Na EVANS MAGEGE – DAR ES SALAAM
WAKATI hali ya sintofahamu imetanda kutokana na mwenendo wa maiti kuokotwa mara kwa mara katika fukwe za Bahari ya Hindi, zikiwa zimefugwa ndani ya mifuko ya sandarusi (viroba) au ya plastiki,
wazoefu wa masuala ya bahari, hususani wavuvi, wamesema ni jambo la kawaida kwao, hasa msimu wa pepo za kusi.
Lakini licha ya kuwa matukio hayo ni jambo la kawaida kwao, kwa sasa nao wameingiwa hofu kubwa ndani ya msimu wa pepo hizo kwa mwaka huu, baada ya kuona maiti nyingi zikiwa zimefungwa katika sandarusi, mtindo waliodai ni mpya machoni mwao.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA Jumapili kwa kuwafikia wavuvi, madalali wa samaki na wafanyabiashara wadogo wadogo kwa nyakati tofauti katika fukwe tano za Bahari ya Hindi zilizopo Dar es Salaam, umebaini kuwa licha ya mshangao na hofu kubwa ya kuwapo matukio hayo, lakini wengi wao hawapendi kutoa taarifa katika vyombo vya dola pindi wanapoziona maiti zikielea baharini.
Baadhi waliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa hawapendi kutoa taarifa katika vyombo vya dola kwa sababu ya kukwepa usumbufu.
Kuhusu uzoefu wao wa masuala ya baharini, walisema kuwa msimu wa pepo za kusi zinazoanza Juni na kumalizika Oktoba, umekuwa ni kawaida kwao kuona maiti nyingi baharini za watu wa jinsia tofauti.
Lakini walisema hali hiyo imekuwa tofauti katika msimu wa mwaka huu, baada ya kuona maiti nyingi baharini zikiwa zimefungwa ndani ya sandarusi na kufungwa kamba miguuni kiunoni na mikononi.
Pia walisema wamekuta maiti nyingine zikiwa zimefungwa mifuko myeusi iliyoziba uso hadi shingoni, huku miguu na mikono nayo ikiwa mefungwa ama kamba au nyaya.
Simulizi ya wavuvi hao inatoa picha tata yenye maswali mengi kuhusu mwenendo wa matukio hayo. Ni nani anayeua watu kwa mtindo huo? Wanauawa kwa sababu gani? Maiti hizo zinatoka wapi?
Zipo hisia kutoka kwa baadhi ya wavuvi, kwamba miili hiyo huenda imesukumwa na mawimbi ya bahari kutoka kusini mwa Tanzania, ambako pia kuna mataifa yanayotumia Bahari ya Hindi kama Msumbiji, Visiwa vya Comoro, Mayotte, Afrika Kusini, na Madagascar.
UCHUNGUZI
Wavuvi waliofanya mahojiano na MTANZANIA Jumapili katika Ufukwe wa Mbweni, walidai kwamba maiti zilizofungwa hazijawahi kuonekana katika maeneo ya ufukwe huo.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wavuvi hao, waliziona maiti zilizowekwa katika sandarusi kwa nyakati tofauti katika sehemu mbalimbali za katikati ya bahari.
Embes Haji Alli ambaye ni mmoja wa wavuvi katika eneo hilo, alisema Agosti, mwaka huu, akiwa katika eneo la kina kirefu cha bahari upande wa Unguja akifanya shughuli zake za uvuvi, aliona mzigo ukielea na alipousogelea kwa udadisi zaidi, akabaini ni maiti ambayo tayari ilikuwa imeharibika.
“Ilikuwa usiku wakati navua samaki huko mkondoni (kina kirefu cha bahari) upande wa Unguja, niliona kitu kinaelea ikabidi niwe makini kukifuatilia, nilipokisogelea nikamulika vizuri kwa tochi kubwa, nikabaini ni maiti na tayari ilikuwa imeharibika na macho yalikuwa yamenyofoka.
“Baada ya kubaini hivyo, niliachana nayo kisha nikaendelea na shughuli zangu, lakini siku chache baadaye nilipata taarifa kwamba wavuvi wengine kwa upande wa Zanzibar walidai kuona maiti tano zikiwa katika mtindo ule ule wa kuwekwa katika sandarusi,” alisema.
Naye Abas Juma ambaye pia ni mvuvi katika ufukwe huo, alisema kati ya Julai na Septemba, mwaka huu, aliziona maiti tatu baharini, mbili kati ya hizo zilikuwa zimetiwa ndani ya sandarusi na moja ikiwa imefungwa kwa mfuko wa plastiki kichwani.
Juma alisema siku chache baadaye alipata taarifa kuwa wavuvi wenzake mkoani Tanga nao waliona maiti mbili zikiwa katika mtindo huo huo aliouona.
Pamoja na simulizi ndefu ya wavuvi hao, mwandishi aliwahoji kutaka kujua hatua walizochukua baada ya kuziona maiti hizo.
Juma alisema kuwa kwa kawaida huwa wanatakiwa kutoa taarifa polisi, lakini wavuvi wengi wamejenga tabia ya kutoripoti kwa kukwepa usumbufu, hivyo hata yeye hakuripoti sehemu yoyote zaidi ya kuwasimulia wenzake.
“Huku baharini tunakutana na maiti nyingi, lakini wengi wetu tumekuwa wazito kutoa taarifa kwa sababu unapotoa taarifa ya kuonekana maiti unajikuta katika wakati mgumu wa kutoa maelezo mara kwa mara polisi kana kwamba wewe ni mhalifu, hali hii unajikuta unapoteza muda wako polisi badala ya kwenda kutafuta riziki,” alisema Juma.
Katika Ufukwe wa Ununio, dalali mkuu wa samaki wa Soko la Ununio, Rashid Athuman, alieleza kuwa ana uzoefu wa miaka 15 katika shughuli hiyo na kwa muda wote huo hajawahi kusikia au kuona maiti imeingizwa katika mifuko ya sandarusi kama inavyotokea mwaka huu.
Alisema wakati wa pepo za kusi, maiti moja au mbili huonekana baharini, lakini si kama za sasa.
Alidai kuwa baadhi ya wavuvi katika ufukwe huo, waliwahi kumdokeza kwamba wakiwa katika shughuli zao waliona maiti zikiwa zimefungwa katika mifuko ya sandarusi.
“Hapa wavuvi wanashangazwa na hata sisi tunashangazwa, unajua nyakati kama hizi miaka ya nyuma tulikuwa tunapata habari ya kuonekana maiti huko baharini, labda watoto au watu wazima, lakini mazingira ambayo maiti hizo zinakutwa si ya kufungwa katika viroba au mawe kama inavyoripotiwa sasa.
“Nakumbuka mara ya mwisho nyakati kama hizi katika pwani hii, ulionekana mguu wa mtu akiwa amevaa viatu aina ya chachacha, tulitoa taarifa kwa mamlaka husika kisha tukauzika huo mguu, lakini tangu tukio hilo hakujawahi kuwapo taarifa za kuonekana maiti baharini zaidi ya hizo zinazotajwa sasa za watu kufungwa katika viroba,” alisema Athuman.
Naye Sesye Mwafongo, ambaye ni mvuvi katika ufukwe huo, alisema kawaida huwa anakwenda kuvua samaki baharini umbali wa kilomita 20 kutoka nchi kavu na kuna siku moja alidai kukutana na wavuvi wenzake baharini wakamwambia wameona mfuko wa sandarusi uliokuwa na maiti.
Hata hivyo, alisema hakuweza kuiona maiti hiyo kwa sababu alishindwa kusonga mbele zaidi kutokana na upepo mkali uliovuma kwa siku tatu mfululizo.
Mvuvi mwingine katika ufukwe huo, Mohamed Makuchele, alisema ndani ya miezi mitatu iliyopita amekutana na maiti tano baharini zikiwa zimewekwa katika mifuko ya sandarusi.
Pasipo kukumbuka tarehe, Makuchele alisema Septemba, mwaka huu aliona maiti tatu zilizofungwa katika mifuko ya sandarusi, zikiekea katika eneo la kina kirefu cha bahari upande wa Bagamoyo.
Pia alisema ndani ya mwezi huo huo, alikutana na maiti nyingine mbili zikiwa zimefungwa kwa mtindo huo huo katika eneo la kina kirefu cha bahari kwa upande wa Unguja Shamba.
Makuchele mwenye uzoefu na uvuvi baharini kwa zaidi ya miaka 25, alisema shughuli zake ni za kuhama hama kutokana na eneo wanakopatikana samaki wengi, ndiyo maana hakuweza kutoa taarifa sehemu yoyote.
Akielezea uzoefu katika mambo ya baharini, alisema ni kawaida nyakati za pepo za kusi kukuta maiti zikielea baharini na hali hiyo inatokana na ama wavuvi au wasafiri kutumia vyombo duni ambavyo ni rahisi kuzama kama kukiwa na upepo baharini.
Pia alisema maiti alizoziona zikiwa zimefungwa katika sandarusi ni suala geni kwake.
“Miaka ya nyuma kidogo tulikuwa tunavua samaki huko karibu na Visiwa vya Comoro na ulikuwa msimu wa pepo hizi za kusi, kweli tuliwahi kukutana na maiti kama 10 hivi za watu waliofungwa mikono na miguu, nyingine zimefungiwa mawe kifuani na hilo lilikuwa ni jambo geni machoni mwetu, lakini hizi maiti za sasa za kuwekwa ndani ya mifuko ya sandarusi kama mizigo kwa kweli nastaajabu na sijawahi kuona tangu nimeanza kazi yangu hii,” alisema Makuchele.
Pamoja na Makuchele kudai kukutana na maiti zilizofungwa katika mifuko ya sandarusi kwa nyakati tofauti, lakini naye hajaripoti sehemu yoyote kwa sababu ya kukwepa usumbufu.
Bekuli Haule ambaye pia ni mvuvi katika eneo hilo, alisema kwa mambo aliyoyaona baharini katika kipindi hiki, hawezi kumsimulia mtu yeyote.
Alipoulizwa kama mambo hayo ndiyo maiti zilizowekwa katika mifuko ya sandarusi, alisema atakufa na siri yake moyoni.
Katika Ufukwe wa Kunduchi, Ali Mohamed ambaye ni nahodha wa boti ya uvuvi inayobeba wavuvi 12 hadi 15, alisema Septemba, mwaka huu akielekea katika eneo la uvuvi la kina kirefu cha bahari, kilomita chache kutoka Kisiwa cha Mbudya, alikuta maiti tatu zilizofungwa katika mifuko ya sandarusi zikielea.
Alisema wakati anarejea kutoka katika shughuli zake za uvuvi, alikuta miili miwili, kati ya hiyo, ikiwa imesogea karibu na kisiwa hicho ndipo akachukua jukumu la kutoa taarifa katika Ofisi za Idara ya Hifadhi za Bahari na maeneo tengefu zilizopo kisiwani Mbudya.
“Wakati tunaenda tuliona maiti tatu, moja imewekwa katika mfuko wa sandarusi na mbili zikiwa zimefunikwa kwa mfuko wa plastiki kichwani.
“Wakati tunarudi hatukuona maiti moja, ila tuliziona mbili, ile iliyowekwa katika sandarusi na moja iliyokuwa imevishwa mfuko wa sandarusi kichwani, lakini mfuko ulikuwa tayari umepasuka labda kwa sababu ya maiti kuvimba.
“Niliamua kufika pale kisiwani Mbudya na kuutaarifu uongozi wa Idara ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kisha sisi tukaendelea na kazi zetu,” alisema Mohamed.
Nahodha wa boti katika ufukwe huo, Idrisa Abdallah, alisema kati ya Agosti na Septemba, mwaka huu, ameona mifuko sita ya sandarusi iliyofungawa mizigo na minne kati ya hiyo ilikuwa na maiti.
Abdallah alisema mifuko hiyo ilikuwa imetawanyika katika maeneo mbalimbali ya karibu na visiwa vya Mbudya na Bongoyo.
Alisema baada ya kuona maiti hizo, alitoa taarifa kwa uongozi wa Idara ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu na hajui kilichoendelea baada ya hapo.
“Sio simulizi tu kaka, kwa macho yangu nimeona maiti nne zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi, niliiona mifuko sita usiku wakati nakwenda kuvua, nikajaribu kudadisi nikaona maiti moja wakati tunarudi alfajiri nikaiona tena mifuko ile, ikabidi niidadisi zaidi, nikakuta maiti nyingine tatu na mifuko miwili ikiwa imefungwa kama kifurushi, sasa sikujua kuna nini ndani yake,” alisema Abdallah.
Naye Mjumbe wa Soko la Samaki la Kunduchi, Bakari Poka, alisema pamoja na kwamba maiti zinazokutwa katika mazingira ya kuwekwa katika mifuko ya sandarusi au kufungwa mifuko ya plastiki kichwani, bado haijaonekana katika ufukwe huo, lakini wavuvi wamedai kuona maiti nyingi za aina hiyo katikati ya bahari.
Katika Ufukwe wa Kawe, wavuvi waliokuwapo eneo hilo, walikataa kutoa ushirikiano kwa kile walichokieleza kwamba kuna kamanda wao anayehusika na kuzungumzia jambo lolote kwa niaba yao.
Walipoulizwa mahali alipo kamanda wao huyo, walisema yuko baharini anaendelea na uvuvi na walipoombwa mawasiliano yake ya simu, waligoma huku wakimweleza mwandishi kuwa analazimisha upelelezi.
Baada ya mahojiano hayo kuonekana kuibua hasira miongoni mwao, mwandishi aliachana nao na akaenda kuwahoji baadhi ya wafanyabiashara waliopo eneo hilo.
Justine Khalifani, anayefanya biashara ya chips na peremende katika ufukwe huo, alisema Septemba, mwaka huu ilionekana maiti ikiwa imenasa kwenye mawe ya pembezoni mwa bahari.
Khalifani alisema maiti hiyo ilionekana saa tisa mchana ikiwa imevishwa mfuko wa plastiki kichwani na kufungwa shingoni, huku miguu na mikono nayo ikiwa imefungwa.
Alisema polisi walifika eneo hilo mara moja na kuichukua.
Katika Ufukwe wa Coco, mwandishi alizungumza na wafanyabiashara ambao baadhi walidai kuona maiti tatu na wengine tano.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Hassan Haruna, alisema kati ya Agosti na Septemba, mwaka huu ziliokotwa maiti tatu kwa nyakati tofauti katika ufukwe huo.
Haruna alisema miili yote ilikutwa imewekwa katika mifuko ya sandarusi na imefungwa miguu, kiuno na mikono.
Naye Mathius Tumesana, maarufu kwa jina la Baharia, alisema mwili wa kwanza ulionekana eneo hilo karibu na sehemu wanakouza mihogo.
Alisema baada ya kuonekana, walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na askari walifika kuuchukua mwili huo.
“Mimi nilipiga mbizi kwenda kuuchukua mwili, nilipewa glovu na askari nikaenda kuuchukua, maiti hiyo ilikuwa haijaharibika sana, ila tayari macho yalikuwa yamenyofoka na ilikuwa imefungwa kwa pamoja miguu na mikono kwa nyuma kisha wakamwingiza katika mfuko mkubwa wa sandarusi,” alisema.
Tumesana alisema baada ya wiki tatu, ilionekana miili mingine miwili katika eneo hilo hilo, ikiwa imefungwa katika mifuko ya sandarusi na mwishoni mwa Septemba, mwaka huu ulionekana mwili mwingine ukiwa umefungwa kwa mtindo huo huo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wafanyabiashara wa Ufukwe wa Coco, Abdallah Hassani, alisema matukio hayo ameyasikia, lakini hajaziona maiti hizo kwa sababu hakuwapo katika eneo lake la biashara kwa muda mrefu.
Safari ya Mbudya
Uchunguzi wa gazeti hili ulikwenda mbali zaidi kwa kutembelea Kisiwa cha Mbudya kunakodaiwa kuonekana maiti kadhaa.
Nahodha wa boti ndogo, Hassan Ramadhan, anayesafirisha watalii kwenda Mbudya na Bongoyo, alisema katika ufukwe huo kuelekea eneo la White Sand, zilionekana maiti mbili zilizofungwa katika mifuko ya sandarusi.
“Ukiacha tukio hilo, siku moja jioni nilikuwa nafuata watalii katika Kisiwa cha Bongoyo nikitokea Mbudya, hapo katikati niliona maiti nne zikielea, huku zikiwa zimevishwa mifuko ya sandarusi miguuni na kufungwa kwa kamba.
“Nilipata hofu sana na ilikuwa inasukumwa na mawimbi kuelelea Ufukwe wa Kawe.
Kutoka Mbundya hadi Bongoyo ni takribani kilomita nne, hapo kuna uwazi mkubwa kutoka eneo lenye kina kirefu cha bahari na ukidadisi vizuri simulizi za wavuvi, miili mingi inaonekana katika eneo hilo kwa nyuma, ambako kuna mkondo mkubwa wa bahari na mawimbi yana nguvu sana,” alisema Ramadhani.
Mwandishi wa habari hii alipanda boti na kuelekea Mbudya ambako alifanikiwa kumhoji Ofisa Utalii na Uwekezaji wa Idara ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Hussein Ngenje, aliyesema hana cha kuongea kuhusu suala hilo.
Alipoulizwa kama ana taarifa yoyote alijibu: “No coment.” Kisha alimtaka mwandishi akamuulize Mwenyekiti wa Mbudya, Khamis Azizi.
Alipoulizwa Azizi kama ana taarifa zozote juu ya kuonekana kwa maiti iliyofungwa katika sandarusi, alisema hawezi kuongelea jambo hilo hadi apewe ruhusa maalumu kutoka mamlaka za juu.
Alipoulizwa mamlaka za juu ni zipi, alisema ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu.
Alipofuatwa Meneja wa Idara ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu zilizopo Upanga, Dar es Salaam, Dk. Milali Machumu, alikiri kupata taarifa mara mbili kuhusu maiti hizo na alizifikisha kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa utaratibu wa kuziopoa.
Alipoulizwa idadi ya maiti zilizookotwa, alisema hafahamu kwa sababu jambo la msingi kwake alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za uopoaji.
“Sina ufafanuzi zaidi kwa kuwa lengo letu la msingi ni utalii, nadhani naomba nikomee hapo, ila taarifa nilipewa na mimi nikazifikisha katika ngazi husika ya usalama wa raia,” alisema Dk. Machumu.
Septemba 26, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alitoa taarifa ya matukio ya kuonekana maiti zilizowekwa katika mifuko ya sandarusi na kutupwa baharini.
Alisema kutokana na matukio hayo, jeshi hilo kwa kushirikiana na askari wa majini, wanaendelea na uchunguzi dhidi ya matukio ya mauaji yanayoendelea kutokea katika baadhi ya maeneo na kisha miili kutupwa.
Pia alisema matukio hayo yanaonekana kudhamiriwa na watu wanaoyafanya kwa sababu miili yote inakutwa imefungwa kamba.
“Jeshi la Polisi tunaendelea na ufuatiliaji tukishirikiana na askari wa majini, kwa sababu matukio haya yanatokea huko, kama kanda tunaendelea na uchunguzi wa hali ya juu na hawa wauaji wanakuwa wanadhamiria kabisa kufanya hivyo. Ni vifo vya shaka kwa kweli, yote inakutwa imefungwa, hii inamaanisha huyo mtu anadhamiria,” alisema Mambosasa.
Alisema miili mingine iliyookotwa katika Ufukwe wa Msasani haikujulikana ni kina nani na hakukuwa na mtu aliyekwenda kuripoti kupotelewa na ndugu yake, hivyo waliikabidhi Manispaa ya Kinondoni kuizika.