30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MUHIMBILI, AGA KHAN KUFANYA UPASUAJI WA KUPANDIKIZA MATITI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KWA mara ya kwanza Hospitali ya Aga Khan imeanza kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti kwa wanawake wasiokuwa nayo baada ya kukatwa ili kutibiwa saratani ya matiti.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Aga Khan, Dk. Aidan Njau.

Alisema madaktari wa Aga Khan watafanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari wenzao kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Shirika la Kimataifa lisilo la Serikali la Women for Women la nchini Marekani.

Pia alisema tayari wanawake wawili wameandaliwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo wa aina yake.

“Ni awamu ya tatu sasa tunafanya upasuaji kwa akina mama, watoto na mabinti waliopata madhara katika miili yao kutokana na ajali mbalimbali, lakini kwa upande wa upandikizaji matiti huu ni upasuaji wa kwanza tunaanza kufanya hapa nchini,” alisema na kuongeza:

“Tunachofanya ni kutengeneza viungo vyao ili virudi katika hali ya kawaida ili na wao waweze kuendelea na maisha yao kama watu wengine.

“Mara nyingi mtu anapoelezwa kuwa ana tatizo la saratani wengi huathirika kisaikolojia na mama anapofanyiwa upasuaji wa kuondoa titi kama sehemu ya matibabu dhidi ya saratani huzidi kuathirika kisaikolojia.

“Maumivu huongezeka pale anapoelezwa kuwa matibabu ni kuondolewa ziwa lake kama sehemu ya matibabu, hivyo tunaona upasuaji huu utawafaa na utawasaidia wengi ambao walipoteza kiungo hicho.

“Tunachofanya, tunachukua sehemu katika mwili wake na kutengeneza titi ambalo tutakuja kulipandikiza tena kwenye mwili wake, ingawa haitakuwa kama ziwa ambalo Mungu alimpatia, lakini litamwezesha kuwa kama wanawake wenzake”.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Ajali za Moto na Viungo vilivyokakamaa wa MNH, Dk. Edwin Mrema, alisema pamoja na upasuaji huo, wameandaliwa takribani wagonjwa 33 watakaofanyiwa upasuaji wa kurekebisha viungo.

“Baada ya upasuaji tunaendelea kuwafanyia mazoezi, kuna wagonjwa wapo nyumbani wanaishi kwa woga wakiogopa macho ya watu, tunatoa wito watu wajitokeze tuwatibu, ni huduma endelevu,” alisema.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Shirika la Women for Women, Andrew Pusic, alisema: “Nafurahi kuwapo Tanzania, tunachofanya ni ushirikiano wa pamoja ili kuweza kuwasaidia wanawake wenye shida mbalimbali na kutoa mafunzo kwa njia ya upasuaji.”

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles