WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametegua kitendawili kuhusu hatima ya madai ya wananchi katika mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Lukuvi amesema kutokana na hali hiyo kuanzia sasa kila mwananchi mwenye kiwanja au nyumba yake atalazimika kuuza kiwanja chake kwa bei anayoitaka au kujenga nyumba kwa mujibu wa ramani ya mji mpya
Akizungumza na wananchi hao juzi katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam, Lukuvi, alisema sintofahamu iliyokuwapo ilitokana na hapo awali wananchi kutowekwa wazi kuhusu mchakato wa uuzaji wa maeneo yao.
“Wananchi wamekuwa katika sintofahamu juu ya uuzaji wa maeneo yao, wengine mnafikiri Serikali ndiyo itakayonunua ardhi yenu na wengine mnafikiri ardhi inadalaliwa na Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni (KDA),” alisema Lukuvi na kuongeza;
“Hakuna Serikali itakayouza ardhi wala KDA kudalalia ardhi yenu…wananchi wa Kigamboni ndiyo mtakaoamua juu ya uuzaji wa ardhi yenu na serikali itakuwa mwangalizi ili wananchi wasiibiwe kwa kuuza bei ya chini sana,” alisema Lukuvi huku umati huo ukimshangilia.
Alisema wananchi wanachotakiwa ni kuchagua mambo matatu katika mpango huo ambayo ni kuuza ardhi yao wenyewe moja kwa moja kwa wawekezaji, kuingia ubia na wawekezaji na kutafuta fedha za kujenga wenyewe.
Alisema kama mwananchi ataamua kujenga mwenyewe atatakiwa kufuata ramani na mpango wa mji mpya unavyoonyesha.
“Mtu anaweza kuamua kujenga mwenyewe lakini si kwamba unaamua kujenga unachotaka bali utajenga kilichopo kwenye mpango, haiwezekani eneo la kujenga majengo makubwa ya biashara wewe ujenge choo,” alisema Lukuvi.
Alisema ili kuhakikisha wananchi wanatekeleza mambo hayo matatu ni lazima wapatiwe hatimiliki za maeneo yao suala ambalo awali halikuwapo kwa madai kuwa hakuna haja ya kutoa hati kwa eneo ambalo tayari lipo kwenye mpango.
“Katika suala la kutoa hati nilipingana na watu wa Mipango Miji na nikawaambia lazima wananchi wapewe hati zao ili wakati wa kufanya makubaliano na wawekezaji wawe na ushahidi wa kumiliki ardhi hiyo,” alisema Lukuvi.