32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP: TUTAIANGAMIZA KOREA KASKAZINI VITA IKIZUKA

NEW YORK, MAREKANI

UTAWALA wa Rais Donald Trump umesema Marekani haitakuwa na namna nyingine zaidi ya kuiangamiza Korea Kaskazini iwapo vita itazuka kutokana na ukaidi wa taifa hilo kwa jumuiya ya kimataifa.

Utawala huo pia umeyataka mataifa yote kukatiza uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Korea Kaskazini ili kuitenga isipate kiburi zaidi kutokana na kufanyia jaribio kombora lake la masafa marefu kinyume na onyo la kimataifa.

Akizungumza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), mjumbe wa Marekani katika baraza hilo, Nikki Haley alisema jana kuwa Rais Donald Trump amemtaka mwenzake wa China kusitisha usambazaji wa mafuta kwa Pyongyang.

Amesema Marekani haitaki mzozo lakini Korea Kaskazini inafanya uchokozi hivyo itaangamizwa iwapo vita vitazuka.

Onyo hilo linajiri baada ya Pyongyang kufanyia majaribio kombora lake la kwanza katika kipindi cha miezi miwili.

Korea Kaskazini imesema kombora hilo lililorushwa siku ya Jumatano ambalo ilisema liliruka kimo cha kilomita 4,475, ikiwa ni mara 10 zaidi ya kimo cha kituo cha angani.

Madai hayo hata hivyo, hayakuweza kuthibitishwa na wataalamu wa makombora, ambao wametilia shaka uwezo wa taifa hilo kuwa na teknolojia kama hiyo.

Hata hivyo, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kwa namna ya kujivunia, alisema uzinduzi wa kombora hilo ulikuwa wa kufana.

Jaribio hilo likiwa mojawapo ya majaribio yaliyofanywa na taifa hilo limeshutumiwa na jumuiya ya kimataifa na tayari UNSC imeitisha kikao cha dharura.

Haley alionya kuendelea kwa uchokozi wa taifa hilo la kikomunisti kunalenga kuliyumbisha eneo hilo.

“Tunahitaji kuona China ikichukua hatua zaidi,” alisema.

Mapema juzi, Rais Trump alimpigia simu Rais Xi Jinping wa China, akimtaka kuchukua hatua za kuishawishi Korea Kaskazini kusitisha uchokozi na kusitisha mpango wake wa nyuklia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles