28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI MBUNGE CHADEMA KUJIUZULU

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

KUDHOHOFIKA kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumepamba moto baada ya Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (Chadema), kutangaza kujiuzulu ubunge na kujiunga na CCM.

Dk. Mollel amechukua uamuzi huo zimekuwa zimepita siku chache baada ya aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF), kutangaza uamuzi kama huo.

Akizungumza jana kupitia video fupi na tamko lake alilolitoa kwa umma, Dk. Mollel, alisema kuwa amevutiwa na uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, hasa katika kupigania rasilimali za nchi.

“Nimeamua kwa dhati ya moyo wangu kujivua uanachama kuanzia leo (jana) na kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge.

“Huu ni uamuzi wangu mwenyewe, nimeufanya nikiwa na akili timamu, najua watu wa Siha hili litawashtua, lakini muamini kwamba mlinituma niwe jicho lenu, nimetizama nimeona, maamuzi niliyoyafanya hamtakuja kujuta,” alisema Dk. Mollel.

Alisema aliomba ridhaa ya ubunge kwa ahadi ya kupigania rasilimali za nchi, hivyo ameona hana namna nyingine zaidi ya kuungana na CCM katika jukumu hilo.

“Wakati naingia kwenye harakati za kugombea ubunge, niliamini kwamba pamoja na kupigania Wilaya ya Siha kupata maendeleo, lakini nitatumia fursa hiyo kulinda rasilimali za taifa letu.

“Dhamira yangu imeshindwa kuukataa ukweli huu, kuwa hivi sasa uongozi wa nchi yetu chini ya CCM umedhihirisha wazi kupigania rasilimali za nchi.

“Nimeona mbali katika maamuzi haya, kikubwa ninachotegemea wana – CCM mnipokee ili tuweze kupambana kulinda nchi na rasilimali zake,” alisema.

MTANZANIA ilimpomtafuta kwa simu yake ya kiganjani ili kusikia sauti yake na kupata ufafanuzi wa kina kuhusu uamuzi wake huo, simu yake iliwekwa katika mfumo wa kutumika wakati wote.

Alipotafutwa mmoja wa watu wake wa karibu, alisema kwa sasa mbunge huyo yupo mkoani Dodoma ingawa haikueleweka anafanya nini.

Dk. Mollel ambaye pia ana historia ndefu kisiasa, aliwahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na UVCCM Wilaya ya Siha.

Hata hivyo, mwaka 2015, aliondoka rasmi ndani ya CCM na kutangaza kujiunga na Chadema ambako alifanikiwa kugombea ubunge wa Siha na kushinda dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Agrey Mwanri.

CHADEMA

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema sababu alizotoa Dk. Mollel hazina mashiko.

“Kama ameamua kufanya hivyo ni jambo la kushangaza kwa sababu mtu hawezi kusema anaweza kulinda rasilimali kwa kuondoka bungeni wakati Bunge ndilo lenye mamlaka ya kulinda rasilimali za taifa… sasa huyu anakimbia bungeni anakuja uraiani, sijui atatumia miujiza gani.

“Tunawashauri wote ambao wanajitoa waeleze sababu halisi na si kuhadaa umma kwa sababu uchwara,” alisema Mrema.

Hata hivyo, alisema hatua ya wapinzani kuhama vyama na kujiunga CCM ni jambo la muda tu na chama chao kitaendelea kuwa imara.

“Kuna upepo unapita, ni jambo la muda, Chadema tuko imara na tutaendelea na ajenda zetu bila kuyumbishwa na wimbi hili la watu wachache ambao wameamua kuwasaliti wapigakura wao kwa sababu zao binafsi.

“Tutaendelea kujenga taifa na chama chetu bila kujali njaa za baadhi yetu, wale wenye dhamira thabiti ndio wataweza kufika mwisho wa safari salama,” alisema.

KAULI YA CCM

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema kuhama chama ni haki ya kikatiba, lakini akasisitiza kuwa wanaotaka kuhama wawe ni wale wanaokubali sera, siasa na itikadi ya chama hicho.

“Tunampongeza Dk. Mollel na bado tuna wabunge na madiwani wengi zaidi, tunawafunga breki wasije, lakini tukisema tufungulie usajili, vyama hivi vitakosa watu,” alisema Polepole.

Wabunge waliojiuzulu hadi sasa na vyama vyao kwenye mabano ni aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM) na Maulid Mtulia wa Kinondoni (CUF).

Mtulia alitangaza kujiuzulu ubunge na nafasi zote za uongozi ndani ya CUF Desemba 3, mwaka huu.

Watu wake wa karibu na Mtulia, walidai kuwa mbunge huyo alikuwa akikabiliwa na masuala kadhaa ndani ya CUF.

MTANZANIA ilipomtafuta Mtulia na kuzungumza naye, alisema wote wanaomzushia mitaani kwa uamuzi wake, wanasumbuliwa na povu.

Alisema ameamua mwenyewe kwa hiari yake na si suala linalohusu madeni yake. Kwamba amevutiwa na uchapakazi wa Rais Magufuli.

Alipoulizwa kama atawania tena jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, alisema anasubiri kupangiwa na wakubwa wake, lakini kwa sasa hawezi kujipangia.

Na hata alipoulizwa ni kwanini kila kiongozi au mwanachama akitoka upinzani anasema ni kwa sababu anamuunga mkono Rais Magufuli, alisema ni lazima iwe hivyo.

“Hivi unafikiri inakuwa kwa ajili ya nani? Ni Magufuli kutokana na utendaji wake na ndiyo msimamizi na mtekelezaji wa shughuli zote ndani ya chama changu nilichokiona kinafaa.

“Hakuna mwingine ni yeye na huwezi kukwepa kumpa sifa hizo,” alisema Mtulia.

Uamuzi huo wa Mtulia walibarikiwa na CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, na kusema kuwa wameridhia kujiuzulu kwake huku wakimtakia safari njema katika siasa.

Taarifa iliyotolewa  na kusainiwa na Naibu Mkurugenzi wa CUF, Mbarala Maharagande, chama hicho kilitarajia hayo mapema na wala hakikushtushwa kutokana na taarifa za intelijensia walizopata.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Elimu ndogo shuleni na kimaisha ya kujiendeleza na kuelewa.pia uvivu wa kufikiri. Wengi wao hawaelewi mfumo wa vyama vingi unakuwaje. Kama alivyosema yule dada si sawa na kubadilisha shati au kiatu kama wanavyofikiri.ufahamu wao kuhusu namna ya kufikiri, kuamini, na kuishi hawana ueleo wa hali ya juu. Sijawahi ona nchi hata moja duniani watu wakahama vyama kwa kuigana , hadharani kama chupi bila kujiheshimu.Ni mfumo duni wa hali ya kisiasa hasa kutoka ccm. Ni chama kimekaa madarakani toka tupate uhuru ingawa kimebadili jina. Lakini mfumo wa kufikiri toka wakati huo ni duni. Ni ndio au hapana. Kujionyesha hadharani kwa vishindo. Kupewa kanga za bure vijijini, vilemba na hongokwa kujipatia kura nyingi. Watu wako radhi kuuza utu wao, kuuza uhuru wao, kuuza hadhi zao kama wanazo au hawana hawajijui. Kuuza uzalendo na maendeleo ya nchi kwa uchu wa madaraka na kuonyes j wa hadharani imekuwa sifa kubwa kupewa sifa mbele za umati wa watu na hasa mbele ya ndugu Magufuli. Ni kama mtoto asiyejiamini akitafutwa sifa na kupendwa.Bado Taifa liko nyuma kielimu kujijua wengi wetu ingawa tunaelimu za juu lakini hatujiamini wala hatjajijenga kuwa huru na kujipa ajira wenyewe na kujivunia kile kidogo tilichokivuna kwa jasho letu. Tunajilinganisha kiutajiri wa kupeana, wizi, na udanganyifu na kufichiana siri. Ndo maana tumekwama kujikomboa kiuchumi wa kweli nchini. Imekuwa rushwa, hongo, wizi, na ufisadi ndani ya ccm toka juu mpaka chini. Kama hupo kwenye mfumo huo upo nje ndo maana watu wapo radhi kujiunga na ccm ingawa hawaamini lakini watasaidiwa kichama kiupendaleo badala ya kunyanyasika, kuonewa, wanachukua short cut.sababu ukiwa nje ya mfumo utapata mateso makubwa. Kwa mfumo huu Tanzania haitakomesja rushwa, ufisadi, wizi, wala kujiinua kiukweli. Bado tutakuwa vibaraka licha ya kuwa na elimu. Hatuna uzalendo wa kweli, umebaki wa maneno matamu, na kujionyesja majukwaani kama cinema. Hatujui kuzitumia elimu zetu kwa hadhi, ushujaa, na majivuno. Bado ni vibaraka tu. Soni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles