JENNIFER ULLEMBO NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
WAKATI klabu ya Yanga ikiendelea kusajili nyota wake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans Van der Pluijm, amewashtukia viongozi wa timu hiyo akieleza anahisi baadhi ya wachezaji waliosajiliwa hadi sasa hakuwapendekeza katika ripoti yake.
Klabu hiyo hadi sasa imefanikiwa kupata saini za wachezaji watatu ambao ni Deus Kaseke aliyetoka Mbeya City, Haji Mwinyi wa Zanzibar na Benedicto Tinoco kutoka Kagera Sugar.
Akizungumza na MTANZANIA jana kutoka Ghana, Pluijm alisema mbali na wachezaji hao, pia amepata habari za chini chini kuwa viongozi wanaosimamia masuala ya usajili wamepanga kuongeza wachezaji wengine ambao hawapo kwenye listi yake.
“Habari zote za usajili zinavyoendelea nazipata na nafuatilia kwa umakini, tayari nimeanza kugundua mambo yanaenda tofauti na nilivyopanga,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo ambaye anatarajiwa kurejea nchini Juni saba mwaka huu, alisema hatasita kufanya mabadiliko pindi atakapowasili na kugundua wachezaji waliosajiliwa hawana kiwango.
“Tukiharibu kwenye usajili ndiyo basi, hakuna tena muda wakuanza kurekebisha hasa ukizingatia tunakabiliwa na mashindano ya kimataifa na lazima msimu ujao tutetee taji letu la Ligi Kuu. Ukikosea kufanya usajili mara baada ya msimu kumalizika ujue utabeba mizigo hadi msimu mwingine kwani hata usajili wa dirisha dogo ni wamaboresho,” alieleza Pluijm.
Alisema yeye ni mwalimu hivyo anajua mapungufu ya timu hiyo, kama viongozi watafanya kinyume timu itakapoboronga asilaumiwe kwa lolote.
Pluijm ameeleza atakaporudi nchini atavianika vifaa vipya alivyopendekeza kutua Jangwani, ambapo anatarajiwa kurejea nchini wiki ijayo tayari kuanza mazoezi ya kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
Pluijm tayari amehakikisha kiungo mchezeshaji raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima na beki Mrundi Mbuyu Twite wanaendelea kuitumikia klabu hiyo.
“Kwa sasa nipo mapumzikoni, ni vigumu kuzungumzia mambo ya wachezaji wapya wanaosajiliwa Yanga kwa ajili ya msimu ujao, lakini mambo yatakuwa mazuri zaidi tukakapoanza mazoezi Juni 8, mwaka huu,” alisema.
Mbali na Niyonzima na Twite, klabu hiyo pia imemsainisha mkataba wa miaka miwili kipa, Deogratius Munishi ‘Dida’ ambaye alikuwa akiwaniwa na watani wao wa jadi Simba.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pia wanawania saini ya winga Haroun Chanongo, kuziba pengo la Mrisho Ngassa aliyejiunga na klabu ya Free State ya Afrika Kusini na kusaini mkataba wa miaka minne.
Pluijm alisema ana mipango ya kuandaa kikosi imara kitakachoonyesha ushindani katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, ili kiweze kufika mbali zaidi ya hatua waliyofikia kwenye Kombe la Shirikisho.
Hakuna mchezaji mpya wa kulipwa aliyesaini Yanga, licha ya uongozi wa klabu hiyo kukiri kuwa na majina saba mezani wakiwemo walioomba wenyewe na walioitwa kwa majaribio.