Raia wanne wa Ethiopia wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja kutokana na kukiri shtaka la kuingia na kuishi nchini bila kibali.
Washtakiwa hao wamehukumiwa leo Novemba 21, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambaye aliwataja washtakiwa hao Zainabu Aleul, Mulugeta Asifa, Amana Ally na Adame Hudar.
Washtakiwa hao baada ya kukiri mashtaka waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu walikuwa wanakwenda nchini Afrika Kusini kwa lengo la kutafuta maisha kutokana hali ngumu ya kiuchumi.
Walidai ni wakulima na kwao kuna ukame hivyo walishindwa kulima na kuamua kutoka kutafuta maisha kwa kuwa wanafamilia na wazazi wanaowategemea.
Raia hao wanadaiwa kuwa  Novemba 3, mwaka huu katika ofisi ya Uhamiaji Ilala, Dar es Salaam waliingia na kuishi nchini bila kibali.