26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

AZAM FC, YANGA VITA YA MAFAHARI

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Azam FC leo itawakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo utakaokuwa na upinzani wa aina yake.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo, ambaye awali uongozi wa Azam FC kupitia kwa Ofisa Mtendaji wake mkuu, Abdul Mohammed, uliiandikia barua Bodi ya Ligi Tanzania Bara ya kutokuwa na imani na mwamuzi huyo.

Itakumbukwa kuwa mwamuzi, Nkongo, ndiye aliyechezesha pambano la Azam FC dhidi ya Yanga, Machi 2012 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo wachezaji wa mabingwa hao watetezi walimpiga.

Katika mchezo huo, Azam waliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Azam FC wataingia uwanjani wakiwa na morali ya hali ya juu baada ya kutoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons, katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Yanga wao wataingia uwanjani pia wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mafahari hao, Azam na Yanga, watakuwa vitani katika mchezo huo, huku kila mmoja akisaka ushindi, ambapo ‘Wanalambalamba’ wakihitaji kukalia usukani wa ligi hiyo, huku Yanga wakitaka kusogea kileleni na kutimiza azma yao ya kutetea ubingwa.

Azam inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 30, huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 25, wakati vinara wakiwa ni Wekundu wa Msimbazi, Simba wakiwa na pointi 32.

Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Azam FC, Iddy Cheche, alisema wanahitaji kuweka heshima katika mechi hiyo, hivyo watahakikisha wanapambana na kupata pointi tatu zitakazowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Wachezaji wapo vizuri, tumejiandaa kwa ajili ya ushindani katika mchezo ili tuweze kupata ushindi, hivyo tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwapa sapoti wachezaji wetu,” alisema.

Kwa upande wa Yanga kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Dismas Ten, alisema wanawaheshimu Azam lakini hata hivyo watapambana ili wapate pointi tatu kwani lengo lao ni kutetea ubingwa wao na hawafikirii kupoteza kirahisi.

“Mchezo ni mgumu kwani kila timu imejiandaa vizuri, lakini kama tunavyosema kila siku kwamba lengo letu ni kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, hivyo mashabiki wajitokeze kuisapoti timu yao,” alisema.

Katika mchezo wa mwisho timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ilikuwa kwenye raundi ya kwanza msimu uliopita, ambapo Yanga walishinda bao 1-0.

Yanga wataingia uwanjani bila nyota wao, Pius Buswita, mwenye kadi tatu za njano, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Thaban Kamusoko, Yohana Nkomola, Pato Ngonyani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambao ni majeruhi, huku mshambuliaji wao, Obrey Chirwa, akitarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha leo.

Msimu wa mwaka wa 2014/15, timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa kwanza, Desemba 28, 2014, zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, wakati mzunguko wa pili Azam FC walishinda 2-1.

Msimu wa 2015/16, hakuna timu iliyoonyesha umwamba kwa mwenzake kwani mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 17, 2015, zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, huku mzunguko wa pili uliochezwa Machi 5, 2016, zikatoka tena sare ya kufungana mabao 2-2.

Michezo mingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo, Stand United  wataikaribisha Ndanda FC katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, huku Mbeya City wakiwakaribisha Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles