NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) umeipa siku saba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ufumbuzi wa namna watakavyoandikishwa katika daftari la kudumu la kupigia kura kupitia mfumo wa BVR, kwa kuwa kuna mwingiliano na ratiba za masomo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa TSNP, Shitindi Venance, alisema wanaiomba NEC ieleze jinsi gani wanafunzi walioko vyuoni na wale walioko sekondari za bweni ambao wana sifa za kupiga kura watakavyoandikishwa kutokana na ratiba za uandikishaji kupishana na zile za vyuo na za sekondari.
Alisema kumekuwepo na changamoto kubwa kwa upande wa wanafunzi nchini zinazosababisha kutofahamu hatma ya uandikishwaji wao.
“Mtandao huu umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu mchakato wa uandikishwaji tangu kuanza kwake kupitia matawi yake yaliyoko Njombe, Ruvuma, Mtwara na Mbeya na kubaini kuwa kundi la wanafunzi limekuwa na changamoto kubwa.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uandikishwaji unaendelea wakati huo huo wanafunzi wakiendelea na ratiba zao za masomo, huku wengine wakiwa shule za bweni,” alisema Venance.
Alisema ni bora NEC ikapeleka mashine za BVR katika kila taasisi ya elimu kwa ajili ya uandikishwaji wa wanafunzi wakiwa katika taasisi zao.