28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KUCHAPA SI NJIA YA KUMFUNZA MTOTO ADABU


Na CHRISTIAN BWAYA

FAMILIA zetu zimetuumba kuwa hivi tulivyo. Tabia zetu, mitazamo, misimamo na imani zetu, mara nyingi ni matokeo ya vile tulivyolelewa. Hiyo inaitwa nguvu ya malezi. Upo ukweli wa dhahiri kuwa bila mchango wa familia zetu tusingekuwa na mafanikio tuliyonayo. Hii ndiyo sababu hatuachi kuwashukuru wazazi wetu kwa yale waliyoweza kuyafanya kwetu. Bila maelekezo, makaripio tuliyoyaona kwa wazazi, bila pengine tungekuwa watu tofauti na hivi tulivyo leo.

Hata hivyo, yapo mambo ambayo pengine hayakuwa mazuri tumejifunza kwa wazazi wetu. Tunaweza tusipende iwe hivyo lakini huo unaweza kuwa ukweli. Kusema hivyo haimaanishi wazazi wetu walifanya hivyo kwa makusudi, hapana. Mara nyingi hutokea bila hata wao kujua tena wakati mwingine ni kwa sababu tu ya desturi zilizokuwa zimezoeleka kwenye eneo walilokulia.

Inawezekana, kwa mfano, unachelewa kurudi nyumbani bila sababu ya msingi kwa sababu ndivyo baba alivyokuwa. Inawezekana huwezi kuwa karibu na watoto kwa sababu ndivyo ilivyokuwa kwenye familia yenu. Haya yote hayawezi kuwa makosa ya moja kwa moja ya wazazi wako lakini yanaweza kuathiri namna unavyowalea watoto wako.

Ninakuletea mjadala huu si kwa lengo la kuwanyooshea kidole wazazi wako bali kujitathimini na kuona hatua unazoweza kuchukua kubadili mwelekezo wa mambo kama mzazi unayetazamwa na wanao. Bila kuchukua hatua mapema kukabiliana na hali hiyo, upo uwezekano mkubwa hayo unayoyafanya ukayahamisha kwa watoto wako ambao, kama tulivyosema, kila siku wanakutazama.

Pengine unaweza kusema; “haya hayanihusu. Ninawalea wanangu vizuri sana.” Sawa. Lakini kumbuka wakati mwingine kuna mambo tunayafanya tukiamini ni sahihi lakini kumbe ni alama tulizoachiwa na wazazi wetu. Nilitoa mfano juma lililopita kwamba, unaweza kuwa umewaachia uhuru mno watoto wako ukiamini ni sahihi. Usichojua ni kwamba inawezekana unafanya hivyo kama namna fulani ya kulipiza kile ulichokikosa ukiwa mtoto. Hili usipolirekebisha linaweza kuwaathiri wanao.

Pia inawezekana wewe ni mwepesi sana kuadhibu watoto ukiamini hiyo ndiyo njia sahihi ya kulea watoto. Wakati mwingine unawachapa makofi watoto na hata kutumia fimbo kwa sababu hivyo ndivyo ulivyolelewa. Unafikiri ni sawa kwa sababu na wewe ulichapwa na umefika hapo ulipofika. Lakini usichokijua ni kwamba hiyo huenda ni alama uliyoachiwa na wazazi wako hawakuwa na mbinu mbadala ya kunyoosha tabia. Kumbe unaweza kujifunza mambo yanayoweza kukuza nidhamu ya mwanao bila ulazima wa kuwaadhibu mara kwa mara.

Najua unasoma safu hii kwa sababu ungependa kuwa mzazi anayewafunza wanae tabia njema. Nayaandika haya ili uwajibike na malezi unayowapa wanao badala ya kuendeleza mnyororo wa malezi yenye athari kwa wanao. Natamani uweze kukata mnyororo wa tabia na hulka usizopenda wanao wajifunze.

Kwa kuanzia hebu jiulize maswali haya kukusaidia kujitafakari na pengine kuchukua hatua. Je, mwanangu anapoonesha tabia nisiyoipenda, nina mazoea ya kuchukua hatua nilizozoea kuziona wazazi wangu wakinichukulia kama kufoka, kupiga kelele na kupiga? Kwa nini?

Je, kuna uwezekano kuwa ninachowafanyia wanangu kinaweza kisiwe haki na labda ni kuwaonea lakini binafsi naona sawa kwa sababu tu ndicho nilichokiona kikifanywa nyumbani na kwenye jamii? Je, kuna namna naweza kubadilika na kujifunza tabia mpya?

ITAENDELEA

Christian Bwaya ni mhadhiri wa saikolojia, mtafiti na mshauri wa masuala ya malezi na familia. Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles