AGOSTI 16, 1993 Mwalimu Julius Nyerere alifanya mazungumzo na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani, jijini Dar es Salaam, na kufafanua hotuba aliyoitoa kwa wabunge mwishoni mwa juma lililokuwa limepita (wakati huo) kuhusu masuala mbalimbali ya Katiba ya Muungano.
Mwalimu Nyerere alianza kwa kuwaambiwa waandishi hivi:
Nawashukuruni kwa nafasi hii. Juzi nilipotoka pale, niliwakuta nje ya Bunge nikawaruka. Sikuona kama jambo lenyewe linanihusu. Halafu baadaye baadhi yenu walikuja hapa, wakanivizia-vizia. Nao nikawaruka. Lakini naelewa kwanini walitaka tuzungumze. Na sasa tunazungumza.
Kwanza nilisita kusema na magazeti au kutoa maoni yangu wazi katika hadhara kwa sababu ya uzito wa mambo yenyewe yanayohusika. Nilisita kutokana na uzito wake na kwa hali ile iliyokuwepo wakati ule. Na sasa nasema vile vile kutokana na uzito wake. Kwa hiyo kilichonifanya nisite ni uzito. Sikuona nitasema nini wakati huo na kilichonifanya nikubali hadi sasa ni uzito wake.
Niliona kuwa pengine ni vizuri yakatoka maelezo kama ninavyoyaona kuhusu mambo haya mazito ili yaweze kueleweka; kwa sababu nadhani viongozi wetu watapata taabu kuyaeleza vizuri na yalivyo. Kwa hiyo si vibaya nikifanya jitihada ya kuyaeleza kwa sababu yasipoeleweka yalivyo na ni mazito inawezekana vitendo vya watu au maneno yao baadaye yatategemea hivyo wanavyojua na kumbe hivyo wanavyojua sivyo ilivyo kweli.
Kwa hiyo nilidhani ni vizuri nitumie nafasi hii kuyaeleza vizuri na ichukueni nafasi yenu kuniuliza maswali ili yaeleweke vizuri kwa matumaini ya kwamba mtayaandika vizuri. na watu wakisema huyu mzee anasema nini wawe hicho wanachokisema ndicho kile nilichowaambia. Kwa sababu haya nitakayosema sidhani kama yatampendeza kila mtu. Lakini ni vizuri yakajulikana.
Mimi naamini katika matatizo tuliyokuwa nayo sasa tumefika mahali yanaweza kuelezwa. Mimi nilikuwa naona matatizo mawili tu: yote ya Katiba.
Moja la maoni ya kubadili Katiba ya nchi yetu ili ilingane na hali ya sasa ya utaratibu wa vyama vingi. Kwa maana moja ilikuwa la maoni tu. La pili nalo ni la Katiba. Ni la uamuzi wa Zanzibar kuingia katika OIC (Jumuiya ya Kiislamu). Nalo ni la Katiba.
Endelea kufuatilia…
SWALI: Kwa muda mrefu viongozi wetu wamekuwa hawana utamaduni wa kuwajibika hata pale ambapo imebainika wamevuja sheria. Mwalimu hivi karibuni kumetokea suala la OIC ambalo ni uvunjaji wa Katiba ya Muungano. Wewe una maoni gani kuhusu utamaduni huo?
JIBU: Mimi naamini kwamba ni haki. Mimi ninawaambieni kuwa misingi tunayotaka na ambayo tumekuwa tukiijenga ni kwamba tutawaliwe kwa mujibu wa Katiba tu. Tufunzane, tuzoezane kuongoza nchi kwa mujibu wa Katiba, kwa mujibu wa sheria na kama haifanyiki wanadhibitiwa wale ambao wamevunja katiba. Hakuna mtu above sheria (aliye juu ya sheria). Wale wanaovunja Katiba ya nchi wanadhibitiwa, na lazima tuwe serious (makini) katika jambo hilo. Sasa jambo la kudhibiti viongozi tukiliogopa … hapa hapa nilisema hivyo na niliwaambia wabunge, si kama nateta, na hili ni jambo nalisema waziwazi … Sasa mimi nasema ni jitihada za kutengeneza na kujenga utaratibu kusudi tuiongoze nchi yetu kwa mujibu wa sheria; kwa mujibu wa utashi.
Na nilieleza hivyo bungeni, lakini mbunge mmoja akaniambia ‘Mwalimu sasa tizama mambo yenyewe. Liko soko la Kariakoo. Liliwekwa kwa mujibu wa sheria. Ipo menejimenti yake, lakini anakuja mtu anaiweka kando hiyo menejimenti anaweka yake.’ Sasa si ndiyo hivyo nikawaambia si mnamdhibiti huyo? Sasa mbona mnaogopa? Wakaniambia tunajaribu lakini wanakuwa wakali sana. Ala! Sasa katika mambo ya msingi haya lazima tukubali ku-pay the price (kulipa gharama) ya kuyasimulia kama yanaharibika.
Kwa hiyo katika hili, jambo lililokuwa la maana kama viongozi wetu wanaendelea kuwa wakorofi ni kuwadhibiti. Lakini kuigawa Tanzania sasa iwe na serikali yake, tuigawe tu, tuigawe. Na mimi naamini kabisa Muungano huo utavunjika na Rais (Ali Hassan) Mwinyi atakuwa Gorbachev (Rais wa iliyokuwa Urusi) na niliwatania hapa (wabunge) kwamba Yeltsin (wakati huo alikuwa Rais wa Russia) mmeshampata?
Sasa vema iko siku moja Rais atatoka Bukoba na tutaanza kuuliza mbona huyu katoka Bukoba? Ama! Sasa kwani atatoka mbinguni? Si atatoka Bukoba? Sasa hizi si argument (hoja) za maana. Sasa mtaendelea hivyo hivyo mpaka lini? Tujenge utamaduni wa kudhibiti viongozi wetu kama wanavunja sheria. Tusiogope. Mkianza mkiwa na woga, I promise you (nawaahidi), iko siku mtatawaliwa na dikteta. Mkiogopa-ogopa namna hii ninyi, wabunge, mkiogopa-ogopa, mkisema mzee wanakuwa wakali, then you are making absolutely fake, you will be under a dictator (basi mnajidanganya na mtajikuta mko chini ya dikteta).
SWALI: Mwalimu umesema hivi sasa tujaribu kuponya majeraha ambayo yameletwa na hili suala la Zanzibar kujiunga na OIC. Lakini naona hili litakuwa gumu kwa kuwa hao ambao wamesababisha majeraha hawaoni kwamba wamesababisha hayo. Nasema hivyo kwa sababu nimesikiliza hotuba ya Rais Salmin (wa SMZ na Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati huo) na amekuwa akisisitiza kuwa hakuna kosa. Sasa tuponyeje majeraha ambayo walioyasababisha hawayaoni?
JIBU: Sasa mimi nasema hivi, kwa maana ya nchi, kitendo tunachokitaka kimeshafanywa. Zanzibar imetoka katika OIC. Mimi jitihada yangu ni kuwaelezeni kitendo cha nchi kujiunga na OIC. Zanzibar imetoka. Maneno ya mtu mimi sina. Yeye ni mtumishi. Viongozi wetu hawa, pamoja na Salmin, walikuwa wamefika pagumu sana. Walikuwa wamechukua public position (msimamo) ya kuonekana kuwa jambo hili ni alright (sawa). Walifika. It’s a very difficult position humanly speaking (ni msimamo mgumu sana kiutu).
Gumu ukishasema jambo hili ni sawa halafu kesho linaonekana si sawa. Lakini viongozi wetu wamefikia uamuzi huo. Sikufanya mimi. Hamkufanya ninyi. Kama kulikuwa na ugumu kufanya hivyo ilikuwa vigumu kwa Rais wetu na Salmin. Gumu sana wamefanya. Na Rais juzi mbele ya wabunge alisema kosa likifanywa, linasahihishwa. Limesahihishwa. La maana kwangu, la maana kwenu, na la maana nadhani kwa Watanzania wenye nia njema.
Sasa kama mnashindania Urais wa Zanzibar mshindanie, lakini la maana kwa nchi ni kwamba kitendo ambacho kilikuwa kinaweza kuhatarisha umoja wa nchi yetu kimeshasahihishwa na viongozi wetu. Wamekwishatoa statements (maelezo) katika hali ngumu kabisa, lakini wamejisahihisha. Sasa hilo kwa nchi ndio la maana. Sasa ninyi mkitana kufuata fuata hayo mengine, yafuateni, lakin imsinitumbukize.
SWALI: Mwalimu hebu fikiria hizi emotion (hisia) zinatokea wapi. Iko dhana kwamba hii ni rushwa tu. Watu wanakula bila hata kunawa. We waonaje mawazo kama haya ya Watanganyika?
JIBU: Mimi nasema hivi jambo hili nimefanya consultations (mashauri) limekwisha. Nimekaa na viongozi wetu. Mimi najua kwamba wabunge wamechachamaa huko. Lakini sababu ambazo mimi naziona ni relevant (muhimu kuhusiana na suala lenyewe) ni uvunjaji wa Katiba. Tabia ya kuvunja Katiba na OIC haikuwa peke yake. Mimi ningependa sana wabunge—na bila shaka watasema tu—kwamba OIC haikuwa peke yake. Sasa tuje kote tulikovunja turekebishe.
Lakini hili lilikuwa gumu zaidi kujisahihisha. Lakini madhali tumejisahihisha basi hayo mengine ambayo tulikuwa tunavunja Katiba sasa tufuate Katiba. Tuanzie hapo. Tujenge tabia ya kujenga upya kwa mujibu wa Katiba. Lakini wameniambia jana tu.
Mbunge amenipa orodha ndeeeefu ya corruption (rushwa). Majibu yake ni kuona Serikali ya Tanganyika? Kwa maana rushwa nchi hii ni ya Wazanzibari? Kwamba Bara hakuna watu corrupt (wala rushwa)? Ndivyo mnavyoamini kweli hivi?
Ndiyo maana nilikuwa nasema kuamini hivi ni sawa na kuamini kwamba Mbarbaig yuko karibu zaidi na mtu wa Bagamoyo culturally (kiutamaduni) kuliko mtu wa Bagamoyo na Pemba. Sasa corruption ni corruption na corruption huvunji nchi. Unadhibiti watu corrupt. Unadhibiti the corrupt. Huwezi kuzungumza kwamba … Hivi kweli Zanzibar iwe na serikali yake na Bara iwe na serikali yake. Hii mimi naona ni ku-miss point (kukosa hoja). Kama inaweza kufanyika chini yangu, na kama si chini yangu inaweza kufanyika chini ya serikali ya Tanganyika. Bado itafanyika tu corruption, na dawa yake ni kuwadhibiti hao. Dawa yake si kuzungumza kuwa na serikali tatu.
SWALI: Mwalimu, kumekuwa na matukio mengi ya namna hii (uvunjaji sheria na kanuni). Na kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale, hata katika mambo kadhaa ya utawala, ingawa mengine si ya uvunjaji sheria, kama ya uteuzi wa mawaziri wanaotoka Zanzibar kushika nyadhifa katika wizara zisizo za Muungano. Wewe kwa maoni yako unaona wapi kuna tatizo la kiutawala linalosababisha matukio na malalamiko kama haya sasa hivi na si kule nyuma ambako hata wewe ulikuwa unafanya uteuzi kama huo?
JIBU: (Baada ya kimya cha sekunde kama kumi hivi) Sijui. Mimi bado nasema nina matatizo ya Katiba. Katiba ya nchi lazima tujitahidi tuongozane kwa mujibu wa Katiba. Kwa mujibu wa sheria. Sheria nyingine ambazo si za kikatiba, lakini bado ndizo zinazotawala uongozi. Katiba ya nchi yetu hivi ilivyo sasa, na labda ngoja nieleze hilo.
Nchi zetu zilipoungana, Zanzibar na Tanganyika, na wakatai huo mimi jitihada yangu ilikuwa kushauri nchi za Afrika Mashariki zote. Kwa hiyo wakati Mapinduzi ya Zanzibar yanafanyika nilikuwa katikati ya Mazungumzo na Kenyatta (alikuwa Waziri Mkuu wa Kenya wakati huo), Obote (Waziri Mkuu wa Uganda) juu ya kuona kuwa nchi zetu zinaweza kuungana zikawa moja. Tangu kabla ya uhuru wa Tanganyika mpaka leo naamini. Basi historia imetufikisha hapo. Hivyo vitendo vya watu au maneno yao yatategemea hivyo wanavyojua na kumbe sivyo.
Mimi ningependa nijiite African (Mwafrika) na sana sana mtu wa Afrika Mashariki. Nilikuwa sitaki urais, nilikuwa naogopa … Matumaini yangu ilikuwa tutampata Kenyatta, manake mzee yule. Na mimi ambition (matakwa) yangu, kwa vile na mimi nilikuwa rais hapa, nilitarajia nitamwomba aniteue kama permanent representative (balozi) katika Umoja wa Mataifa (UNO). Nilitarajia niwe mwakilishi wa East African Federation (Shirikisho la Afrika Mashariki). Nawaambieni kabisa hiyo ndiyo iliyokuwa ambition yangu.
Lakini haikuwezekana. Sasa Zanzibar inafanya Mapinduzi tuko katika hali hiyo. Sasa Karume nilichomwambia, nilimwambia, tizama Karume sasa nimo kwenye mazungumzo kwamba wao watakapokuwa tayari sisi tuko tayari kuungana. Sasa na wewe nakwamba ukishakuwa tayari sisi tayari kuungana. Karume akaniambia, ‘vipi? Nini maana ya kuniambia nikiwa tayari? Waite watu wa magazeti, waite sasa hivi niko tayari.’ Na naendelea kusema bila yeye hakuna Tanzania. Si niliwaambia wakakataa. Hakuna East African Federation. Lakini yeye nilivyomwambia akaniambia “sasa hivi. Waite watu wa magazeti. Na we ndo rais’ na Karume akitaka serikali moja. Sasa mimi nikakataa. Ilikuwa matamko yale tuyafanye tarehe 17 Machi, lakini hatukuweza kwa sababu naogopa mimi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, naona afadhali niendelee na mazungumzo haya.
Hivyo, ingawa wengine walikataa, lakini Karume alikubali bila kusita na akaniambia ita watu wa magazeti. Hatukuungana siku hiyo. Na ndipo tukaja tukatangaza tarehe 26 Aprili mwaka 1964. Sasa kama ni federation ingekuwa ni pale nilipowataka wenzangu wale tuungane wakakataa. Lakini Karume alikubali pale pale. Hivyo, wakati huo tungeweza kuwa na serikali tano kutokana na kuwepo kwa Tanganyika, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Zanzibar.
Sasa tulipoungana na Zanzibar, ndipo tukawa na utaratibu wa baadhi ya mambo kuwa ya Muungano. Tukafanya mambo ya nje, ulinzi lakini tukaona polisi si lazima. Zanzibar wanaweza kuwa na polisi wao na Bara polisi wao. Lakini Karume akasema haiwezekani bwana, tuna Commander-in-Chief (Amiri Jeshi Mkuu) mmoja tu.
Hivyo tukaacha mambo mengine yaendelee kwa ajili ya historical identity (utambulisho wa kihistoria) yao. Kwa mujibu wa Katiba, Mzanzibari anaweza kuongoza wizara isiyo ya Muungano. Kwa mfano, waziri wa afya anaweza kusimamia afya kwa wote, yeye, na kuwa waziri wa afya tu.
Sasa kuhusu kosa liko wapi. Mimi nasema Katiba ni muhimu. Na kwamba ili viongozi wetu waongoze vizuri, hawana budi kuheshimu Katiba.
Lakini ninavyoelewa mimi kipo kifungu. Kipo kifungu katika Katiba—labda wakifute. Lakini ninavyoelewa kipo kifungu kinachomruhusu Rais ateue kama mimi nilivyofanya. Sina uhakika kama bado kipo au vipi, lakini mimi najua kilikukwepo kifungu ndani ya Katiba kinachomruhusu Rais kuteua Mzanzibari kushika madaraka katika wizara zisizo za Muungano. Na hazuiwi. Sasa kama mimi nilikuwa nafanya hivyo mkanyamaza, na mwenzangu anafanya, basi nyamazeni.
SWALI: Lakini kama unavyosikia watu wanapigapiga kelele. Kwa mfano kama watu watasema Rais Mwinyi ajiuzulu. Nini maoni yako?
JIBU: Rais Mwinyi, mtu yeyote akisema anataka ajiuzulu atataja sababu zake. Atasema sababu hii, sababu hii, sababu hii na raia wote sasa wata-argue (watajadili) kuona kama sababu hizo zina msimamo au sivyo. Mimi nazungumza habari ya Katiba ya nchi yetu. Usifikiri watu sasa … kama wangekuwa wanataka Rais Mwinyi ajiuzulu … mimi nafikiri hawakuelewa hivyo. Mimi nasema tuendeshe nchi yetu kwa mujibu wa Katiba.
Nchi hii iongozwe kwa mujibu wa Katiba. Kama watu wanaiendesha bila mujibu wa Katiba wanadhibitiwa. Tunajitahidi kuwadhibiti. Lakini kusema kweli hili wengi tunalikwepa. Tunataka ku-side (jitenga) pembeni tu. Jambo la msingi ni kujitahidi kuwaambia viongozi wetu kwamba mtaiendesha nchi kwa mujibu wa Katiba. Na mnapoivunja tunawadhibiti. Huu ni msingi wa kuendesha nchi ya watu huru.
SWALI: Kwanini Mwalimu tusiwaambie wenzetu wa Zanzibar kwamba kama ni Muungano basi tufanye Muungano wa serikali moja kuliko kukazania kuwa hawa wanamezwa?
JIBU: Mimi siwezi kusema zaidi ya nilivyokwishasema, nasema mtu mwenye nia njema na Tanzania, tunayo Katiba. Mimi naamini kwamba haina tatizo. Tatizo ni kwamba haitekelezwi. Kama Katiba hii ikitekelezwa kama ilivyokusudiwa, mimi nadhani itatosheleza hali ya kwamba hii ni nchi ya nchi ambazo zilikuwa mbili zikaungana. Inatosheleza kabisa ikitekelezwa.
Mtu mwenye nia nzuri na nchi yetu akisema Katiba hii haitoshi, atasema tuzungumze kwenda kwenye serikali moja. Hazungumzi kwenda kwenye serikali tatu hata kidogo. Serikali tatu itavunja nchi. Lakini nasema serikali moja, kwa sababu nia ya serikali moja ilikuwa ni lazima kukubaliana na Zanzibar. Serikali moja haiwezi kupitishwa tu sisi tunataka serikali moja.
Kwa sisi ndivyo tunavyotaka Bara. Kwa sababu matokeo yake ni yale yale kama vile serikali tatu zitakavyovunja Muungano. Madai ya serikali moja by (na) Bara peke yake yatavunja Muungano. Kwa sababu sasa mtafanya Zanzibar kuwa koloni. Hamwezi kufanya. Kwa hiyo kama mnataka kwenda kwenye serikali moja, mtaona wote Watanzania kwamba ya nini. Hii kung’ang’ania hapa serikali tatu zinaleta gharama, zinaleta misunderstanding (kutoelewana).
Wabunge hawa, wakati mwingine Bara wanadai kuwa na serikali yao. Kwa nini? Kwa nini tusiungane tukafanya serikali moja? Nimesema hivyo katika Bunge. Lakini hata mkikubaliana bado nawaambia watu wenye nia nzuri watasema lakini kweli Wazanzibari tutawafanya kama Lindi. Wana watu laki tano.
Lindi nayo ina watu laki tano. Hivi kweli nchi yenye watu laki tano, hata kama mkikubaliana kwa nia njema tu na Wazanzibari, nasema watu wenye busara watasema msiifanye Zanzibar kama Lindi. Na Zanzibar bado representation (uwakilishi) yake kwenye Bunge itakuwa tofauti na representation ya Lindi. Watu watakuja kuuliza baadaye mbona hawa Wazanzibari wako watu laki saba, wana watu wengi katika Bunge hili kuliko Lindi. Maelezo yatakuwa ni historical (ya kihistoria). Na ndivyo ilivyo duniani kote.
Wataambiwa kuwa huko nyuma nchi hizi zilikuwa mbili—Zanzibar na Bara. Haya ni matokeo ya hayo yaliyoziunganisha nchi hizo mbili. Wataelezwa hivyo. Kama tunavyoelezwa sasa Zanzibar kuwa na serikali yake pamoja na Zanzibar sasa hivi ndani ya Bunge ina representation ya peke yake. Ni tofauti kabisa na wengine. Hivyo bado hata kama mki-move kwenye serikali moja bado mtasema Zanzibar bado haina budi itendewe tofauti na Lindi. Lakini jambo mnalizungumza kama watu wazima wanavyoendesha nyumba yao, siyo kama bwana mkubwa mmoja anasema tumechoka na watu hao sasa tuwameze hasa. Haiwezekani. Haiwezekani hata kidogo.
SWALI: Mwalimu umesisitiza sana suala la kufuata Katiba. Lakini mimi naona ukija kwenye suala hili utaona kwamba ni vigumu sana kudhibiti kama Rais akiamua kuwa dikteta. Kwa mfano, pale bungeni wabunge wanaweza kudadisi suala kwa undani linachukuliwa kijanjajanja. Na kunachukuliwa uamuzi wa kupiga kura na mle kuna mawaziri, wakuu wa mikoa na wabunge wa Taifa. Kwa hiyo unakuta mara zote serikali inashinda tu—kama hili suala la OIC kule Dodoma. Ingawa wabunge walidadisi sana, lakini serikali hatimaye ilishinda na ikawaacha wabunge na malalamiko yao. Sasa ni vipi utawadhibiti madikteta?
JIBU: Mimi nasema hivi bwana, tunazungumza hapaa sasa hivi, lakini msifikiri kwamba mambo haya mimi kuyazungumza ni rahisi sana kuyasema kama hivi. Rais Mwinyi ni successor wangu (kachukua madaraka kutoka kwangu). Na nilipokuwa natoka niliwaelezeni sifa zake. Anazo sifa nyingi. Moja nilisema ni mpole sana. Sidhani kama nilisema ni mpole mno, nilisema ni mpole sana.
Na hiyo nasema mpaka sasa ni mpole sana. Na mambo ya nchi hayapendi upole sana. Siku nyingine lazima uwe rough (madhubuti) na watu—hasa wahalifu. Rais ni mpole. Rais Mwinyi kwa vyovyote vile hawezi kuwa—huwezi kum-accuse (shutumu) kwa dictatorship (udikteta). Unaweza kum-accuse kwa kitu kingine. Udikteta hata kidogo. Hakuna mtu anayemjua yeye, akasema sasa niko mbele ya dikteta. Actually (kwa kweli) mimi, mtu angeweza kusema huyu … Mimi wangenionea, lakini wangeweza kufanya hivyo. Lakini Rais Mwinyi hapana.
Ila nawaambieni. Nawaammbieni kuwa njia kubwa ya kuzuia udikteta ni kuongozwa na sheria. Na hamwezi kuongozwa na sheria kama hilo linakuwa siyo wito wa Taifa. Taifa zima linaelewa. Ni taifa la watu huru, na kwamba wote ndivyo wanavyosema. Na wale viongozi wanapokiuka, wanakemewa na taifa bila woga. Na mimi sidhani kama jitihada zangu zote hizi ilikuwa ni kujenga Taifa la watu waoga sana. Haikuwa nia yangu. Kama inatokea hivyo, basi nasema Mwenyezi Mungu anisamehe.
Saa kwa hiyo msingi wa kwanza kabisa ni kuona kwamba viongozi wetu wanatutawala, wanatuongoza kwa kufuata sheria. Sheria zinawabana hivyo. La pili ni kuona kwamba viongozi wetu wanatuongoza kutokana na maamuzi ya vikao. Ndiyo maana ya demokrasi. Maamuzi ya demokrasi yanatokana na vikao.
Ziko tabia mbili sasa hivi. Moja, ni kujaribu kukwepa vikao. Sasa kwa mfano, jambo la kuamua suala la OIC lisizungumzwe kwenye vikao. Mimi najua Rais alishauriwa hivyo na watu wasiopenda mazungumzo haya (ya vikao). Sasa tabia hii isizoewe ya kuzuia vikao kuzungumza. Ndiyo maana hata katika Bunge, wakati tunazungumza, na kwamba Mwalimu pengine ingekuwa vyema ungekuja katika Bunge. Lakini hata kidogo. Isiwe kwamba ni mbinu za ujanjaujanja mimi nizuie wabunge kusema mambo haya. Hata kidogo. Tuzungumze tu mambo haya.
Mambo ya nchi lazima yazungumzwe waziwazi katika vikao rasmi vilivyowekwa. Hivyo, lazima jitihada kwamba tunasimamia tusimamie. Nchi yetu inaendeshwa na Katiba. Maamuzi makubw aya nchi yanatokana na vikao. Central Committee (Kamati Kuu) kwenye Chama, National Executive (Halmashauri Kuu ya Taifa) maana Chama hiki ndicho kinachotawala. Na mpaka sasa kila nikitazama sioni kingine, ni hicho hicho.
Basi chama hicho kiendelee kuwa na tabia ya kuwa maamuzi yake yanafahamika katika vikao. Kwani kwa sasa hivi maamuzi ya chama hicho bado ni kitu kizito sana. Sasa Central Committee inazungumza mambo, National Executive inazungumza mambo, lakini kuna ujanja wa kuepusha mazungumzo. La Makamu (wa Rais) liliepushwa. La OIC nadhani halikufikishwa kabisa. Nadhani halikufika kabisa kabisa.
Na Bunge lilipotaka kuzungumza ikawepo janjajanja ya kuwatoa pale. Hizi ndizo dalili za dictatorship. Na lazima zikemewe. Hapana kuwa na uamuzi wa janjajanja hivi. Nchi haiongozwi kwa ujanja hata kidogo. Nchi inaongozwa kwa msimamo. Inaongozwa kwa taratibu zinazojulikana kabisa kabisa. Watu wanakutana katika Central Committee wanaelewana, wanatenda jambo. Na kama kuhitilafiana, wanahitilafiana saaana katika jambo la msingi. Wengine wana-resign (jiuzulu). Ndiyo. Waziwazi kabisa na wanaeleza kwa nini wana-resign.