25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WA CHADEMA WARUDISHWA MAHABUSU

Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO

WABUNGE wawili wa Chadema, Suzan Kiwanga wa   Mlimba na Peter Lijualikali wa   Kilombero, wamerudishwa mahabusu.

Wabunge hao  waliofikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro  kusikiliza maombi ya rufaa yao jana, walirudishwa tena mahabusu baada ya hakimu anayesikiliza kesi yao  kuugua.

Kiwanga na Lijualikali, wanashtakiwa pamoja na wanachama wengine 37 wa Chadema.

Kutokana na ugonjwa wa hakimu anayesikiliza shauri hilo, Ivan Msack jana, kesi hiyo ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi, Erick Rwehumbiza huku upande wa mashtaka ukihusisha Mawakili wawili wa Serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki.

Upande wa utetezi ambao sasa una mawakili watano, unahusisha mawakili Peter Kibatala, Bartholomew Tarimo, Ignas Punge, Fredirick Kiwelo na John Nyabinyiri.

Wakati shauri hilo likiendelea, Wakili wa Utetezi, Kibatala, aliiomba mahakama hiyo iruhusu watu kuingia mahakamani  wajue kinachoendelea kwa kuwa kesi hiyo ina mvuto kwa wananchi.

Pia, wakili huyo aliomba kesi hiyo ipangiwe kwa hakimu mwingine kwa kuwa haijulikani Hakimu Msack atapona lini.

Akijibu hoja hizo, Hakimu Rwehumbiza alisema kama kesi hiyo itahamishiwa kwa hakimu mwingine, kuna uwezekano mkubwa ikachukua muda mrefu kuanza kusikilizwa kwa kuwa kuna utaratibu mrefu wa kuanza kuisikiliza.

Alisema washtakiwa wanaweza kukaa muda mrefu mahabusu bila sababu za msingi tofauti na ilivyo sasa.

Hakimu Rwehumbiza aliahirisha kesi hiyo hadi kesho na washtakiwa walirudishwa mahabusu.

Kiwanga, Lijualikali na wenzao hao  walifikishwa mahakamani hapo Novemba 30, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la uchochezi, kuchoma nyumba na ofisi ya ofisa mtendaji wa Kata ya Sofi iliyoko Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, Novemba 26, mwaka huu.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao, washtakiwa hao waliyakana na kurudishwa mahabusu.

Juzi, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Devotha Minja, walihudhuria kesi hiyo   kuona mwenendo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles