29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KAMPENI KINONDONI HUKU LOWASSA, SUMAYE KULE MWIGULU

  • Mbowe asema Mollel alikuwa gunia la misumari CHADEMA

AGATHA CHARLES Na OMARY MLEKWA -DAR /SIHA

VYAMA viwili vyenye upinzani mkali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo vinazindua kampeni zao katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam.

Vyama hivyo, CCM ambacho kimemsimamisha Maulid Mtulia kutetea nafasi yake ya ubunge baada ya kujiuzulu na kujiunga na chama hicho na Chadema, ambacho kimemsimamisha Salum Mwalimu, vyote vitatumia siku 21 zilizobaki kunadi sera zao na kuwashawishi wapigakura waweze kuvichagua.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema, aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa, chama hicho kitazindua kampeni zao saa nane mchana, kwenye viwanja vya Ali Mapilau, vilivyoko karibu na Hospitali ya Mwananyamala.

Alisema kampeni hizo zitaongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, akiambatana na viongozi wengine, akiwamo Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye.

Lowassa na Sumaye wote wawili ni Mawaziri wakuu wastaafu na walihamia Chadema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wakidai kuchoshwa na CCM.

Wakati Chadema kikisema hivyo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba, alisema chama hicho kitazindua kampeni zake saa sita mchana katika viwanja vya Biafra, Kinondoni.

Kwa mujibu wa Mwakifamba, miongoni mwa watu ambao wataambatana na mgombea wa CCM katika uzinduzi huo wa kampeni hizo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba pamoja na viongozi wa Mkoa na Wilaya wa chama hicho.

Kampeni katika jimbo hilo zinatarajia kuwa za kusisimua kutokana na mpambano baina ya vyama hivyo, huku pia Chadema pamoja na Ukawa kikipambana na mgombea wa CUF, inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba, Rajabu Juma.

Upande wa CUF unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, unampigia debe mgombea wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa, Mwalimu.

Hata hivyo, tayari mpasuko huo wa upinzani kama usipoangaliwa kwa jicho la tatu, utasababisha kupunguza nguvu ya upinzani.

Ugumu pia upo kwa CCM, ambacho kinamnadi  mgombea kiliyewahi kumpinga katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 akiwa CUF.

Si hilo tu, bali pia ni mgombea ambaye aliwahi kuwa mbunge kabla hajakihama chama hicho na kwamba tayari hilo limewagawa baadhi ya waliokuwa wapiga kura wake.

Itakumbukwa kuwa, uchaguzi huo unafanyika baada ya Mtulia kujivua uanachama wa CUF na kuhamia CCM, huku akitoa sababu ya kuchukua uamuzi huo kuwa ni kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Tayari Jeshi la Polisi la Mkoa wa Kinondoni limetoa wito kuwa, kampeni hizo zifanyike kistaarabu na kufuata misingi ya kisheria, kanuni na taratibu zilizoidhinishwa na Tume ya Uchaguzi.

Kamanda wa Polisi Kinondoni, Murilo Jumanne, alisema Jeshi hilo liko tayari kwa ulinzi na litahakikisha kuwa sheria zinafuatwa.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 17, mwaka huu, ukihusisha pia Jimbo la Siha pamoja na kata nne za Tanzania Bara.

MBOWE AMKAANGA MOLLEL

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe, amesema wananchi wa Jimbo la Siha hawapaswi kusononeka kwa kuondoka kwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Godwin Mollel, kwani walikuwa wamejitwika gunia la msumari.

Akihutubia wananchi wa Kata ya Ngarenairobi katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia Chama hicho, Elvis Mossi, alisema katika tathmini waliyoifanya kwa kipindi chote alichokaa katika nafasi hiyo alikuwa gunia la misumari si tu kwa chama, bali na kwa wananchi wa jimbo hilo, kwani alishindwa kuwasaidia na kuwatetea.

Alisema huu ni uchaguzi wa marudio, ingekuwa nchi za demokrasia, Chadema wangeruhusiwa kufanya uchaguzi kwa kumchagua mtu mwingine kutoka chama hicho.

Katika hatua nyingine, Mbowe aliwataka wananchi wa Siha kupuuza maneno yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jaffo, kuwa wasipoichagua CCM hakuna maendeleo.

“Mgawo wa fedha za maendeleo unapangwa kwa kufuata taratibu na namna  jinsi shughuli zinavyofanyika hata hapa Siha, barabara zinajengwa, shule na hata zahanati zinajengwa, hata kwenye majimbo yanayoshikiliwa na Ukawa,” alifafanua.

Kwa upande wa mgombea ubunge kupitia Chadema, Mossi, aliwataka watu wa Siha kumwamini kumpa kura na hakuna atakayeweza kumnunua, endapo ikitokea hivyo, wananchi wa Jimbo hilo wamchome moto yeye na familia yake.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama hicho mkoani Kilimanjaro (Bawacha), Grace Kiwelu, alisema aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo alishindwa kuwatetea wananchi wake na badala yake alikuwa mnafiki.

Mratibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema maigizo aliyoyafanya Dk. Mollel ni aibu kwake na familia.

“Naamini kitendo hicho kimewafedhehesha sana Wanasiha na uchaguzi huu naomba uwe kati ya wananchi na kumrudisha Mollel ni kurudisha laana katika jimbo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles