32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AMWASHIA MOTO KIGOGO WAZAZI

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA


RAIS Dk. John Magufuli, amemtupia lawama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Maalim Seif, kwa sababu hajawahi kumpa majina ya watu wanaotakiwa kuteuliwa katika nafasi mbalimbali.

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimshutumu kiongozi huyo mjini hapa jana, wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa jumuiya hiyo.

“Jumuiya ya Wazazi sikupata orodha ya ninaoweza kuwateua na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi yupo hapa, asimame aseme kama aliniletea orodha ya majina.

“Najaribu kuzungumza hapa kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu na ni lazima nimtangulize Mungu mbele.

“Ninataka niwaeleze kwamba mnaweza mkazungumza kwamba wengine sikuwateua, lakini eleweni kwamba Jumuiya ya Wazazi na UWT ilikuwa ni tatizo zaidi.

“Kwa sababu orodha ya wale waliopendekezwa niwateue haikuletwa, ilikuwa vigumu kujua nimteue yupi kwa sababu CV zao sina.

“Kwa sababu waliokuwa viongozi wa UWT hawakuwa na lengo la kuisaidia UWT, lengo lao lilikuwa ni kusaidia maisha yao kwa sababu waliwekwa na watu kwa ajili ya shughuli za watu,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, alisema kuanzia sasa katika nafasi atakazokuwa akiteua viongozi, atakuwa na idadi sawa kutoka katika kila jumuiya za CCM.

“Hili ombi la ninaowateua kuwa katika idadi sawa, nitaangalia taratibu zote zitakavyokwenda,” alisema.

 

ELIMU

Kuhusu suala la shule za jumuiya hiyo, Rais Magufuli alisema anajua jumuiya hiyo ina shule 54 na kwamba Serikali itaendelea kuzinunua ili jumuiya ipate fedha za kuendesha miradi mingine.

“Kama mtaona inafaa kwa baadhi ya shule ambazo mmeshindwa kuziendesha, hasa hizi 54, mkaamua shule 10 ama 20 zichukuliwe na Serikali, sisi tutazichukua ili mpate fedha za kuendesha miradi mingine,” alisema.

 

RUSHWA

Akizungumzia kuhusu rushwa, alisema wagombea watakaotoa rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo, wasipigiwe kura kwa sababu hawafai.

“Katika chaguzi hizi huwa kuna mambo mengi, yakiwamo yanayoitwa msimamo, kwamba msimamo wetu ni fulani.

“Kutokana na msimamo huo, mtu fulani akawaita katika Hoteli ya Mwanga Bar, mkapewa msimamo. Katika hili, ninachotaka kuwaomba wajumbe, ni kwamba msikubali mtu akuchagulie mtu kwa sababu mimi ambaye ni mwenyekiti wenu wa chama, nilichaguliwa na wanachama wala sikuchaguliwa na mtu.

“Msikubali pesa zikawachagulia watu, fedha itakayoletwa kwako hiyo ni zawadi yako kwa sababu haiwezi kuwa sawa na thamani yako, na mkichagua watu kwa sababu ya hisani, majuto mtakuja kuyaona.

“Inawezekana zamani walikuwa wakichagua watu kwa sababu ya maelekezo, lakini sasa kama mnataka kuleta mabadiliko, wapigieni wale watakaowatetea.

“Chagueni watu watakaosimamia kazi za jumuiya, kwa sababu hata mimi sina mtu kama ilivyo kwa Katibu Mkuu, Kinana na Mangula ambao nao hawana mtu hapa. Napenda ‘message’ hii iwafikie wote kwa sababu vijana huwa wanasema ‘message sent and delivered’,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles