25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MWISHO WA ZAMA ZA MUGABE

Na Waandishi Wetu

NI dhahiri kuwa, mwisho wa zama za Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, zimefika ukingoni baada ya jeshi la nchi hiyo, kumweka kizuizini nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Zimbabwe, jeshi hilo linawashughulikia wahalifu waliomzunguka kiongozi huyo aliyetawala taifa hilo tangu mwaka 1980.

Hatua hiyo imekuja siku moja tu baada ya vifaru kuripotiwa kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo, Harare huku vingine vikifunga barabara kuu za kuingia mjini humo na kulizingira Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC) katika kile kilichoonekana ni hatua za awali za kumdhibiti Mugabe.

Hali hiyo ni kiashirio kwamba, hata kama jeshi halitamwondoa madarakani Mugabe kwa sasa ama kumtaka ajiuzulu kwa hiyari yake, nguvu zake zimeshapunguzwa.

Baadhi ya viashiria vya nguvu za mkongwe huyo kupunguzwa ni pamoja na jeshi lililoaminiwa kuwa linamtii kuweza kumweka kizuizini na kushikilia maeneo muhimu kama kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC), Ikulu, Bunge na Mahakama.

Kiashirio kingine ni kurudi nchini kwa makamu wa Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa (75), ambaye alikuwa amevuliwa madaraka na Mugabe hivi karibuni na sasa anatajwa kuwa anaweza kukabidhiwa madaraka na jeshi mara baada ya kumaliza wanachotaka kukifanya.

Baada ya jeshi kuchukua hatua hiyo, jana Rais Jacob Zuma, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), alisema ameongea na Mugabe na amemweleza kuwa yuko kizuizini nyumbeni kwake.

Taarifa kutoka ofisi ya Zuma zilisema: “Rais Zuma alizungumza na Rais Robert Mugabe mapema leo na amedokeza kwamba anazuiliwa nyumbani kwake lakini alisema yuko salama” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Zuma, zinasema kiongozi huyo wa Afrika Kusini pia amewasiliana na Majeshi ya Ulinzi ya Zimbabwe (ZDF).

Katika taarifa yake ya awali, Zuma alisema atafuatilia kwa karibu yale yanayoendelea katika taifa hilo jirani na alitoa wito kwa jeshi kusuluhisha mzozo uliopo kwa njia ya amani.

Milio ya risasi

Mapema jana, milio ya risasi na milipuko ilisikika kwa muda mrefu karibu na nyumba binafsi ya Rais Mugabe na baadaye kutangazwa kuwa anashikiliwa na yuko salama pamoja na familia yake.

Hata hivyo jeshi hilo limekanusha kupindua Serikali lakini liliapa kukabiliana na ‘wahalifu’ waliomzunguka Rais Mugabe, uamuzi ambao umekuja baada ya kueleza kutofurahishwa anavyowashughulikia wanachama wa ZANU-PF wanaohusika na harakati za ukombozi.

Mwenendo huu mpya katika siasa za Zimbabwe, ambao haukutarajiwa na wengi ulianza juzi jioni kwa magari ya jeshi kuonekana yakielekea Harare, ingawa Gazeti la Serikali la Herald lilijaribu kupuuza hali hiyo likisema ‘ni sehemu ya mazoezi ya kijeshi’.

Jeshi hilo lilithibitisha kupitia ZBC juu ya uamuzi wake huo usiku wa siku hiyo. “Tunataka kuhakikishia taifa kwamba Rais Robert Mugabe, mkewe Grace na watoto wao wako salama na wamehakikishiwa usalama wao,” alisema msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Sibusiso Moyo.

“Tunalenga tu wahalifu waliomzunguka ambao wanatenda uhalifu na kuharibu uchumi wetu. Punde tutakapokamilisha lengo letu tunatarajia hali itarudi kuwa ya kawaida. Niwahakikishieni haya si mapinduzi ya serikali”.

Katika miaka ya hivi karibuni jeshi hilo limekuwa likishutumiwa na Mugabe kuingilia siasa za ZANU-PF.

Juzi Vijana wa ZANU-PF wanaomuunga mkono Grace kumrithi mumewe, walimshambulia Mkuu wa Jeshi Constantine Chiwenga kwa ‘mienendo ya uasi’ baada ya kumkosoa Rais kwa kumfukuza Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa.

Chiwenga, ambaye ni mshirika wa karibu wa Mnangagwa alikuwa ameonya kuhusu uwezekano wa wanajeshi kuingilia kati kutatua taharuki ya kisiasa inayohusu urithi wa mamlaka, ambayo imedumu kwa miaka kadhaa sasa.

HATIMA YA FAMILIA YA KWANZA

Kwa mujibu wa ripoti za awali, Grace Mugabe huenda akaruhusiwa kuondoka Zimbabwe, baada ya mumewe kuwekwa kizuizini.

Kituo cha Habari cha Afrika Kusini News24, kimesema Mugabe amefanya majadiliano ili Grace aondoke wakati yeye akijiandaa kung’atuka.

Pia ripoti nyingine zinasema Grace tayari ametorokea Namibia usiku wa kuamkia jana na miongoni mwa waliosema tarifa hiyo ni Mbunge wa upinzani, Eddie Cross.

Mwanasiasa huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC), alisema taarifa za uhakika alizo nazo, Grace aliruhusiwa na jeshi kuondoka nchini humo usiku wa kuamkia jana.

Ameongeza kuwa Grace alikuwa hana sehemu nyingine ya kwenda kutafuta hifadhi baada ya mahali ambako ni chaguo la kwanza Afrika Kusini alikozaliwa kuharibu.

Miezi michache iliyopita, Grace alimjeruhi mwanamitindo mmoja akimtuhumu kuwaharibu wanae wa kiume, kitendo ambacho kilishuhudia miito ya kumtaka ashitakiwe. Lakini Serikali ya Zuma ikamnusuru kwa kinga ya kidiplomasia.

Kwa sababu hiyo safari hii Grace asingeweza kwenda akawa salama. Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa na jeshi.

Lakini Nick Mangwana, mwakilishi wa chama tawala cha Zanu-PF nchini Uingereza, amekaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akisema amepokea taarifa Grace hayupo tena Zimbabwe.

MAWAZIRI WAKAMATWA 

Wakati hayo yakitokea, idadi kadhaa ya mawaziri tayari wamekamatwa kwa mujibu wa vyanzo vya habari.

Awali miili ya risasi  ilitawala katika kitongoji wanachoishi matajiri na vigogo cha Borrowdale usiku kuchwa na kuashiria operesheni za jeshi kuanza kama ilivyotabiriwa.

Vyanzo vya habari vilisema kwamba jeshi lilikamata vigogo wa kundi liitwalo Kizazi 40 (G40) lililopo ndani ya chama tawala cha Zanu-PF‚ likiongozwa na Grace Mugabe.

Waliokamatwa ni pamoja na Waziri wa Elimu Jonathan Moyo‚ Waziri wa Serikali ya Mitaa Saviour Kasukuwere na Waziri wa Fedha Ignatius Chombo.

Aidha Kiongozi wa Kitengo cha Vijana Zanu PF, Kudzai Chipanga, amekamatwa mjini Harare, siku moja baada ya kusema kuwa wafuasi wake walikuwa tayari kufa wakimpigania Rais Robert Mugabe.

Mapema wiki hii, Chipanga alimpinga hadharani Jenerali Constantino Chiwenga, baada ya mkuu huyo wa Majeshi kusema alikuwa amejiandaa kuchukua hatua kumaliza hisia za kutengwa katika chama cha Zanu PF.

Kisha kiongozi huyo wa vijana akajibu juzi na kusema kuwa Jenerali Chiwenga hakuwa na uungwaji mkono wa jeshi lote

MNANGAGWA RAIS WA MPITO?

Akaunti ya Twitter ya Chama tawala cha Zanu PF imedai Emmerson Mnangagwa (75) ambaye ndiye sababu ya yote yanayotokea sasa baada ya kufukuzwa na Mugabe kwa madai ya kukosa uaminifu anakuwa rais wa mpito.

Awali kufukuzwa kwake, kulimaanisha Grace Mugabe anatarajiwa kuteuliwa kuwa makamu wa rais wakati wa mkutano maalum wa chama tawala cha Zanu-PF mwezi ujao.

Taarifa za twitter za chama hicho pia zilikana uwapo wa mapinduzi badala yake ikiita kinachoendelea nchini humo kwa sasa kuwa makabidhiano ya madaraka yasiyo na umwagaji damu.

Katika mlolongo wa ujumbe uliotumwa jana asubuhi, akaunti hiyo ilisema: “Jana usiku (juzi) familia ya kwanza ilishikiliwa lakini iko salama. Ni hatua iliyolenga ulindaji wa katiba na ustawi wa taifa letu. Si Zimbabwe wala ZANU-PF inayomilikiwa na Mugabe na mkewe.

“Tunasisitiza hakuna mapinduzi, bali uhamashaji wa madaraka usio wa umwagaji damu, ambao ulishuhudia wala rushwa na wahuni wakikamatwa na mzee ambaye mkewe alitumia fursa hiyo vibaya wamekamatwa.”

“Ile milio michache ya risasi na mizinga mliyoisikia ilitokana na wahuni hawa waliokataa kukamatwa, lakini sasa wanashikiliwa.

“Leo zinaanza nyakati mpya na komredi Mnangagwa atatusaidia kuipata Zimbabwe nzuri na iliyostawi,” ilijieleza sehemu ya ujumbe hiyo inayoonekana kutumwa na washirika wa Mnangagwa, ambaye kabla ya kufukuzwa alimchefua Mugabe kwa kusema ‘ZANU-PF si mali ya Mugabe wala mkewe kiasi cha kufanya mambo kwa kadiri wapendavyo.’

ZBC YAZINGIRWA

Shirika la Utangazaji la Taifa (ZBC) lenye makazi yake Pocket Hills mjini Harare‚ nalo lilitwaliwa na jeshi saa 10 alfajiri ya jana, baada ya awali vifaru kuonekana kujongea zilipo ofisi zake juzi jioni.

Hata hivyo taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo, waliambiwa na wanajeshi hao hawapaswi kuwa na wasiwasi na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.

Kwa upande wa Gazeti la The Herald, ambalo awali lilikuwa likikana ukweli wa mambo unaotokea sasa, lilianza kuripoti uhalisia hasa taarifa zilizotolewa na jeshi la Zimbabwe.

Aidha televisheni na redio za serikali vimekuwa vikicheza nyimbo za wakati wa uhuru miaka ya 1980 na kurudia matangazo ya Meja Jenerali Sibusiso Moyo.

CHINA YAKANA KUSAIDIA MAPINDUZI

Serikali ya China ilisema kuwa Mkuu wa Jeshi la Zimbabwe Jenerali Constantino Chiwenga alizuru taifa hilo wiki iliyopita kwa ziara ya kawaida ya kijeshi isiyohusiana na mapinduzi.

China inafuatilia kwa karibu hali ya mambo nchini humo na matumaini kuwa pande husika zitatatua mgogoro huo wa ndani kwa amani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Geng Shuang aliuambia mkutano wa wanahabari jana.

UINGEREZA, MAREKANI ZATOA NENO

Raia wa Uingereza na Marekani wameshauriwa na balozi zao nchini humo kubakia ndani kuhofia uwezekano wa kutokea machafuko.

Aidha Ubalozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wake wa Tiwtter ulisema utasitisha shughuli za kiofisi ubalozini hapo kutokana na halisi ya sasa mjini Harare.

Aidha Marekani imesema kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya Zimbabwe na kutoa rai pande zote kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.

Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini Isack Moyo ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa Serikali ipo imara katika jambo hilo na kuzuia uwezekano wowote wa kufanyika kwa mapinduzi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles