29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

GIGGY MONEY SAWA… VIPI VIDEO ZA NJE ZISIZO NA MAADILI?

Na RAMADHANI MASENGA

TANZANIA kama ilivyo mataifa mengi duniani, ina maadili yake. Maadili ya taifa ndiyo yaifanyayo jamii ijue iishi kwa misingi gani ili thamani na hadhi ya utaifa wao uendelee kudumu.

Maadili ya jamii ya Tanzania yako mengi ila miongoni mwao ni pamoja na heshima kwa wakubwa na wadogo, heshima juu ya kila dini iliyopo, kuvaa mavazi ya stara na kuongea lugha isiyokwaza wengine.

Wizara iliyopewa kusimamia maadili, ni Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambayo ipo chini ya Dk. Harrison Mwakyembe na naibu wake, Juliana Shonza.

Wiki kadhaa zilizopita, Rais wa nchi, Dk. John Magufuli alioneshwa kukwazwa na mavazi ya nusu utupu ambayo huwa yanavaliwa na baadhi ya wasanii wa kike. Kimsingi tamko la Rais ni agizo kwa walio chini yake.

Na hapa wizara inayohusiana na sanaa na utamaduni haikulala. Juzi tumeona Naibu Waziri, Juliana Shonza akishirikiana na Basata wakianza kufanyia kazi tamko la Rais kwa vitendo.

Kwa kuanza kuna baadhi ya wasanii wameitwa Basata  kuonywa na wengine kufungiwa. Katika kundi hilo wapo kina Pretty Kind na Gigy Money. Mwanzo mzuri.

Kitendo hiki kinatoa picha namna wizara hii ilivyoamua kwa makusudi kupambana na wavunjifu wa maadili. Kwa miaka mingi wazazi na walezi wamekuwa wakilalamika aina ya maneno na mavazi yanayotumiwa na wasanii wetu.

Mavazi na maneno hayo kwa kiwango kikubwa yamekuwa sababu ya mmomonyoko wa maadili kwa sababu sanaa hususani muziki husambaa kwa kasi ya umeme. Hivyo kama yapo ya kupotosha yanafika haraka na kama yako ya kuelimisha halikadhalika yanafika haraka.

Ila pamoja na yote hayo, wizara na Basata haitakiwi kuishia kwa kina Giggy Money na wasanii wa ndani tu. Wizara inatakiwa kufika mbali zaidi na kukagua tathimilia na muziki kutoka nje.

Itakuwa haina maana kufungia kina Giggy Money wakati runinga za ndani zinaonesha video za wasanii wa Magharibi wakiwa wamevaa nusu utupu huku tamthilia zisizo na maadili pia zikioneshwa kila kukicha.

Tamthilia zilizobeba maudhui ya kishoga zinaoneshwa na watoto wadogo wanaziangalia. Katika hili wizara inatakiwa kuwa macho. Unaweza kumfungia Giggy na wengine ila bado ukakuta maadili ya taifa lako yanabomoka kutokana na aina ya maudhui ya nyimbo na tamthilia zinazooneshwa.

Binafsi najua Dk. Mwakyembe ni mtu makini. Ni mzalendo halisi mwenye kulipenda taifa lake. Kwa uzalendo alionao, basi inafaa ajue kuwa kuna tamthilia hata vikaragosi (Cartoon) vinavyooneshwa katika runinga zetu zikiwa na maudhui ya kishoga na kisagaji.

Wakati akipambana na wasanii wa ndani katika kulinda na kuimarisha maadili yetu, anapaswa atambue kuna kazi pia ya kuangalia vya nje visije vikaua maadili yetu kwa makusudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles