26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ATAKA UCHUNGUZI ASKARI WALIOUAWA DRC

Na PATRICIA KIMELEMETA

SERIKALI imeutaka Umoja wa Mataifa (UN), kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha vifo vya wanajeshi 14 wa Tanzania waliouawa wiki iliyopita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema wanajeshi hao waliuawa na askari waasi wa ADF kutoka Uganda wakati wa majibizano ya risasi yaliyodumu kwa saa zipatazo 13.

Majaliwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa kuaga miili ya askari hao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Tunaitaka UN ifanye uchunguzi wa kina, wa wazi na wa ukweli tuweze kubaini chanzo cha mauaji hayo kwa askari wetu, na uchunguzi huo ufanywe kwa haraka iwezekanavyo.

“Pamoja na vifo vya askari wetu, bado Watanzania wataendelea kuwaombea majeruhi 44 walioumia kwenye mapigano hayo waweze kupona na kuendelea na majukumu yao kama kawaida,” alisema Majaliwa.

Pamoja na shambulio dhidi ya askari hao, Majaliwa alisema Tanzania haitakata tamaa katika masuala ya ulinzi, bali itaendelea kusonga mbele katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ilianza kulinda amani katika nchi mbalimbali baada ya kupata uhuru mwaka 1961, kuzisaidia zipate uhuru.

Alizitaja nchi ambazo Tanzania imepeleka askari wake kwa ulinzi wa amani kuwa ni DRC, Lebanon na Sudan na kwamba katika nchi hizo, askari hao wanasifiwa kutokana na nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji wao.

Katika mazungumzo yake, Majaliwa aliishukuru UN kwa jinsi ilivyoshirikiana na Serikali, JWTZ na ndugu wa marehemu tangu maafa hayo yatokee wiki iliyopita.

“Naishukuru UN kwa jinsi walivyoshirikiana na sisi na nasema Tanzania itaendelea kujivunia kuwa na askari wenye weledi na uadilifu kutokana na kazi wanazozifanya.

“Kwahiyo, nawaomba Watanzania tuungane pamoja katika kipindi hiki cha majonzi na tuwafariji wafiwa kwa kuwa wako katika kipindi kigumu,” alisema.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema pengo lililoachwa na askari waliofariki dunia, haliwezi kuzibika kutokana na umuhimu wao.

“Tunaungana na ndugu na jamaa wa askari hawa katika kipindi hiki cha msiba tuweze kuhuzunika nao. Lakini hatutakatishwa tamaa na tukio hili, bali tutaendelea kusonga mbele katika majukumu yetu,” alisema Dk. Mwinyi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alisema maafa hayo ni ya kwanza kutokea tangu JWTZ ianze kulinda amani katika mataifa mbalimbali na hivyo utafanyika uchunguzi wa kina kujua chanzo cha tukio hilo.

“Tukio hili linatisha zaidi kwa sababu halijawahi kutokea katika kipindi chote cha kutekeleza majukumu yetu katika kulinda amani nchi mbalimbali.

“Lakini hatuwezi kukata tamaa, bali tumeongeza morali wa kupambana zaidi,” alisema Jenerali Mabeyo.

Wakati wa kuaga miili ya askari hao, viongozi mbalimbali walikuwapo, akiwamo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Mstaafu wa uliokuwa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), Salim Ahmed Salim.

Wakati hayo yakiendelea Dar es Salaam, Mkuu wa Majeshi Zanzibar, Meja Jenerali Sharif Othman, amesema shambulio dhidi ya askari wa JWTZ, linaongeza moyo wa kufanya kazi na kamwe hawatarudi nyuma.

Aliyasema hayo jana katika hafla ya kuaga miili ya wanajeshi hao iliyofanyika katika Kambi ya Jeshi Migombani, Zanzibar.

“Tumepoteza roho za wanajeshi wetu waliokuwa tegemeo katika kutekeleza majukumu ya kazi zetu, lakini hatutarudi nyuma hadi hapo DRC itakapokuwa salama,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles