Na Elizabeth Kilindi-Njombe
SERIKALI mkoani Njombe, imeokoa zaidi ya Sh bilioni 7 katika ujenzi wa mradi wa barabara unaojengwa kwa ufadhiri wa benki ya dunia kwa kiwango cha Lami kutoka Nyigo-Igawa.
Utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Bil 103.2 unaojengwa na Kampuni ya China Railway Groups(CRSG) unatokana na uadilifu ,uwazi pamoja na jitihada za wataalamu hasa wakala wa barabara Tanroad mkoa wa Njombe pamoja na mkandarasi anayejenga mradi huo.
Akikagua ujenzi wa barabara hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasilano na Uchukuzi, Elias Kwandikwa alisema ameridhishwa na uzalendo kwa hatua iliyofikiwa na mkandarasi pamoja na Tanroad katika kutekeleza mradi huo kwa kurejesha serikalini bakaa ya fedha zaidi bilioni 7.
Katika hatua nyingine naibu waziri huyo aliwataka wakandarasi wazawa kujifunza kwa kampuni hiyo kwani imekuwa ni mara ya kwanza kampuni kurejesha serikalini bakaa ya fedha.
“Wakandarasi wazawa igeni mfano huu ulioonyeshwa na hawa wakandarasi wa kigeni ambao wamefanya kazi ya serikali kwa uzalendo na kurudisha kile kilichobaki katika ujenzi huu,” alisema Kwandikwa.
Meneja wa Tanroad Mkoa wa Njombe, Yusuph Mazana alisema kuwa pamoja na kampuni hiyo kufanya kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na wakandarasi wengine lakini pia imefanikiwa kumaliza ujenzi kabla ya muda uliopangwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Mazana alisema kuwa barabara hiyo inatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali Agosti 22, 2018 itakapokamilika.