa ufisadi.
Alisema ili nchi ifikie malengo na kujikomboa katika uchumi imefika wakati kwa Watanzania kuamua jambo moja kwa kuchukua hatua na kuiweka CCM pembeni na kuwapa nafasi Ukawa waweze kufanya mabadiliko nchini.
“ Watanzania lazima wawe makini kumpata rais ambaye si mbinafsi anayeguswa na matatizo ya wananchi ambaye ana upeo wa hali ya juu kuiongoza nchi yake,”alisema Seif.
Pia alisema kwa sasa CCM wajiandae kisaikolojia kwa kuwa wananchi wa wamechoshwa kuonewa na wanahitaji kufanya mabadiliko yatakayoleta tija ndani ya jamii.
Seif alisema ni vema jamii ikajiandaa vizuri katika Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba mwaka huu kumpata kiongozi atakayejenga uchumi imara wenye manufaa kwa kila mwananchi kwa masilahi ya jamii nzima.
“Hapa kwa Tanzania ni Profesa Lipumba pekee ndiye anayeweza kuiongoza nchi hii kwa ridhaa ya Ukawa kwa sababu hana ubinafsi na watanzania wa sasa wamechoka kuongozwa na utawala mbovu … anaweza kuimarisha uchumi wa nchi,”alisema Maalim Seif.
Alisema endapo wananchi watawapa nafasi Ukawa katika awamu ijayo hakutakuwa na matajiri wa kupindukia wala maskini wa kutupwa kwa sababu tofauti ikiwa kubwa ndani ya jamii ni dhambi.
Seif alisema kwa sasa baadhi ya watu wanamiliki mamilioni ya dola huku Watanzania wengine wakiwa hawanufaiki na nchi yao kutokana na ufisadi uliokithiri.
Mzee Waikela
Naye mpigania uhuru tangu enzi za utawala wa ukoloni, Billal Rehan Waikela, aliwataka vijana wengi wajitokeza kujiunga na CUF kwa vile ndicho chama chenye viongozi imara.
Alisema binafsi ameitumia CCM tangu enzi za TANU akiwa na baba yake Profesa Lipumba, mzee Haruna Lipumba ambao walikuwa wanapambana kuhakikisha wanawaondoa Waingereza lakini hadi sasa hakuna matunda waliyoyapata.
Waikela alisema anaishangaa Serikali kuona inashindwa kumpa heshima Lipumba wakati anajulikana dunia nzima kutokana na uwezo wake mkubwa wa elimu alionao.
“Mimi binafsi ninaona kwamba anayefaa nchi hii kuiongoza na kuifikisha mahali pazuri ni Lipumba pekee yake kwani si mbinafsi, anayebisha katika hili aje anitoe roho na nipo tayari,”alisema Weikela.
Juma Duni
Makamu Mwenyekiti na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar kupitia chama hicho, Juma Duni Haji, alisema Profesa Lipumba hajachoka kupigania maslahi ya wananchi ingawa anagombea kwa awamu ya tano sasa.
Alisema CCM hakiwezi kuwatoa wananchi kwenye umasikini hivyo amewataka wananchi kuzinduka kutoka usingizini na kufanya uamuzi mwaka huu ambao ni wa mabadiliko.
Alisema Profesa Lipumba ambaye ni mpambanaji katika masuala ya kupigania masilahi ya wananchi alipigwa mchana kweupe na polisi lakini wezi wanapata haki.
“Profesa Lipumba alipigwa na polisi mchana kweupe na jamii ikishuhudia lakini huyo huyo aliyepigwa ndiye aliyeshitakiwa lakini wanaoiba mapesa hawashitakiwi licha kuwapo kwa ushahidi, wanadai hadi wafanye upelelezi,” alisema Duni.
Alisema alikutana na Profesa Lipumba mwaka 1972/73 akiwa anachukua Shahada ya Uchumi na yeye akichukua Shahada ya Sayansi na tangu hapo wamekuwa wakishirikiana hadi leo.
“Tumekuwa tukigombea kwa pamoja kwa hawamu tatu akiwa na hali ileile ya kutaka kuwakomboa watanzania hivyo kutokana na matatizo yanayoikumba nchi yetu kutoka kwa uongozi wa CCM… hata watanzania wazikili wakiwa uchi hawawezi kupata msaada wowote kutoka kwa CCM,” alisema Duni.
HABARI HII IMEANDALIWA NA SHABANA MATUTU, CHRISTINA GAULUHANGA, KOKU DAVID NA ADAM MKWEPU, DAR E S SALAAM.