JUDITH NYANGE Na BENJAMIN MASESE-MWANZA
RAIS Dk. John Magufuli amesema mkuu wa mkoa yoyote atakayeshindwa kupeleka wawekezaji kujenga viwanda katika mkoa wake hatamvumilia.
Amewataka wakuu wote wa mikoa kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye amekaribisha wawekezaji wanaojenga viwanda vipya.
Agizo hilo alilitoa Mwanza jana alipokuwa akituhubia mkutano wa hadhara eneo la Nyakato wilayani Ilemela.
Rais alisema viwanda si mali yake bali ni mali ya wananchi ambao ndiyo walipa kodi.
Alisema ingawa Tanzania ilikuwa na viwanda vingi, hivi sasa Watanzania wamebaki hawapati majibu vilikwenda wapi hali inayoifanya Serikali iamue kufanya kazi ya kuvifufua vya zamani na kujenga vipya.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo Rais alizindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona kilichojengwa Nyakato. Leo anatarajiwa kuzindua viwanda vingine viwili.
Alisema amefurahishwa na ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela na kwamba kila anapopita ndani ya mkoa huo, lazima huzindua kiwanda ama viwanda kwa vile wawekezaji wengi hukimbilia kuwekeza mkoani humo.
“Nataka nichukue fursa hii kukupongeza mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwatafuta wawekezaji wengi na kuwekeza kwenye viwanda.
“Nataka wakuu wa mikoa wa aina hii, mkuu wa mkoa ambaye kila siku napita mkoa wake bila kuzindua kiwanda sitamvumilia kufanya naye kazi, lazima ang’oke.
“Mkuu wa Mkoa ambaye haleti wawekezaji katika mkoa wake kujenga viwanda… kwanza hivyo viwanda si vya wakuu wa mikoa bali ni mali ya wananchi. Kuwapo viwanda kutasaidia kutengeneza ajira, hayo ndiyo maendeleo tunayotaka.
“Haiwezekani Tanzania iwauzie … tulime pamba tuwauzie wazungu watengeneze nguo wazivae kisha kutuletea zikiwa mitumba.
“Tunataka nguo zitengenezwe hapa na Mwatex ili ziuzwe kwa bei nafuu kuliko hiyo mitumba. Sizuii mitumba lakini nguo mpya na bora lazima zitengenezwe hapa,” alisema Rais Magufuli.
Alimweleza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ajirekebisha na afanye kazi ya kufufua, kufunga na kuchukua viwanda visivyofanya kazi na awape watu wengine.
“Haiwezekani unapewa kiwanda kutoka mwaka wa kwanza hadi wa 20 bila uzalishaji, wenye viwnada hivyo virudisheni haraka kwa sababu tutakapoanza kuwashika tutadai faida ambayo walikuwa wakiipata miaka hiyo,” alisema.
Mgogoro wa Meya
Akizungumzia suala la mgogoro wa Meya, Rais Magufuli alisema ameyaona mabango likiwamo lililokuwa limeandika kuwa Meya wa jiji la Mwanza, James Bwire, amewekwa ndani na Mkuu wa Mkoa ili asionane na rais ingawa alikuwa ameachiwa huru.
Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Mwanza kuacha malumbano na kukaa meza moja kumaliza mambo yao kwa kuwa wanatoka chama kimoja.
Alisisitiza kwamba wakiendelea na tabia hiyo hawatafika popote.
“Mkiendelea kulumbana mtashindwa kutatua kero za wananchi, haya mabango ya mara kwa mara yanatokea kwa sababu mnashindwa kutatua matatizo yao.
“Wajane wanadhulumiwa na masikini hivyo hivyo, tambueni mkishindwa kutatua mgogoro mapema, utawashinda ukikaa muda mrefu,” alisema.
Alisema pia kuwa sababu mojawapo iliyofanya kutotekeleza ahadi yake ya kupeleka Sh milioni 50 kwa kila kijiji inatokana na ufisadi mkubwa uliokuwa umeota mizizi.
Rais alisema baada ya kuwabana matokeo yameanza kuonekana huku miradi mingi ikianza kutekelezwa.
“Nilipoingia madarakani nimeona mengi na kuchukua hatua nilizochukua, nikafikiria nianze kugawa Sh milioni 50 kwa kila kijiji au ninunue treni, kujenga hospitali, kusambaza X ray, elimu na mengineyo.
“Nimeamua kuwekeza katika miradi mingine, hivyo ahadi yangu ya Sh milioni 50 itakuja baadaye,” alisema Rais Magufuli.
Azui boabomoa
Awali katika mkutano wake kwenye uzinduzi wa daraja la watembea kwa miguu la Furahisha, Rais Magufuli, alitangaza kupiga marufuku mpango wa kubomoa nyumba za wakazi wa mitaa ya Mhonze na Kigoto Wilaya ya Ilemela.
Nyumba za wananchi hao zimejengwa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni makazi ya Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Mwanza na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Alitoa agizo hilo baada ya baadhi ya wananchi kuinua mabango yao kumwonyesha alipokuwa akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Mabango hayo yalikuwa na ujumbe mbalimbali ukiwamo wa kudai kutapeliwa, kubomolewa na kudhulumiwa maeneo hayo kwa kigezo kuwa ni wamevamia.
Alisema Rais ndiye msimamizi wa ardhi na wananchi ndiyo waliomchagua.
Kwa sababu hiyo aliagiza hatua ya kubomoa nyumba zaidi ya 2000 isimamishwe huku akizitaka wizara zinazohusika, vyombo vya mamlaka hizo, na uongozi wa CCM Mkoa wa Mwanza kukaa pamoja kuangalia ramani zote na mahali palipo na usalama wa watu na kutoa mapendekezo mapya.
“Nimeona mabango yenu ya wale mliojenga Kigoto na Mhonze, mpo zaidi ya 2000 na mmeishi hapo zaidi ya miaka 30 lakini leo mnaambiwa mmevamia.
“Kwa vile nimeliona suala hili leo naomba uongozi wa mkoa, polisi na uwanja wa ndege, hakuna kubomoa mpaka nitakapotoa maelekezo mengine.
“Sheria namba 4 ya 1999 na sheria ya vijiji namba 5 inasema msimamizi wa ardhi ni Rais… ninyi ndiyo mlionipa urais mkiamini chama changu ndicho chenye huruma, sasa kwa kuwa niliwaahidi kuwatumikia naomba wasibomolewe kwanza,” alisema.
Alisema wale ambao wapo karibu na maeneo hatarishi aliyotaja kama eneo la ndani ya uwanja wa ndege na wale waliojenga karibu na vifaru vya jeshi, hao wataangaliwa uwezekano wa kuwahamisha kwa sababu ni maeneo yenye athari.
“Mliojenga ndani ya uwanja ni hatari, ndege ikiruka inaweza kuwaletea athari, lakini kama umejenga karibu na kifaru cha jeshi ukitokea mlipuko itakuwa ni hatari sana au wale waliojenga ndani ya kambi ya polisi ikitokea mbwa wa polisi akavamia makazi yao…,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia ujenzi wa daraja, Rais Dk. Magufuli alisema ana historia ya eneo hilo ambalo awali lilikuwa likiitwa Black sport kutokana na ajali nyingi panapokuwapo shughuli za mahubiri, michezo na shughuli nyingine ndani ya uwanja wa mpira wa CCM Kirumba na Furahisha.
Alisema wakati anaomba kura kura na kutoa ahadi za kujenga daraja hilo, baadhi ya watu walibeza na kusema haitawezekana lakini anashukuru Mungu kwa wananchi kumwamini na kumchangua pamoja na wabunge na madiwani kutoka CCM, hivyo hana cha kuwalipa isipokuwa kuwaletea maendeleo.
“Leo upanuzi wa barabara hii na ujenzi wa daraja umewezekana kwa kuvunjwa sherehe za muungano, kuna watu walinibeza wakidai siheshimu muungano.
“Sherehe zingeisha na kubaki na matatizo yetu leo hii tuna ukumbusho … huenda zikitokea sherehe nyingine nitazuia ili fedha zikafanye kazi Zanzibar ama Mtwara,” alisema.
Alisema amekwisha kuzungumza na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuongeza miundombinu kuruhusu ndege za mashirika makubwa duniani kama Emirates, kutua Mwanza na kupunguza adha kwa wafanyabiashara.
Kuhusu meli, alisema tangu kuzama meli ya MV Bukoba mwaka 1996, wananchi wa Kanda ya Ziwa wamepata shida na hawajawahi kupata meli mbadala.
Alisema Serikali imekusudia kuanza ujenzi wa meli mpya kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, magari na mizigo.
Rais alisema kampuni kutoka Korea Kusini imeshinda tenda ya ujenzi wa meli hiyo na hadi kufikia Januari 2018 itaanza kuijenga. Hata hivyo, alisema hivi sasa Serikali inaendelea na ukarabati wa meli ya MV Liemba na Victoria.
APONGEZA CUF
Rais Dk Magufuli, alipongeza mabadiliko yanayofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) akisema kuwa yanaungwa mkono na CCM.
Bila kutaja mabadiliko ya aina gani, Rais Magufuli alisema: “Tunawapongeza kwa mabadiliko mnayofanya”.
Kauli hiyo aliitoa wakati akikamilisha hotuba yake na kumtambua Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka(CUF), ambaye awali alipanda jukwaani na kusifia utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mbunge huyo ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu. Kuchauka alikaribishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Norman Sigalla kuwasalimia wananchi mbali ya kumwagia sifa Rais Magufuli.
KAULI YA MEYA
Akizungumza baada ya kuachiwa na polisi baada ya kuhojiwa kwa saa saba jana, Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, alisema hatua hiyo inatokana kutuhumiwa kutaka kuhatarisha msafara wa Rais Dk. John Magufuli wakati akiwasili Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
“Nikiwa uwanjani nilifuatwa na askari wawili ambao waliniambia nipo chini ya ulinzi.
“Niliwauliza tatizo ni nini wao walinijibu wamepewa maelekezo kutoka juu kisha walinipeleka kituo kidogo cha polisi uwanjani na kuniweka hapo.
“Baada ya rais kuondoka uwanjani nilichukuliwa na askari wengine watatu ambao walinipeleka kituo kikuu,” alisema.
Alisema askari hao waliomfuata uwanjani walimchukua kwa gari dogo binafsi na alipofikishwa kituo kikuu cha polisi katika ofisi ya RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa), walimueleza kuwa wamearifiwa kuwa alikuwa ameandaa kitu kibaya kwenye msafara wa rais kitendo ambacho alidai kilimsikitisha.
“Walipomaliza kunichukua maelezo niliendelea kukaa pale nje ya ofisi yao na ndipo alipokuja RCO na kuniita ofisini kwake ambako alinieleza kwamba shida iliyopo ni ‘sisi kwa sisi tunasigana’.
Aliniambia: “Nyie kwa nyie mnavutana mnatupa kazi ngumu sisi watendaji, kisha akaniruhusu nidhaminiwe na kutoka”.