23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAKILI DK.TENGA KIZIMBANI KWA KUTAKATISHA FEDHA

KESI: Wakili Maarufu wa kujitegemea Dk. Ringo Tenga (kulia) na aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Peter Noni (wa pili kulia) na wenzake wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi, Dar es Salaam jana. Picha na John Dande

NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

WAKILI maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakurugenzi wenzake wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidh Shamte na Peter Noni, wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha Dola za Marekani zaidi ya milioni tatu.

Ni mara ya kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufungua mashtaka ya kutakatisha fedha katika tuhuma za kukwepa malipo kwa mawasiliano ya simu za kimataifa.

Washtakiwa hao na mwenzao, Noel Chacha ambaye ni Ofisa Mkuu wa Fedha, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Waliposomewa shtaka la kutakatisha fedha, miguno ilisikika kila kona kwa waliofika kusikiliza kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Jackline Jantori, akisaidiana na Jehovanes Zakari, waliwasomea washtakiwa mashtaka matano yanayowakabili.

Akisoma mashtaka, Nyantori alidai shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote wanne na Kampuni ya Six Telecoms, ambao wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016, Dar es Salaam kwa nia ya kupata fedha walidanganya kwa kutoza kiwango cha chini ya Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa mawasiliano ya simu za kimataifa.

Shtaka la pili, washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho, kwa udanganyifu na kwa nia ya kukwepa malipo, walishindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kama kodi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

“Mheshimiwa hakimu, shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote, wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016, walishindwa kulipa ada ya uendeshaji Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

“Mheshimiwa, shtaka la nne linawakabili mshtakiwa wa kwanza mpaka wanne, ambao kwa pamoja wanadaiwa walitenda kosa la kutakatisha fedha Dola za Marekani 3,282,741.12, huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la udanganyifu,” alidai Nyantori.

Alidai shtaka la tano linaikabili Kampuni ya Six Telecoms ambayo inadaiwa katika kipindi hicho ilitakatisha kiasi hicho cha fedha.

Wakili Nyantori, alidai shtaka la sita linawakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa katika kipindi hicho walisaibabisha hasara ya zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu kwa TCRA.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu mashtaka yanayowakabili kisheria yanasikilizwa Mahakama Kuu.

Kimya kilitawala huku wengine wakitikisa kichwa wakati mashtaka ya kutakatisha fedha yalipokuwa yakisomwa.

Wakili wa utetezi, Dk. Masumbuko Lamwai, aliwasilisha hoja mahakamani hapo akidai kwamba mashtaka hayo ni batili hayastahili kuwepo.

Alidai hakuna hati ya mashtaka iliyopo mahakamani sababu mashtaka yaliyopo hayaelezi nani kafanya nini.

“Shtaka la nne, tano na sita halielezi nani kafanya nini, mahakama haipokei kesi kwa sababu kutakatisha fedha lazima liwe kweli shtaka la kutakatisha fedha, shtaka la kughushi lazima lieleze nani kaghushi wapi… Sio kusema wote.

“Huwezi kuondoa mashtaka, lakini mahakama inaweza kuamuru hati ya mashtaka ibadilishwe, haya ni mashtaka yaliyolewa harakaharaka bila kufikiria wanashtaki nini… Mheshimiwa hakuna mashtaka mbele yako.

“Jamhuri waende wakajipange upya… maji hayapandi mlima yanashuka, wasijaribu kuyapandisha kwa pampu,” alidai Lamwai.

Akijibu, Wakili Zakaria, alidai upande wa utetezi ulichotakiwa kufanya ni kuishauri Jamhuri na si kuomba amri ya mahakama kwani haina uwezo wa kutoa amri yoyote.

Baada ya kusema hayo, aliiomba mahakama kutozingatia hoja za upande wa utetezi kwani hazina msingi.

Hakimu Nongwa, aliahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa wiki hii kwa kutoa uamuzi kutokana na hoja zilizowasilishwa.

Hata hivyo, shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana kisheria.

Kabla ya kusomewa mashtaka mahakama hiyo, ilifuta kesi ya awali iliyofunguliwa miaka miwili iliyopita dhidi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidh Shamte na wafanyakazi wengine watano.

Washtakiwa walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni nane.

Mbali na Shamte, washtakiwa wengine ni Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Raphael Hongo, Mhasibu Said Ally, Ofisa Masoko, Noel Chacha, Msimamizi wa Mtandao, Tinisha Max na Mkuu wa Takwimu za Biashara, Vishno Konreddy.

Walidaiwa kushindwa kulipa Dola za Marekani 3,836,861 zilizopatikana kutokana na huduma za simu za kimataifa zilizokuwa zinaingia na kushtakiwa kwa kusabisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Kesi hiyo ilifutwa na baadhi ya washtakiwa waliunganishwa katika mashtaka mapya na Dk. Tenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles