BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana limepitisha muswada wa sheria tano zilizofanyiwa marekebisho mbalimbali ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Sheria hizo zimo zinazohusu mikataba ya maliasili na rasilimali za nchi na Sheria ya Mahakama ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi.
Nyingine ni ya Upimaji wa Ardhi, Sura ya 324, Sheria ya Usajili wa Maofisa Mipango Miji, Sura ya 426 na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263.
Akiwasilisha bungeni muswada huo wa sheria mbalimbali, katika Sehemu ya nne ambayo ni Sheria ya Mikataba ya Maliasili na Rasilimali za Nchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema sheria hiyo ilivyo sasa haiko wazi kutamka kama madini na mafuta ni miongoni mwa maliasili na rasilimali zilizoainishwa katika tafsiri ya maneno ‘natural wealth and resources’ iliyoko katika kifungu cha tatu cha sheria hiyo.
Alisema ibara ya 22 ya muswada, inapendekeza kifungu hicho kirekebishwe kwa kuongeza madini na mafuta kuwa miongoni mwa maliasili na rasilimali zilizoainishwa katika tafsiri ya maneno hayo.
Tunakubaliana na Jaji Masaju kuwa lengo la marekebisho hayo ni kuainisha katika sheria kuwa madini na mafuta ni maliasili na rasilimali inayosimamiwa ipasavyo na masharti ya sheria na si vinginevyo kama ilivyokuwa awali.
Aidha tunakubaliana na marekebisho ya Sheria ya Mahakama ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi kwani kwa kipindi kirefu tumeshuhudia Taifa likipitia katika wakati mgumu.
Tunasema hivyo kwa sababu migogo ya ardhi imesababisha madhara makubwa kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali, watu wamepoteza maisha, huku mifugo nayo ikiuawa.
Tunaamini sasa kwa sheria hii, hata halmashauri zetu ambazo ndiyo zinasimamia utekelezaji wa sheria, zitafanya kazi kwa kujiamini tofauti na ilivyokuwa awali.
Lakini pia vyombo vya utatuzi wa migogo ya ardhi sasa, ikiwamo mabaraza ya ardhi ya kata na wilaya yanaweza kuanzishwa katika maeneo mengine ya kiutawala ikiwamo miji, manispaa na majiji.
Katika eneo hili tunasisitiza kuanzishwa haraka ili kupunguza vilio vya wananchi ambavyo kwa kweli vimekuwa vya muda mrefu, licha ya Serikali kuchukua hatua kali kila wakati.
Katika mabadiliko haya, tunaona kifungu cha 10 (1) cha sheria hiyo, kinaweka masharti kuwa kila baraza la ardhi la kata, litakuwa na mamlaka ya kusikiliza migogoro ya ardhi katika eneo la halmashauri ya wilaya ambako limeanzishwa ili kupunguza msongamano wa kesi nyingi kwenda ngazi nyingine za juu.
Jambo jingine ambalo ndani ya sheria hii, ni kipengele cha kumpatia waziri mwenye dhamana ya ardhi kuwa na mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu utendaji wa madalali ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa chanzo kikubwa cha migogoro.
Sisi MTANZANIA, tunasema sheria hizi zimekuja wakati mzuri kwa sababu kumekuwapo na malalamiko ya muda mrefu hasa kwa katika kitengo cha mipango miji ambacho kimekuwa kikilalamikiwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wao vizuri.
Tunasema hivyo kwa sababu, miongoni mwa malalamiko makubwa ni kushindwa kuzuia ujenzi holela ambao umeshamiri katika maeneo mengi yakiwamo yanayotaharisha usalama wa wananchi.
Tunaamini kuanzia sasa baada ya kupitishwa sheria hii, tutaona mabadiliko katika maeno yote yaliyoguswa na sheria hii, kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote. Ndiyo maana tunasisitiza sheria hizi zisimamiwe na mamlaka husika ipasavyo.