25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MZIMU WA LUKAKU BADO UNAWATESA EVERTON

NA BADI MCHOMOLO


KOCHA wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho na uongozi wa klabu hiyo uliona mbali sana kuhakikisha katika kipindi cha usajili wa majira ya joto wanakiboresha kikosi chao hasa katika safu ya ushambuliaji na kiungo.

Waliamini kuwa mshambuliaji wao ambaye alikuwa ni nahodha wa timu hiyo Wayne Rooney ni maji ya jioni, hawezi tena kuwa kwenye kiwango chake cha miaka miwili iliopita, hivyo United walitupa jicho lao hadi kule kwenye viwanja vya Goodison Park, ambapo ni maeneo ya Everton ya kujidai.

Walimuona mshambuliaji wa timu hiyo Romelu Lukaku akiwa kwenye ubora wake wa kupachika mabao na ndipo walifikia maamuzi magumu ya kufikiria kuachana na mshambuliaji wao Rooney aliyowafanyia makubwa kwa kipindi kirefu.

Kumbe Manchester United walikuwa sahihi kupambana na wapinzani wao ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Chelsea, katika kuwania saini ya mchezaji huyo. Chelsea walikuwa na lengo la kumrudisha kikosini mchezaji huyo na hapo ndipo ushindani ulipoanza.

United walitangaza kuamuacha Rooney, hivyo Everton wakajaa na kuamua kumuacha mshambuliaji wao Lukaku ajiunge na Man United ili wao wamrudishe mchezaji wao wa zamani Rooney.

Everton walikuwa sahihi kumuacha Lukaku kuondoka kwa kipindi hicho kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichokiweka Man United, pauni milioni 75, huku mchezaji mwenyewe akigoma kuongeza mkataba mpya.

Lukaku alikuwa tayari kukaa huku akisubiri mkataba wake umalizike ili aondoke bure, hivyo Everton walilazimika kumuuza mchezaji huyo kwa shingo upande na kumpa nafasi Rooney huku wakiamini kuwa anaweza kuziba nafasi hiyo hasa katika kupachika mabao, lakini hali imekuwa tofauti.

Everton wamekuwa kwenye ukame wa mabao tangu Rooney ajiunge ikiwa amefanikiwa kupachika mabao matatu katika michuano ya Ligi Kuu wakati huo upande wa Lukaku ndani ya Man United amekuwa kinara wa kupachika mabao pamoja na Ligi Kuu kwa ujumla akiwa na jumla ya mabao saba kabla ya michezo ya mwishoni mwa wiki iliopita.

Manchester United wamefanikiwa kulamba dume kwa Lukaku, wakati huo Everton wakiendelea kuteseka na mzimu wa mchezaji huyo kwa kuwa mashabiki wana kiu ya kuiona timu yao ikiwa inashinda mara kwa mara kama ilivyo wakati mchezaji huyo yupo kikosini.

Manchester United kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi England kabla ya michezo ya mwishoni mwa wiki, wakati huo Everton wakiwa wanashika nafasi ya 16 baada ya kucheza michezo nane na kuvuna pointi nane.

Mabao saba aliyofunga Lukaku ametumia dakika 720 kwa michezo yote aliyocheza huku akitoa pasi moja ya mwisho, wakati huo Rooney akitumia dakika 612, lakini hajatoa pasi hata moja ya mwisho.

Rooney mwenye umri wa miaka 31, bado ana deni kubwa sana kwa mashabiki wa Everton ambao walimuamini kuwa anakuja kuitendea haki timu yake ya zamani, hivyo ni lazima ajitoe kwa hali na mali kuwakonga nyoyo zao.

Lakini unaweza kusema amekuja na gundu baada ya wiki chache zilizopita kupigwa faini na uongozi wa timu hiyo kutokana na kuendesha gari huku akiwa amekunya pombe kupita kiasi.

Klabu ilifikia hatua ya kumkata mshahara wa wiki mbili ambao ni pauni 300,000 huku kila wiki akiwa anachukua pauni 150,000 nusu ya mshahara ambao alikuwa anauchukua katika klabu ya Manchester United akiwa kama nahodha kabla ya kujiunga na Everton.

Lukaku hakuwa anayafanya hayo ndani ya Everton, akili yake kila wakati ilikuwa inawaza gori, kumbe ilikuwa njia pekee ya yeye kukaa sokoni vizuri, hivyo Everton wataendelea kukumbuka mchango wa Lukaku msimu huu wote kwa kuwa Rooney hawezi kuwafanya mashabiki wa timu hiyo wakamsahau mchezaji huyo, ana kazi kubwa ya kufanya.

Wapo ambao wanaamini kuwa hii ni safari ya mwisho ya mfalme wa soka nchini England, Rooney, hatoweza kurudi katika kiwango kile alichokionesha miaka mitatu iliopita, kuna uwezekano msimu ujao akaonekana akiwa anatokea benchi kutokana na kasi ya wachezaji chipukizi na yeye atabaki kuwa kama mkongwe.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles