25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SHAHIDI AINGIA NA BASTOLA MAHAKAMANI

Na UPENDO MOSHA-MOSHI

KESI ya maauaji ya aliyekuwa Mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite, Bilionea Erasto Msuya, ililazimika kuahirishwa jana, baada ya shahidi wa 16 wa upande wa mashtaka, kuingia kizimbani na bastola.

Shahidi huyo ambaye ni  Insipekta wa Polisi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) makao makuu Dar es Salaam, William Mziu (36), aliingia na silaha hiyo  alipokuwa akitakiwa kutoa ushahidi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi.

Mziu yuko katika ofisi ya DPP kitengo cha ukaguzi wa makosa ya mtandao na kompyuta.

Aliyegundua kwamba shahidi huyo ana bastola kiunoni ni Wakili wa Upande wa Utetezi, Hodson Ndusyepo, wakati shauri hilo likiendelea, saa 6:5 mchana.

Shahidi huyo  alikuwa akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili mwingine wa upande wa mashtaka, Omari Kibwana wakati shahidi alipokuwa akimuonyesha Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo, simu mbili za marehemu Bilionea Msuya ambazo ni kati ya vielelezo vya kesi hiyo.

Katika tukio hilo, shahidi huyo alionekana akiwa amepachika  silaha hiyo  kiunoni huku akiwa ameifunika kwa nguo alizokuwa amevaa.

Tukio hilo lilionekana kuzua minong’ono mahakamani hapo ikiwa ni pamoja na   mawakili wa upande wa utetezi na watu mbalimbali waliofika mahakamani hapo kufuatilia mwenendo wa shauri hilo.

Wakati akilalamikia kuwapo  silaha hiyo, Wakili Ndusyepo alidai   kwamba kulikuwa na tishio la usalama mahakamani hapo na hivyo akataka silaha hiyo iondolewe.

“Mheshimiwa jaji, hapa mahakamani kwa sasa hakuna utulivu na hakuna amani kwa sababu  tumemuona shahidi anayetoa ushahidi akiwa na silaha na ameingia nayo hapa.

“Ili hali ya utulivu irejee na watu tuwe na amani hasa sisi mawakili wa upande wa utetezi, tunaiomba mahakama iamuru shahidi aende kuihifadhi silaha yake kwanza.

“Mheshimiwa jaji, hapa mahakamani kila mtu anayeingia mlangoni anakaguliwa na askari ili kama ana kitu kisichostahili, anatolewa.

“Sasa iweje huyu aruhusiwe kuingia na silaha hapa, tunaomba shahidi akaihifadhi silaha yake ndipo aje aendelee kutoa ushahidi maana hali ya hewa si nzuri katika eneo hili kwa sasa,”alisema Wakili Ndusyepo.

Baada ya wakili huyo kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Upande wa Mashtaka, Abdallah Chavula,  aliiomba mahakama iahirishe shauri hilo ili shahidi akafuate taratibu za sheria za kukabidhi silaha yake kwa wahusika.

Jaji Maghimbi alikubali ombi la kuahirisha kesi hiyo kwa muda   shahidi akatunze silaha yake kabla ya kuendelea na ushahidi.

Kabla kesi haijaahirishwa  shahidi huyo alipokuwa akiongozwa na Wakili Kibwana, aliiambia mahakama   kwamba  baada ya Bilionea Msuya kuuawa, yeye ndiye aliyekabidhiwa simu mbili za marehemu,   Samsung Galax na Iphone kwa ajili ya kuzichunguza   kusaidia upelelezi wa kesi hiyo.

“Agosti 8, mwaka 2013, nilipokuwa katika mafunzo ya vitendo ya medani za kivita katika maeneo ya Kilelepori, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, niliitwa na mkuu wa mafunzo na kuniambia nahitajika katika ofisi ya RPC Kilimanjaro kuchunguza hizo simu.

“Nilipozungumza na RPC, Robert Boaz, nilikwenda kwa RCO Ng’anzi ambako niliunganishwa katika timu ya askari kama saba au nane hivi tukaelekea Kituo cha Polisi Bomang’ombe ambako nilikabidhiwa hizo simu.

“Inspekta wa Polisi, Samweli alinikabidhi simu hizo kwa maandishi pamoja na IMEI namba zake na nimezitambua kwa sababu ya namba za IMEI za simu hizo pamoja na sahihi yangu ya makabidhiano.

“Kwa kifupi, mimi ni mtaalamu wa vifaa vya elekroniki  na mchambuzi wa data katika vifaa vya aina hiyo kwa sababu  elimu ya hiyo niliipata  ndani ya Jeshi la Polisi.

“Pia, nimepata elimu hiyo kutoka katika mbalimbali ikiwamo Israel na India tangu mwaka 2000 na nina uzoefu wa zaidi ya miaka minane katika kitengo hicho,” alisema shahidi huyo.

Bilionea Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka 2013, saa sita mchana, kando ya barabara ya Arusha kuelekea Moshi, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014, inawakabili washitakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shahibu Said, maarufu kama Mredi, Musa Mangu, Jalila Said, Sadiki Jabiri, Karim Kihundwa na Ally Musa Majeshi. Kesi hiyo iliahirishwa jana hadi itakapopangiwa tarehe nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles