Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM |
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, leo inashuka dimbani kuumana na Township Rollers katika pambano litakalopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo mbili zimetinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kushinda michezo yao ya hatua ya awali.
Yanga ilifuzu hatua hiyo baada ya kuwanyuka mabingwa wa Shelisheli, timu ya St Louis kwa jumla ya mabao 2-1, ambapo walishinda bao 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini jijini Port Louis.
Township kwa upande wake iliiondosha mashindanoni Al Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2, wakishinda mabao 3-0 nyumbani kabla ya kupigwa mabao 2-1 ugenini nchini Sudan.
Katika michuano iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilishiriki lakini ikajikuta ikiishia raundi ya kwanza baada ya kuondolewa mashindanoni na Zesco FC ya Zambia, ambapo ililazimishwa sare bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kutoka suluhu jijini Lusaka.
Hii ina maana kwamba Yanga inatakiwa kupambana kufa au kupona ili kufuzu hatua ya makundi baada ya kuchemka katika michuano iliyopita.
Akizungumzia mchezo huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema wanawaheshimu wapinzani wao kwani wanaamini ni timu nzuri, ndiyo maana ilifanikiwa kuitoa mashindanoni Al Merreikh, lakini wamejiandaa kupambana na kushinda.
“Hatuwezi kuwadharau wapinzani wetu hata kidogo, tunafahamu wana uwezo mkubwa dimbani na hata nje ya uwanja, ni timu iliyojiimarisha kiuchumi.
“Hii ina maana kwamba tunaingia uwanjani kwa tahadhari na kuepuka makosa ambayo yanaweza kutugharimu,” alisema Mkwasa ambaye pia ni kocha wa soka kitaaluma.
Akizungumzia hali ya kikosi chake kwa ujumla, Mkwasa alisema wamefarijika hasa baada ya kiungo wao, Thaban Kamusoko na mshambuliaji, Obrey Chirwa, kupona majeraha yaliyowafanya wakae nje ya uwanja kwa muda mrefu.
“Chirwa na Kamusoko wako vizuri kucheza mchezo wa kesho (leo) kama mwalimu ataona inafaa, ukiwaondoa hao tunawakosa Ngoma (Donald) ambaye ameanza mazoezi madogo madogo hivi karibuni na Andrew Vincent ‘dante’, hawa wanaendelea kuimarika lakini hawako fiti kwa mchezo,” alisema Mkwasa.
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, alisema lengo lao ni kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao ili kuwarahisishia watakapoumana ugenini.
“Tunatakiwa kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani, hili ni muhimu sana kwani litatusaidia kutimiza azma yetu ya kupata matokeo mazuri pia ugenini na kusonga mbele.
“Nimewafuatilia hawa wapinzani wetu kimsingi ni timu nzuri, nimewaambia wachezaji wangu tunapaswa kuwa waangalifu na kuepuka makosa ya kizembe ambayo yanaweza kutugharimu, ukizingatia kadiri unavyozidi kusonga mbele katika mashindano, ndivyo unavyozidi kukutana na ugumu,” alisema Lwandamina raia wa Zambia.
Naye kocha wa Township,Nikola Kavazovic, alisema anawafahamu Yanga baada ya kuwafuatilia kupitia michezo yao, hivyo wamejiandaa kwa mapambano.
“Nimeifuatilia Yanga katika baadhi ya michezo yake, ni timu nzuri lakini na sisi tumejiandaa kwa mapambano na lengo ni kushinda,” alisema Kavazovic.
Beki na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema wanafahamu kwamba mchezo huo hauwezi kuwa rahisi, lakini wamejiandaa kwa ajili ya pambano, lengo likiwa ni kushinda na kufuzu hatua inayofuata.