32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TUMESHTUSHWA NA KASI YA ONGEZEKO LA MIMBA KWA WANAFUNZI

SUALA la mimba kwa wanafunzi limekuwa ni tatizo la muda mrefu, ambalo linapigiwa kelele na Serikali na wadau mbalimbali kila kukicha.

Kwa muda mrefu sasa, Serikali kuanzia viongozi wa kitaifa, mikoa na wilaya, wamekuwa wakali  dhidi ya watu ambao wanawapa mimba wanafunzi, kitendo  ambacho kinawaharibia safari yao ya masomo.

Katika toleo la jana la gazeti hili, kulikuwa na  taarifa kutoka mikoa ya Morogoro, Geita na Simiyu, inayoonyesha tatizo hilo limekuwa likizidi kuongezeka siku hadi siku.

Katika taarifa hizo, Wilaya ya Kilosa, Morogoro, mwaka jana imeripotiwa wanafunzi 15 walikatisha masomo yao, huku katika Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita, wanafunzi 52 wamelazimika nao kuacha masomo kwa tatizo hilo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Hamim Gweyama, anasema wanafunzi walikatisha masomo kati ya Januari hadi Desemba 31, mwaka jana.

Anasema kati ya hao 37 wanasoma shule za sekondari, wakati waliobaki ni shule za msingi.

Akionyesha masikitiko yake, Gweyema anasema idadi hiyo ni kubwa na ya kutisha, kwani lazima ishughulikiwe haraka na mamlaka zinazohusika, sambamba kuwekwa  mikakati madhubuti.

Lakini jambo la kusikitisha ambalo limejitokeza katika matukio yote hayo, hakuna kesi hata moja  kati ya zilizopelekwa mahakamani ambayo imehukumiwa. Hapa  lazima tujiulize tatizo ni nini?

Inawezekana wazi mahakama imeshindwa kuhukumu kutokana na kukosa ushahidi, kwa sababu wazazi wengi wamekuwa wagumu kwenda mahakamani kutoa maelezo ya kina ya kuwatia hatiani wahusika.

Lakini pia hutumia nafasi hiyo, kuwatisha watoto wao wasiwataje watu waliowapa mimba, kwa madai kuwa watawakosesha mahari jambo ambalo haliingii akilini.

Tatizo kama hili limeshamiri pia katika mikoa ya Katavi na kwingineko.

Kwa mfano Wilaya ya Maswa imekuwa na tatizo kubwa la mimba za utotoni ambazo mamia ya watoto wa kike wanaopaswa kwenda shule hawaendi.

Takwimu za mwaka jana katika wilaya hiyo, zinaonyesha wanafunzi 68 walipata ujauzito.

Hili ni janga kubwa ambalo linahitaji kudhibitiwa haraka.

Kutokana na hali ilivyo, tunazishauri mamlaka zinazohusika kuongeza  nguvu zaidi ili kuwakomboa watoto wa kike ambao ndoto zao zinazimwa na watu wasiowatakia mema.

Tunasema hivyo kwa sababu tunatambua Serikali ina mkono mrefu wa kupambana na watu wa aina hii katika jamii, lakini haitafanikiwa bila kupata ushirikiano kuanzia kwa mwanafunzi mwenyewe hadi mzazi.

Sisi MTANZANIA, tunawashauri wazazi na watoto wanaokumbwa na tatizo hili, kuwa mstari wa mbele kwenye vyombo vya dola na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia kuwatia mbaroni wahusika hawa.

Tunasema hivyo kwa sababu kwa kipindi kirefu kumekuwapo na taarifa kuwa kesi nyingi zinashindwa kuhukumiwa kutokana na kukosa ushahidi wa pande zote mbili, yaani mwanafunzi na mzazi, kitendo ambacho kinazidi kuwapa mwanya mafataki haya.

Tunamalizia kwa kusema  kuwa tumeshtushwa na wingi huu wa mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi na tunamwomba kila Mtanzania kuwa balozi wa kupiga vita ukatili huu ambao unazima ndoto za watoto wetu ambao ni tegemeo la taifa katika siku zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles