Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amewaomba wakuu wa mikoa na wilaya nchini kusimamia usambazwaji wa mbolea zinazoingia katika mikoa yao ili kuhakikisha zinawafikia wakulima vijijini kwa bei iliyopangwa na serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Tizeba, alisema ni vema wafanyabiashara wasimamiwe ili wasiuze mbolea kinyume na bei elekezi.
“Nawaomba wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanisaidie katika kusambaza mbolea hii hadi vijijini ambako kilimo ndipo kinapofanyika, wakulima hawaishi katika makao makuu ya mikoa wala wilaya hivyo ipo haja ya kulisimamia hili la usambazaji,” alisema Dk. Tizeba.
Mapema mwaka jana serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilitangaza utaratibu wa kuagiza mbolea kwa pamoja na kuweka bei elekezi katika mbolea za kupandia na kukuzia ambapo mbolea ya DAP haitakiwi kuuzwa zaidi ya Sh 56,000 na UREA isizidi Sh 48,000.
Dk. Tizeba, alisema bei hiyo elekezi inatofautiana na maeneo kulingana na umbali kutoka jijini Dar es Salaam.
“Mbolea ipo ya kutosha kiasi cha tani 28,000 na ina uwezo wa kufika kwa wakulima wote msimu mzima, lakini lazima iwepo nidhamu ya kuisambaza ili iwafikie walengwa vijijini ambako ndiko kilimo kinapofanyika,” alisema Dk. Tizeba.
Alisema mbolea inazidi kwenda katika mikoa yenye uhaba na kuwahakikishia kuwa itawafikia walengwa kwa wakati kwa sababu magari yanayoisafirisha yamepewa ulinzi maalumu na askari.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Lazaro Kitandu alisema mbolea ipo kwenye maghala licha ya upungufu ulijitokeza baadhi ya mikoa ya Rukwa na Katavi.
“Siyo kwamba mbolea haikuwepo Rukwa bali iliyokuwepo ilichukuliwa yote hivyo kukawa na uhaba, lakini tayari mipango imewekwa sawa mbolea itafika kila eneo.
“Haya maeneo mengine ambayo mtandao wa usambazaji ni mkubwa kuna hawa wanaoitwa mawakala ambao si wa serikali, wapo kwa ajili ya kuhakikisha inawafikia wakulima,” alisema Lazaro.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Sumbawanga mkoani Rukwa, mkulima wa mahindi, Josephat Mwananjelwa alisema tayari wameshaanza kuona magari ya mbolea yakiwasili kwa msururu hali inayowaongezea matumaini ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Wiki iliyopita Rais Dk. John Magufuli alitoa agizo kwa Waziri Tizeba ahakikishe mbolea inawafikia wakulima.