Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), leo vinatarajiwa kutoa msimamo endapo vitashiriki uchaguzi mdogo wa majimbo matatu Januari mwakani. Vyama hivyo vitatu ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi,
Majimbo hayo ni Songea Mjini (Ruvuma), Singida Kaskazini (Singida) na Longido mkoani Arusha.
Taarifa za awali ambazo MTANZANIA ilizipata zilieleza kuwa vyama hivyo vinatafakari kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo kwa kile vinachodai kuwa demokrasia inaminywa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, vyama hivyo vya upinzani vilisononeshwa na uchaguzi wa marudio wa madiwani uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita kwa kile vilichodai ulitawaliwa na ubabe wa polisi.
Katika taarifa yake jana, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema vyama hivyo vitazungumza na waandishi wa habari kujadili mustakabali wa masuala muhimu ndani ya nchi hususan mwenendo wa siasa.
Hata hivyo, mkutano huo ambao ulipangwa kufanyika jana katika hoteli ya Colosseum Oysterbay, Dar es Salaam, uliahirishwa ghafla.
Hiyo ni mara ya pili kuahirishwa mkutano na waandishi wa habari. Juzi Chadema ilitoa mwaliko kwa vyombo vya habari kwamba kingetoa taarifa kuhusiana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichomalizika hivi karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari waliofika katika hoteli hiyo kwa ajili ya mkutano huo jana kuwa mkutano hulo uliahirisha kwa kuwa majadiliano yalikuwa hayajakamilika.
“Tunaomba mtuwie radhi, kuna maazimio ambayo tuliyafikia lakini kuna wenzetu wamechelewa hatujawa-brief, hivyo muda huu tunarudi kwenye kikao ili tuwa-brief.
“Tukisema muondoke halafu mrudi baadaye tutakuwa tunawasumbua, tunaomba tukutane kesho (leo) kwa ajili ya mkutano huo,”alisema Mwalimu.