32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

USHIRIKINA USIPEWE NAFASI KATIKA SOKA LETU

SOKA ni mchezo unaopendwa na una mashabiki wengi kuliko mchezo mwingine wowote duniani, lakini pia katika zama hizi za karne ya 21, kumekuwa na biashara kubwa inayotokana na mchezo huo.

Soka yenyewe ni burudani inayovutia kwa kuwa inachezwa kwa kuonekana na matokeo yanawafanya mashabiki wa timu inayoshinda wafurahie na kuwapa faraja zaidi wawapo uwanjani.

Ukiachana na hilo, soka ni mchezo wa kiungwana kama Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) linavyosisitiza (Fair Play), lakini kumekuwa na vitendo ambavyo si vya kiungwana na vinapewa nafasi kubwa kuendelea miongoni mwa viongozi au wachezaji.

Jambo lenyewe ni kuhusiana na ushirikina ambapo kumekuwa na baadhi ya wachezaji au viongozi ambao wamekuwa kwa namna moja au nyingine wakijihusisha na masuala ya kishirikina katika mchezo wa soka.

Kadiri siku zinavyokwenda katika soka la Tanzania, kumekuwapo na ongezeko kubwa la vitendo vya kishirikina na hili limekuwa likifanyika sana katika mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga zinapokutana.

Juzi katika mchezo uliozikutanisha Simba na Yanga, kulitokea jambo kama hilo ambapo watunza vifaa vya timu hizo walikuwa wamesimama nyuma ya magoli, jambo ambalo lilileta hisia za imani za kishirikina kwa mashabiki waliokuwa uwanjani hapo na kulazimika Polisi kuwaondoa na baadaye kuruhusiwa.

MTANZANIA tunakemea vitendo vya kishirikina katika soka la Tanzania kwa kuwa vinazorotesha na kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo.

Pia tunaliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhakikisha kuwa wale wote wanaoleta vitendo vya kishirikina uwanjani wanachukuliwa hatua kali ili jambo hili lisipewe nafasi ili kuleta hali ya ushindani na kuifanya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa bora kama ligi nyingine.

Ushirikina katika zama hizi usipewe nafasi, badala yake viongozi na wachezaji waweke kipaumbele katika kusaka mbinu mpya na bora zaidi za kupata ushindi na si kuhangaika na masuala yasiyo na msingi kama hayo.

Ni wakati wa kusimamia vema misingi ya kanuni zake kwa kuwashughulikia wale wote wanaovuruga au kuleta masuala ya kishirikina viwanjani.

Sisi MTANZANIA tunapenda kuona kila timu ikicheza ligi kwa ushindani ambapo utafanikisha kumpata bingwa bora ambaye atawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa akiwa amejiandaa vya kutosha kwenda kupambana na kufanya vizuri na si kushughulika na masuala ya kishirikina ambayo hayawezi kuleta tija kama timu haijajiandaa vema.

Ni lazima TFF iwabane watu wenye vitendo vya namna hii, kwani wakati mwingine hata timu zimekuwa zikigoma kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo au kuingilia milango isiyo rasmi katika viwanja kutokana na kuhusisha masuala ya kishirikina.

Ifike wakati viongozi au wachezaji waachane na dhana potofu za kishirikina na badala yake wawape wachezaji mbinu imara za kucheza na kushinda ili kuleta ushindani na si vinginevyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles