25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

VIAZI VITAMU VINAWEZA KUMWEPUSHA MTOTO NA UTAPIAMLO, UDUMAVU

Na ASHA BANI


LISHE duni ni chanzo cha magonjwa na vifo kwa watoto. Kila siku watoto 130 hupoteza maisha kutokana na kukosa lishe bora.

Lishe duni hudumaza ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili na hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni na kukosa ufanisi maishani mwake.

Asilimia 42 (zaidi ya milioni tatu) ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini wamedumaa kutokana na lishe duni kabla ya kuzaliwa hadi miaka miwili baada ya kuzaliwa.

Ripoti zinaonesha kuwa udumavu umefikia takribani asilimia 40 kwa watu wote, huku asilimia 20 ikiwakumba watu wenye kipato kikubwa kifedha.

Takwimu hizi zinaashiria kwamba chanzo cha udumavu ni zaidi ya upungufu wa chakula na umaskini.

Upungufu wa Vitamini A hudhoofisha kinga mwilini na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto.

Ripoti ya Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania ya mwaka 2010, inaonesha kuwa takribani asilimia 40 ya watoto wa umri wa kati ya miezi 5 na 59 hawakuwahi kula vyakula vyenye Vitamin A kwa wingi ndani ya saa 24 kabla ya kufanyika kwa utafiti.

Akizungumzia suala la lishe bora, Meneja Miradi ya Utetezi na Sera kutoka taasisi isiyo ya Serikali ya Health Promotion Tanzania (HDT), Greysmo Mutashobya anasema asilimia 33 ya watoto walio chini ya miaka mitano nchini wamedumaa. Wakati huo huo watoto milioni 652 wenye umri chini ya miaka mitano duniani wamedumaa, jambo linalohatarisha maendeleo.

Naye Mratibu wa Mradi kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA), Jane Msagati anasema Tanzania bado inakabiliwa na tatizo la utapiamlo na udumavu.

Anasema sera ya serikali ifikapo 2020 ni kupunguza ama kumaliza kabisa tatizo la utapiamlo.

Anasema tatizo hilo  likiachwa liendelee Serikali itaendelea kupoteza Sh bilioni 815 kila mwaka.

Kwa upande wake Sikitu Kihinga kutoka  Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), anasema utapiamlo huwaathiri zaidi watoto walio chini ya miaka mitano, wajawazito na wanaonyonyesha kutokana na mahitaji yao ya lishe kuwa makubwa.

“Hakuna asiyefahamu kwamba  mamilioni ya watoto na kina mama  hupatwa na matatizo ya kuwa na udumavu, ukondefu, upungufu wa Vitamin A, upungufu wa madini joto na upungufu wa wekundu wa damu (anemia),” anasema na kuongeza kuwa serikali inapambana kuhakikisha tatizo hilo linakwisha.

Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation, chini ya mradi wa usambazaji wa haraka mbegu bora za mazao ya mizizi kwa wakulima wadogo wadogo kwa viazi vitamu na muhogo waliandaa miongozo.

Miongozo iliyotolewa ni pamoja na walimu shuleni, kuendelea kufundisha umuhimu wa lishe, ambapo chakula kilichopewa kipaumbele ni viazi vitamu.

Mtafiti Mkuu wa Kituo cha Utafiti Mikocheni jijini Dar es Salaam (MARI), Dk. Joseph Ndunguru anaelezea historia fupi kuhusu utafiti uliofanyika kwenye viazi lishe.

Anasema mwaka 2000 walianza na mradi huo katika nchi za Uganda na Kenya, kwa kutumia vikundi vya wakulima na shule za msingi.

“Wakulima wengi waliopokea mbegu hizo baada ya mafunzo walipata mafanikio makubwa na baadaye jitihada zikaelekezwa nchini Tanzania.

“Mwaka 2008 kulikuwa na mradi wa viazi lishe katika Kanda ya Ziwa, ambapo wakulima walifundishwa juu ya umuhimu wa viazi lishe, jinsi ya kuvizalisha na kuvitunza,’’ anasema Dk. Ndunguru.

Anasema watafiti  waliangalia changamoto mbalimbali za magonjwa zilizopo nchini Marekani na kuzifananisha na Tanzania kama viazi lishe vitaweza kustahimili ukame.

Anasema tafiti hizo zilifanyika katika maeneo ya Pwani, Nyanda za juu Kusini maeneo ya ukanda wa Ziwa, Iringa na Ruvuma.

Anasema mafaniko waliyoyapata yamesababisha gunia moja la viazi vitamu viuzwe gunia moja kwa Sh 50,000 wakati mwaka uliopita vilikuwa vikiuzwa Sh 30,000 ambapo mkulima anaweza kutoa magunia zaidi ya 100.

Anasisitiza kuwa viazi lishe vina faida nyingi mwilini, pia husaidia kukuza pato la Taifa na uchumi wa mkulima.

Mtafiti mwingine kutoka MARI, Mariam Mtunguja anasema kina wanga, husaidia kuondoa tatizo la upungufu wa Vitamin A kumwepusha mtoto na utapiamlo.

Anasema viazi vitamu vyote vina viini lishe vya Vitamin C, E, K pamoja na kundi la vitamin B, lakini vile vyenye rangi ya chungwa vina vitamin A zaidi.

Anasema tafiti zinaonesha kuwa kiasi cha gramu 125 ambacho ni nusu kikombe cha chai kwa viazi vilivyochomwa au kuokwa vina uwezo wa kukidhi mahitaji ya vitamin A ya watoto na wajawazoto.

Anataja faida nyingine ya viazi lishe kuwa ni kusaidia kuona vizuri na kujikinga na maradhi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles