32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa walia kuibiwa sera yao ya elimu

suzan-lyimo-april25-2013Na Arodia Peter, Dodoma

KAMBI Rasmi ya Upinzani bungeni imesema Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiba sera yake ya elimu inayozungumzia elimu bure kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.

Mbali na hilo, wapinzani wameonya makada wa chama hicho wanaotangaza nia ya kuwania urais kuacha kutumia sera hiyo ya upinzani kwa sababu walikuwa Serikalini tangu uhuru na wameshindwa kufanya hivyo.

Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo bungeni jana kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Msemaji Mkuu kwa kambi hiyo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo, alisema elimu haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za CCM kwa awamu zote za utawala wake na ndiyo maana imeshindwa kutekeleza hata Ilani yake ya uchaguzi.

“Sera ambayo CCM imepigia upatu kwa miaka yote 53 ya uhuru na ambayo pia imeshindwa kutekeleza ni kilimo, ndiyo maana tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere sera zilizosikika ni Siasa ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa na sasa Kilimo Kwanza. Hatujawahi kusikia elimu kwanza kwa utawala wa CCM kwa miaka yote 53 ya Uhuru,” alisema.

Suzan ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) alisema sera ya elimu kwanza ni ya upinzani na kwamba ipo katika ilani ya uchaguzi ya Chadema ya mwaka 2005 na 2010 na imepewa kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu.

“Itakumbukwa kwamba Chadema iliposema elimu bure kama ingechaguliwa kuunda serikali mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda chafu ya kuwapotosha wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure.

“Lakini ili kuthibitisha ile methali isamayo kwamba njia ya muongo ni fupi, CCM hivi sasa imekubali kula matapishi yake na kusema katika kipengele cha 3.1.5 cha sera mpya ya elimu ya mwaka 2014 kwamba elimu itakuwa bure,” alisema na kuongeza:

“Huu ni uthibitisho kuwa CCM imebobea katika wizi hadi kufikia hatua ya kuiba sera ya upinzani waziwazi bila aibu. Ukawa ikitwaa madaraka ya dola katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu itakuwa bure.”

Sera mpya ya elimu

Kuhusu sera mpya ya elimu, alisema imekuwa hazitekelezeki kwa kuwa ni sera bainishi na imekuwa ikibainisha upungufu pekee na kuacha sehemu ya utekezaji.
Alisema ili sera hiyo iweze kutekelezeka ni lazima kuwapo na walimu bora, zana bora za kufundishia na walimu wenye motisha.

“Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuandika vizuri sera zake, lakini utekelezaji wake ni shida. Mfano sera hii haielezi ni kwa kiasi gani itaondoa ubaguzi au matabaka ya elimu hasa viwango vya elimu. Pia haielezi nini maana ya kufuta ada ikiwa kuna michango mingi kuliko ada yenyewe,” alisema.

Dk. Kawambwa

Awali akiwasilisha hotuba yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imetekelezwa.

Alisema sekta ya elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mikakati hiyo.

Dk. Kawambwa aliainisha vipaumbele vya sekta ya elimu vilivyomo katika mwongozo wa taifa wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2015/2016 kuwa ni
pamoja na kuongeza upatikanaji wa fursa ya elimu kwa usawa katika ngazi zote za elimu na mafunzo, kuinua ubora wa elimu na kujenga stadi stahiki, kuimarisha taasisi za usimamizi wa ubora wa elimu na ufuatiliaji na tathmini ili zitekeleze majukumu yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles