25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUNA HARUFU YA FIKSI NA USANII KATIKA MASHINDANO MENGI

Na RAMADHANI MASENGA  

RICHARD Bezuidenhout alitajwa kushinda zaidi ya milioni 450 katika Shindano la Big Brother 2007. Aliporudi Bongo akatajwa kuingia katika tasnia ya filamu na kufungua biashara ambazo hakuziweka wazi.

Filamu zake kadhaa tuliziona. Kisha ikawa kimya. Baadaye akaibuka tena akisema alikuwa akifanya filamu Canada. Ila ile filamu ya Canada hatukuiona. Wadau wakamuuliza kulikoni.

Hakuwa na jibu la maana wala la uhakika. Siku kadhaa baadaye akaonekana maeneo ya Ubungo akifungua banda la chips. Mshindi wa zaidi ya milioni 450 katoka katika filamu na kuangukia katika kuuza chipsi!

Chips sio biashara mbaya ila ni biashara ndogo sana kwa mshindi wa milioni 450. Wadau wakajiuliza; Richard ana kichwa kibovu kiasi cha kushindwa kupanga mikakati mizuri ya kufanya milioni 450 yake izae?

Ndani ya miaka mitatu mshindi wa zaidi milioni 450 anaangukia katika biashara ambayo haina uhakika wa kumpa hata milioni moja kwa wiki? Kunani?

Ya Richard yakapita. Yakaja ya Idris Sultan. Huyu alitajwa kushinda milioni 500 katika BBA 2014. Mwenyewe alipohojiwa juu ya kiasi hicho cha pesa alikiri kukipata huku akisema ana mikakati mikubwa sana ya kibiashara.

Watu wakaamini. Miezi michache badaye akaonekana yuko busy na Wema Sepetu. Idris hakuzungumzwa tena kama mfanyabiashara bali akazungumzwa zaidi kama mpenzi wa Wema.

Kila uchao kukawa na drama kuhusu yeye na Wema. Kama ilivyotarajiwa, miezi kadhaa baadaye Wema akatengana na Idris. Watu wakawa wanasubiri biashara ya Idris, ila wapi! Baadaye akaanza kupambana na hali yake kwa kuamua kuingia katika utangazaji na komedi.

Watu wakauliza Idris Sultan ile milioni 500 iko wapi? Biashara uliyowahi kusema utaifanya iko wapi? Kiza kikazidi kuwa kinene.

Zipo stori kwamba ameamua kuishi kwenye apartment ili aonekane bado yuko vizuri. Mshindi wa milioni 500 mpaka sasa hana makazi ya kueleweka hata biashara ya kujulikana! Kulikoni pesa za Big Brother?

Ni kweli hela zinazotajwa kupata wanapata ama kunakuwa na usanii? Miezi kadhaa nyuma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe alisimamisha baadhi ya mashindano kwa kile kilichodaiwa kuwepo kwa ulaghai mkubwa katika utoaji wa zawadi.

Je, hata Big Brother kwenye shindano lenye hadhi ya kimataifa pia kuna usanii kama katika mashindano yetu mengine?

Msanii Ney aliwahi kuhoji kuhusu pesa alizopata Walter Chilambo katika Shindano la Bongo Star Search (BSS). Alisema mbali na kudaiwa kupata pesa nyingi lakini bado anaishi kwa kubabaisha huku maisha yake yakiwa hayana tofauti sana na yale aliyokuwa akiishi zamani.

Wadau hawakutilia mazingatio kwa kuamini Ney aliropoka kama kawaida yake. Kuna haja washiriki wa haya mashindano wawe wakweli katika nafsi zao. Ni kweli hizi zawadi wanazodaiwa kupata huwa wanapata kweli?

Kama kweli wanapata, basi kuna tatizo sana katika vichwa vya vijana wetu wa Kitanzania. Mshindi wa milioni 500 anarudi tena kuajiriwa kwa mshahara usiofika milioni 4 kwa mwezi?

Mshindi wa milioni zaidi ya milioni 450, anarudi mtaani kuanza kupambana na mabanda ya chipsi? Kama kina Walter Chilambo na Idris kweli walipata kinachodaiwa kupatikana katika mashindano waliyoshiriki, basi Tanzania ina safari ndefu sana kufikia maendeleo ya kweli.

Zaidi ya asilimia 60 ya Watazania ni vijana. Kama asilimia yote hii inajengwa na watu wenye kupata milioni 500 kisha baada ya miezi michache zinakauka, basi ndoto ya nchi hii kuifikia Canaan ni nzito mno kuliko kuhamisha mlima Kilimanjaro Moshi na kuuleta Manzese!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles