32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

ZINATAKIWA HATUA MADHUBUTI KUINUSURU DAR NA MAFURIKO

KWA mara nyingine, mvua imesababisha uharibifu, matatizo, adha na usumbufu mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam.

Mvua hiyo iliyonyesha kwa siku mbili imeleta  vifo, kubomoa nyumba, kuharibu barabara na madaraja na kubomoa nyumba huku makazi ya watu katika maeneo mbalimbali na barabara nyingi zikijaa maji.

Safari hii hata huduma ya mabasi ya mwendo wa haraka ilibidi isimamishwe jana baada ya barabara sehemu ambayo mabasi hayo yanapita (hasa Msimbazi na Jangwani),  nayo kujaa maji!

Ni hali inayodhihirisha jinsi ambavyo Jiji la Dar es Salaam liko hatarini muda wote mvua (kubwa) inaponyesha. Kinachoshangaza ni kwamba hali hiyo haikuanza jana wala leo bali imekuwa ikijitokeza miaka nenda rudi.

Kwa nini hazichukuliwi hatua madhubuti kuhakikisha tatizo hilo linatafutiwa ufumbuzi  kama siyo angalau kupunguzwa?

Kwa mfano, kukosekana mifereji ya maji ya mvua katika barabara nyingi za Jiji ni jambo la kawaida na ambalo pia liko kwa miaka chungu nzima.  Barabara zinajengwa bila mifereji ya  maji ya mvua.

Ndiyo sababu mvua ikinyesha hata iwe ndogo, harakaharaka maji hutuama barabarani na inaponyesha kubwa, barabara nyingi zinakuwa kama mto!

Vilevile kuziba mifereji ya maji ikiwamo ya maji machafu, nacho kimekuwa kitu cha kawaida.  Mara nyingi mifereji mingi huwa imejaa taka kiasi kwamba mvua inaponyesha ni rahisi kuziba.

Hakuna hatua zozote madhubuti ambazo huchukuliwa kuizibua mifereji hiyo hata wakati ambao  mvua hainyeshi.

Tunatambua pia kwamba ujenzi holela, hasa zile ambazo zilikuwa ni mapitio ya maji zamani zikiwamo za mabondeni, ni miongoni mwa sababu za mafuriko jijini mvua inaponyesha.

Lakini,  tunachosema ni kwamba angalau zingekuwapo juhudi  za kutosha kuhakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa salama mvua inaponyesha.

Hatua hizo zingekuwa zinachukuliwa kwa awamu, kwa maana kwamba kila halmashauri (Ilala, Temeke, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni) zipewe majukumu maalum kama siyo kuwapo operesheni maalum.

Hatua hizo ziwe na lengo la kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha barabara zote zinakuwa na mifereji ya maji ya mvua, zikiwamo zinazojengwa sasa.

Vilevile, kuisafisha  mifereji ya maji machafu wakati wote isiweze kuziba kwa namna yoyote ile.

Jambo jingine muhimu ni kuhakikisha jiji linakuwa na mpangilio mzuri wa majengo, hasa nyumba za kuishi ambazo nyingi zimejengwa ovyoovyo katika maeneo ambayo hajayapimwa.

Kwa mara nyingine tunasema, watendaji na viongozi katika Jiji la Dar es Salaam hawana budi kuchukua hatua za makusudi za haraka na endelevu kuwanusuru wakazi wake na adha wanazokabiliana nazo, kila mara mvua inaponyesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles