Na AZIZA MASOUD ALIYEKUWA MBEYA
WAKALA wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ni taasisi ya serikali inayojishughulisha na masuala mbalimbali ikiwemo kupima kemikali mbalimbali na vinasaba vya binadamu (DNA) .
Ofisi hiyo makao yake makuu yapo Dar es Salaam, kwa sasa imeamua kujitanua katika mikoa kwa mgawanyo wa kikanda lengo ikiwa kuwafikia wananchi.
GCLA ambayo inaongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele, imegawanyika katika kanda sita zinazohudumia mikoa mbalimbali.
Kanda hizo ni kanda ya Kusini yenye ofisi zake mkoani Mtwara ambayo inahudumia Mtwara na Lindi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye ofisi zake mkoani Mbeya na inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa, Njomben Ruvuma na Katavi, nayo ofisi Kanda ya Kati iliyopo Dodoma inayotoa huduma Dodoma, Singida na Morogoro.
Mbali na hizo, GCLA ina ofisi katika Kanda ya Mashariki yenye ofisi yake Dar es Salaam inayohudumia Dar na Pwani wakati Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara. Ofisi ya Kanda ya Ziwa iliyopo Mwanza inahudumia Mwanza, Singida, Simiyu, Mara, Tabora, Kigoma na Geita.
Kati ya kanda sita kanda tatu za Kusini, Mashariki na Kanda ya Kati zimeanzishwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Profesa Manyele.
Katika ofisi zote hizo, wafanyakazi GCLA wamekuwa wakipewa vyumba vichache vya kufanyia shughuli zao katika majengo mbalimbali ya Serikali.
Ili kuondoa adha hiyo, Mkemia Mkuu amejenga ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Iwambi mkoani Mbeya.
Ujenzi wa ofisi hiyo katika majengo ya hospitali ya Wilaya ya Mbeya umegharimu Sh Milioni 402, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya ofisi hiyo.
Kaimu Meneja wa Kanda hiyo, Gasper Mushi, anasema jengo hilo katika eneo la Iwambi lina lengo la kuboresha shughuli za utoaji huduma za kimaabara zinazofanywa na ofisi hiyo.
“Uwepo wa jengo hili utasaidia kusogeza huduma za kimaabara karibu, mfano vipo vipimo ambavyo tunalazimika kuvipeleka Dar es Salaam katika maabara kuu, hii ni kwa sababu tu hatuna eneo la kutosha la kuhifadhia vifaa vya maabara,” anasema Mushi.
Anasema usafirishaji wa sampuli za maabara kwenda Dar es Salaam unasababisha baadhi ya sampuli kuharibika njiani wakati wa kuzisafirisha.
Mbali ya shughuli hizo, ofisi hiyo pia inajishughulisha na kutoa ushauri wa masuala mbalimbali ya kimaabara.
Jengo hilo jipya ambalo ujenzi wake umeshakamilika, lipo katika taratibu za kuunganishiwa umeme linatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwakani likiwa na vifaa mbalimbali vya maabara ikiwemo mashine ya kupimia vinasaba vya binadamu (DNA).
Anasema kiutaratibu mteja anapaswa kupata majibu ya huduma anayoihitaji ndani ya siku 14 kama hakutakuwa na vikwazo na kama atakuwa amefuata taratibu.
“Sisi tunazingatia mkataba wa huduma ambao unataka ndani ya siku 14 watu wapate majibu kama taratibu zote zitakuwa zimefuatwa sawasawa hasa katika mazingira ambayo kunakuwa hakuna matatizo ya kiufundi kama ya umeme,” anasema Mushi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, akizungumzia kuhusu umuhimu wa maabara hiyo, anasema inasaidia kutatua migogoro mbalimbali inayotokea katika hospitali hizo ikiwemo matukio ya wazazi kubadilishiwa watoto.
“Ofisi inawasaidia wazazi ambao watoto wao wamezaliwa na utata, wale wenye wasiwasi kwamba huyu mtoto ni wangu au amebambikiwa huwa wanakuja kuhakiki hapa kupimwa kipimo cha DNA. Wapo wanaobadilisha watoto wanapokuwa wodini huwa wanakuja kupima kwa kutumia kipimo hicho hicho na wanapata suluhu,” anasema Dk. Mhina.
Anasema mbali na hilo uwepo wa ofisi hiyo katika jengo hilo kunasaidia hospitali kupunguza gharama kutokana na kusaidiana kulipia baadhi ya gharama zikiwemo umeme.
Anasema miaka miwili iliyopita walipatiwa Sh milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kupitishia wagonjwa.