MAZOEA ya baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali nchini kujisaidia katika maeneo ya wazi ikiwamo vichakani, porini na katika vyanzo vya maji, yanaendelea kuiweka jamii hatarini kwa kuwa ni sababu kuu ya maradhi.
Hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya kuharisha, kipindupindu na yale yanayotokana na maji machafu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya taifa ya usafi wa mazingira mkoani Dodoma wiki iliyopita, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa Tanzania hupoteza kiasi cha Sh bilioni 400 kwa kutibu maradhi yanayotokana na kukosekana kwa matumizi ya vyoo.
Makamu wa Rais alisema kuwa takwimu nchini zinaonesha watu wapatao 30,000 huugua magonjwa ya kuhara kila mwaka na baadhi yao hupoteza maisha. Idadi ya wanaougua ni sawa na wastani wa wagonjwa 83 kwa siku moja.
Alisema hapa nchini asilimia 40.5 pekee ya kaya ndizo zenye vyoo bora ambapo kaya zipatazo 600,000 hazina vyoo kabisa.
Wakati tatizo la ukosefu wa vyoo likiendelea kuathiri pato la taifa, tunafarijika kwamba kupitia awamu ya kwanza ya kampeni ya usafi wa mazingira, jumla ya kaya 1,662,550 zilijenga vyoo bora katika vijiji na mitaa ipatayo 6,628 na pia shule za msingi 2,133 zimejenga vyoo bora kwa kuzingatia mahitaji ya jinsia.
Kinachotupa faraja zaidi ni taarifa ya makamu wa Rais kwamba Serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ya kupambana na maradhi ya kuambukiza na kwamba usafi wa mazingira ni njia mojawapo.
Kama alivyosema Makamu wa Rais, hatuwezi kuzungumzia kujenga uchumi wa viwanda na kuelekea uchumi wa kati kama bado kuna kundi la wananchi wanakosa huduma ya vyoo bora, tena hata vile vya gharama.
Inashangaza kuona katika karne hii ya sayansi na teknolojia, bado kuna watu hawajaona umuhimu wa kuwa na vyoo na badala yake wanaendelea kujisaidia kandokando mwa bahari, mito na katika vichaka vilivyopo pembeni mwa nyumba zao.
Pamoja na kuhatarisha afya zao, matumizi ya wananchi kujisaidia maeneo ambayo hayakutengwa ni hatari, jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua za haraka.
Kutokana na kuripotiwa kwa vitendo hivyo katika meneo mengi nchini, ni wazi kuwa tatizo hilo ni kubwa na linahitajika kuchukuliwa hatua za makusudi ili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kutokea.
Ni wazi kama kaya nyingi nchini bado hazitumii vyoo si jambo la kufumbia macho na wala halikubaliki kwa mtu yeyote.
Kutokana na mazingira hayo, si ajabu kusikia kila kukicha upo uwezekano wa wananchi kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu ambacho kwa kweli kinaweza kuondoa uhai wa mtu wakati wowote.
Tunatoa wito kwa viongozi wa wananchi katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini pamoja na timu zao za afya kujipanga vizuri  kwa kuanzisha mikakati ya makusudi na ya haraka kukabiliana na tatizo hili.
Tungependa kuona viongozi hawa wanachukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hili. Ni aibu dunia ya leo wananchi kukosa vyoo wakati kila siku Serikali inatoa maelekezo.
Sisi MTANZANIA, tunasema hili si jambo la kupuuza, ndiyo maana tunawataka Watanzania kupambana na adui wa afya kwa kutunza mazingira na kuepuka viashiria vya magonjwa mbalimbali badala ya kulalamika ukosefu wa dawa kwani kinga ni bora kuliko tiba.