Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), wameazimia kumng’oa Rais wa serikali hiyo, John Jilili baada ya kutoa taarifa kwa umma akimpongeza Rais John Magufuli kukataa kuongeza muhula wa uongozi kutoka miaka mitano hadi saba.
Mgogoro huo umezuka baada ya Makamu wa Rais wa DARUSO, Anastazia Antony na Spika wa Bunge la wanafunzi Deogratias Mahinyila kupinga hatua hiyo ya kumpongeza Rais Magufuli kwa madai kuwa imetolewa na mtu binafsi ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na si kama Rais wa DARUSO.
Kutokana na hali hiyo, Rais huyo wa DARUSO, ametangaza kuwavua nyadhifa za uongozi mawaziri watatu wa serikali hiyo ambao ni Matata Juma aliyekuwa Waziri wa Mikopo, Marobo Stanislaus aliyekuwa Naibu Waziri wa Mikopo na Deborah Mlawa aliyekuwa Waziri wa Malazi, Maji na Mazingira kwa kosa la kuipinga taarifa yake hiyo.
Kitendo cha Jilili kuwavua uongozi mawaziri hao tayari pia kimepingwa na baadhi ya viongozi huku Bunge la wanafunzi likianza kukusanya saini ili kupeleka hoja katika kikao cha dharura cha Bunge na kupiga kura ya kumuondoa madarakani.