NA OMARY MLEKWA -HAI
SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imeifunga Shule ya Msingi Kibohehe iliyopo Wilaya ya Hai kwa muda usiojulikana ili kupisha ukarabati kutokana na baadhi ya miundombinu yake kuharibiwa vibaya na mvua na upepo.
Mkuu wa Mkoa huo, Anna Mghwira, alitoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo kujionea uharibifu uliotokea hali ambayo ilisababisha mwanafunzi mmoja wa darasa la sita kupoteza maisha huku wengine watatu wakijeruhiwa vibaya.
Alisema uamuzi huo unatokana na kubaini kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo umejengwa chini ya kiwango jambo ambalo lisipoangaliwa kwa umakini linaweza kusababisha madhara mengine kwa wanafunzi na watumishi wa shule hiyo.
“Tunafunga shule hii ili kupisha ukarabati wa majengo na wanafunzi kuanzia darasa la awali hadi la saba watatawanywa katika shule nyingine za jirani mpaka pale ukarabati utakapokamilika,” alisema Mghwira.
Kwa upande wake mhandisi wa Halmashauri hiyo, Loshiwa Moleli, alisema shule hiyo ilijengwa zamani na tayari walishashauri kuwa majengo hayo yavunjwe ili kuepuka madhara.