Na JOHANES RESICHIUS -DAR ES SALAAM
SERIKALI imeshauriwa kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za binadamu katika mapambano yake dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi.
Ushauri huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland Van der Geer, katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa ‘Tuungane Kutetea haki’ unaofadhiliwa na EU, wenye lengo la kuongeza uelewa wa wananchi katika kukabiliana na tatizo la rushwa na kuongeza uwajibikaji katika ngazi za halmashauri.
Balozi Van Geer pamoja na kutambua mchango wa Rais Dk. John Magufuli na Serikali yake katika kupambana na rushwa, alitaka jitihadi hizo zizingatie uwazi na uwajibikaji.
“Rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo na dawa yake ni uwazi, tunatambua mchango wa Rais Dk. Magufuli katika kushughulikia vitendo vya rushwa hivyo mapambano hayo yawe endelevu na yafuate sheria, utawala bora na kuzingatia haki za binadamu.
“Pia kitendo cha Serikali kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi za rushwa na mafisadi na kupitishwa kwa mpango mpya wa kupambana na rushwa, hizo ni jitihada kubwa sana na EU inaahidi kuendelea kuunga mkono mapambano hayo,” alisema Van der Geer.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi unaotekelezwa na Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS), Maria Kayombo, alisema mradi huo unalenga kuongeza ulewa wa wananchi kukabiliana na rushwa na kuwa na uwezo wa kuhoji masuala mbalimbali kwa viongozi hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji kuanzia ngazi ya mitaa hadi halmashauri.
“Mradi utawajengea wananchi uwezo wa kushiriki kwenye michakato ya maendeleo kama vile kuibua, kupanga, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Serikali inatoa taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo,” alisema Maria.
Alisema mradi huo utatekelezwa ndani ya miaka miwili kuanzia 2017 hadi 2019 ukihusisha zaidi ya kata 1,000 kwenye wilaya 40 na mikoa 7 ya Tanzania Bara na kugharimu Sh bilioni 2.5.