BAADA ya mchakato mrefu, mkali na wenye kila aina ya miiba ya kuwania kumrithi Rais Jacob Zuma kukiongoza Chama tawala cha African National Congress cha Afrika Kusini, hatimaye Rais ajaye wa Taifa hilo amefahamika juzi.
Wajumbe wa kongamano la Taifa la chama hicho walimchagua Naibu Rais Cyril Ramaphosa kuwa kiongozi wao baada ya kumshinda mshindani wake wa karibu, Nkosazana Dlamini-Zuma.
Dlamin-Zuma ni waziri wa zamani wa Taifa hilo na aliyekuwa Mke wa Rais Zuma, akiwa ametokea hivi karibuni kuiongoza Tume ya Umoja wa Afrika.
Licha ya umaarufu wa ANC kupungua kutokana na wimbi la kashfa za ufisadi bado kina uungwaji mkono mkubwa nchini humo na hivyo kwa ushindi huo chamani, Ramaphosa anatarajia kuwa Rais wa Taifa hilo litakapoendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2019.
Rais Zuma ambaye aliingia madarakani akimrithi Thabo Mbeki, amekuwa akiandamwa na kashfa za ufisadi katika sehemu kubwa ya uongozi wake.
Na kumekuwa na jitihada za kumvua madaraka na kumburuza mahakamani ambazo zimekuwa zikigonga mwamba.
Kinyanganyiro hiki cha uongozi kilikutanisha watu sita ingawa ni hawa mafahari wawili waliokuwa wakiangaliwa zaidi.
Kwa ushindi wake, Ramaphosa amenufaika na utamaduni wa muda mrefu wa chama hicho unaoshuhudia Naibu wa Rais, akija kuwa Rais tangu Taifa hilo liachane na mfumo wa ubaguzi wa rangi katika miaka ya 1990.
Lakini pia Dlamini- Zuma (68) anaaminika ameangushwa kutokana na kuhusishwa na jina lililochafuka la Zuma, ambapo pia wakosoaji wake walidai huenda akaendeleza sera za mtalaka wake huyo, ambazo zimesababisha uchumi kuporomoka.
Dlamini-Zuma, ambaye wakati wa kampeni za kuwania urais wa ANC, aliahidi kupambana na kile alichosema kutokuwapo usawa wa rangi alizaa na Rais Zuma watoto wanne kabla ya kutalikiana mwaka 1998.
Vita ya uongozi ilisababisha siasa za kupakana matope na kuibua hofu ya kukimega chama hicho kabla ya uchaguzi huo mkuu ujao, hali iliyowalazimisha wote wawili kujitokeza mara kadhaa kuwatuliza wanachama na wafuasi wao, wakihimiza umuhimu wa umoja na mshikamano chamani.
Ramaphosa, ambaye alishinda kwa kupata kura 2,440 dhidi ya 2,261 za Dlamini-Zuma wakati wa kongamano hilo juzi, kipindi cha kampeni zake alizungumzia namna atakavyopambana na ufisadi na anaungwa mkono na jumuiya ya wafanyabiashara.
Ramaphosa (65), ni mfanyabiashara na alikuwa mwanaharakati wa kutetea maslahi ya wafanyakazi kabla ya kujitosa katika siasa.
Vyama vya upinzani vya Democratic Alliance (DA) na Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa kitengo cha Vijana ANC, Julius Malema vinatarajiwa kutumia sakata za ufisadi zilizoukumba utawala wa Rais Zuma kujipigia debe 2019.
Tukiachana na hilo, makusudio ya makala haya yamejiegemeza kwa Ramaphosa, ambaye ni moja ya visababishi vinavyoshuhudiwa sasa kwa miungano yenye nguvu ya vyama vya wafanyakazi nchini humo kuwa na ushirika wa kisiasa na ANC.
Wakati Ramaphosa alipokuwa kijana mdogo alimwambia rafiki yake kuwa siku moja atakuwa Rais.
Ndoto hizo zilizojiwekea zimekuwa zikiandamana naye kipindi chote cha shughuli zake katika miungano ya vyama vya wafanyakazi, kama msuluhishi wa kikatiba na kama mfanyabiashara.
Kwa sasa amebakiza ‘mkia’ kutimiza ndoto yake hiyo baada ya kuweza kumla ngombe mzima, wakati ANC itakaposhinda Uchaguzi Mkuu wa 2019
Wapi anakotokea?
Ushawishi wake wa awali ulianzia katika vuguvugu la kujitambua kwa weusi katika Chuo Kikuu cha North, ambako alikuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Kikristo.
Yeye na wengine kama kijana Frank Chikane, walipigia debe kisiasa vuguvugu hilo na kuziba pengo lililoachwa wazi na kusambaratishwa kwa uongozi wa vuguvugu la utambuzi wa weusi kulikofanywa na polisi katika miaka ya 1970.
Ramaphosa akajikuta akitumikia kizuizini mara mbili kwa harakati zake ndani ya vuguvugu hilo la weusi.
Aliibuka kutoka kizuizini akisema: “Wakati nilipokuwa kizuizini, nilikuja baini kuwa marafiki ni kama pakiti za majani ya chai, unachemsha maji na unayatumia mara moja,”
Baada ya kukamilika shahada yake ya sheria akawa mratibu wa Cusa, vuguvugu la muungano wa wafanyakazi wa kujitambua kwa weusi.
Ni kutokea hapo akaja endesha vyama vya wafanyakazi wa migodini na kisha kuvifanya kuwa sehemu ya ANC baada ya kuvutiwa na uimara na endelevu wa ANC katika mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu.
Wengi wa vijana kujitambua kwa weusi ambao waliondoka Afrika Kusini kwenda kuishi uhamishoni walirudi kwa ajili ya ufufuo wa harakati hizo.
Ni baada ya kuona hali ya vuguvugu za ukombozi hasa zilizohusiana na vyama vya siasa kama vile PAC na Azapo kuwa katika hali mbaya, kutokana na kumalizwa na utawala wa kikaburu.
Waligeukia ANC, ambayo kulinganisha na nyingine ilikuwa ikiendeshwa vyema, ikiwa na rasilimali za kutosha pamoja na balozi zilizotapakaa Afrika na Ulaya.
ANC ilitoa mafunzo kwa kikosi chake cha wapigania uhuru na lengo lake kuu ni kutwaa madaraka siku moja kutoka kwa utawala kandamizi.
Ramaphosa alikuja kivingine katika harakati za kisiasa kwa kuuleta Muungano wa Taifa wa Wafanyakazi wa Migodini (NUM) ndani ya ANC.
Zaidi ya hayo, NUM ikaja kuwa moja miungano ya wafanyakazi yenye mwelekeo wa kisiasa zaidi na iliyoiunga mkono ANC waziwazi katika Taifa hilo.
Alishiriki kikamilifu katika kuundwa kwa Cosatu, akiwa Rais mwasisi wa mkutano uliosababisha kuundwa kwa Muungano huo wenye nguvu kabisa nchini humo wa wafanyakazi alihakikisha unaiunga mkono ANC na kuwa vuguvugu kubwa la kidemokrasia.
Ramaphosa akawa sehemu ya watu muhimu ndani ya vuguvugu hilo walioweka mawasiliano na viongozi wa ANC walio uhamishoni.
Alikutana na kuwa karibu na kiongozi wa Chama cha Kikomunisti Afrika Kusini (SACP), Joe Slovo na viongozi wengine kama Mac Maharaj.
Viwanja vya machimbo, ambako wafanyakazi walilala katika mashimo ya zege, ililindwa na walinzi binafsi na yalikuwa maeneo ambayo viongozi wa wafanyakazi hawaruhusiwi kufika.
Lakini Ramaphosa aliweza wakati fulani kushawishi menejimenti za migodi kuruhusu watu wake na kupageuza kuwa eneo marufuku kwa utawala wa kampuni za madini na hivyo NUM ikakua na kushamiri.
Kufikia katikati ya miaka ya 1980, NUM ikawa chama kikubwa zaidi cha wafanyakazi na kuanza kujitangaza chenyewe.
Mwaka 1987, Ramaphosa aliuongoza muungano huo katika mgogoro mkubwa kabisa wa kikazi, mgomo wa wafanyakazi wa migodini uliodumu kwa miezi mitatu, mwishoni hakukuwa na mshindi.
Wafanyakazi walishindwa kufanikiwa mengi ya madai yao na kampuni za madini zilitikisika vibaya mno kifedha.
Lakini mgomo huo ulimpaisha vilivyo Ramaphosa katika majukwaa ya kitaifa. Miongoni mwa walioanza kumfuatilia walikuwa wafungwa wa gereza la Kisiwa cha Robben kama vile marais wastaafu Kgalema Motlanthe na Marehemu Nelson Mandela.
Ramaphosa akaja kukutana na Mandela kabla ya kuachiwa kwake kutoka jela na wawili hao wakajenga ukaribu hadi Mandela wakati ananusa hewa ya uraiani mwaka 1990………..
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA.