30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 9, 2022

BENKI YA TPB YATOA MSAADA HOSPITALI YA KIGOMA

Na Editha Karlo -KIGOMA

BENKI ya TPB imetoa msaada wa mashuka 50 na magodoro 20 katika Hospital ya Mkoa wa Kigoma (Maweni), vyenye thamani ya Sh milioni 4.2 kwa wodi ya wazazi.

Akikabidhi msaada huo jana mjini hapa, Mkurugenzi wa Tehama na Uendeshaji wa TPB, Jema Msuya, alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa sekta ya afya katika nchi, kwa kuunga mkono juhudi za dhati za Serikali ya awamu ya tano kwa kuimarisha sekta hiyo.

“Sote tunajua afya ni kitu muhimu katika maisha ya binadamu, na ukiwa na afya njema utaweza kufanya kazi zako kwa ufanisi, hivyo basi Benki ya TPB inaunga mkono Serikali kwa jitihada zake inazofanya za kuboresha afya za wananchi,” alisema Msuya.

Alisema TPB hutenga fungu kila mwaka katika bajeti yake inayotokana na faida wanayopata kwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo elimu na afya.

Mkurugenzi huyo pia aliwataka wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wastaafu, wafanyakazi na vikundi mbalimbali, kufungua akaunti kwenye matawi yao kwani watapata huduma bora na za haraka na kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Mkoa wa Kigoma, Dk. Fadhili Kibaya, aliishukuru TPB kwa msaada waliotoa kwani utasaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zinawakabili, ikiwamo uhaba wa magodoro na shuka.

Alisema Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ina uhaba mkubwa wa madaktari bingwa. Kwa sasa wapo wawili ambao hawatoshi kuhudumia wananchi.

“Hapa tuna changamoto pia ya uwepo wa madaktari bingwa, tuna madaktari bingwa wawili tu ambao ni wachache ukilinganisha na mahitaji ya huduma, hivyo tunaiomba Serikali ituongezee madaktari,” alisema Dk. Kibaya.

Licha ya hali hiyo, aliwataka wadau wengine kuunga mkono kwa kusaidia sekta ya afya, hasa hospitali za Mkoa wa Kigoma kama wanavyofanya Benki ya TPB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,291FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles