27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAMJIBU ZITTO TAWIMU ZA UCHUMI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


 

SERIKALI imemtaka kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe kuweka hadharani ushahidi wa takwimu alionao kuhusu mwenendo wa Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka.

Hatua hiyo ya serikali imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Zitto  kuibua madai kuwa takwimu za serikali kuhusu Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka zimepikwa.

Akizungumza jana na MTANZANIA kwa simu yake ya kiganjani, Mkurugenzi Mkuu wa MAELEZO na Msemaji wa Serikali Dk. Hassan Abbasi alisema Zitto hana uhalali wa kisiasa, kiuchumi wala kijamii kukosoa takwimu za serikali kwa sababu hana vyombo vya kupima uchumi wa nchi lakini serikali inavyo.

“Kwanza Tanzania ipike data kwa hoja gani? Zitto huyu huyu alidanganya umma kuwa mapato ya serikali yameshuka, leo hawezi kuaminika, sasa kama anadhani ana takwimu zinazopingana na hizi za serikali aziweke hadharani,” alisema Dk. Abbasi.

Alisema Zitto amekosa ajenda za kuwatumikia wananchi wake jimboni na sasa anashikilia ajenda ambazo hazina mashiko.

Dk. Abassi alisema Zitto ni msomi hivyo ana wajibu wa kuwaamini wasomi wenzake kwa sababu wanaotoa takwimu ni vyombo vilivyoundwa kisheria na vina wataalamu wanaoaminika ndani na nje ya nchi.

“Zitto ni msomi ana wajibu wa kuwaamini wasomi wenzake kwa sababu wanaotoa takwimu ni Benki Kuu (BoT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Hivi ni vyombo vilivyoundwa kisheria, vina wataalamu wanaoaminika ndani na nje ya nchi hivyo ana wajibu wa kuwaamini wataalamu.

“Zitto huyu huyu zikitoka takwimu zinazomfurahisha yeye huwa anazitumia na kuziamini na kuzitangaza kutoka taasisi hizo hizo, si mara ya kwanza wala ya pili.

“Ametumia takwimu za BoT pale ambapo kuna jambo halijakaa vizuri kufanyia siasa. Hivyo anapaswa ajenge tabia ya kuwa na subira,” alisema Dk. Abbasi.

Aidha, Dk. Abbasi alivitaka vyama vya siasa kutambua kuwa kuweka siasa katika kila jambo kumepitwa na wakati.

Takwimu waja juu

Akizungumza kauli hiyo ya Zitto, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa alisema katu ofisi yake haiwezi kuchezewa na watu kwa masilahi yao kisiasa badala ya kuheshimu kazi ya wataalamu.

Alisema suala la takwimu za kiuchumi hupimwa kitalaamu na si kisiasa na kwamba takwimu zilizopo zinaonyesha Tanzania imekuwa ya pili kwa kuwa na takwimu bora Afrika.

“Kwanza ninapenda kukanusha kwa nguvu kauli ya Zitto kuhusu hali ya uchumi eti takwimu zinapikwa, jamani hii ni nchi yetu, NBS ni ofisi yenye wataalamu waliobobea na kama Mheshimiwa Zitto alikuwa hakuelewa angerudi kwetu kuuliza tungemsaidia kumwelewesha.

“Haiwezekani mtu anakaa kisha anatoka mbele ya umma na kupotosha suala la takwimu za uchumi wa nchi jambo ambalo ni hatari kwa Taifa. Ninasema mwaka 2015 Bunge lilipitisha Sheria ya Takwimu na kifungu cha 37 kinaeleza adhabu kwa mtu anayesema uongo, sasa tutaanza kuitumia bila kujali jina wala cheo cha mtu,” alisema Dk. Chuwa

Alisisitiza kuwa takwimu zilizotolewa na serikali ni sahihi na jambo lililo wazo kuwa hivi sasa hali ya uchumi wa nchi umeendelea kukua kutokana na uzalishaji wa mazao kuwa mzuri.

“Ninarudia tena kusema takwimu zetu zinaheshimiwa na hupimwa na Shirika la Fedha Duaniani (IMF) pamoja na Benki ya Dunia,  na hata hivi karibuni tulikuwa kwenye kikao cha Shirika la Takwimu la Umoja wa Mataifa, wote wamekubali takwimu zetu na kusifu hali ya uchumi wa nchi yetu.

“…kauli nyingine za wanasiasa ni hatari kwa uchumi wa nchi waache kufanya hivyo kwani NBS inaendeshwa na wataalamu tuachiwe tufanye kazi yetu. Yeye kama ana vipimo vyake vya uchumi aleta tuje tuvione kwa mujibu wa viwango vya kimataifa badala ya kusema pembeni.

“Kauli za namna hii ni za uchonganishi na kukosa uzalendo kwa nchi yetu, ninamuheshimu mheshimiwa Zitto kama kuna mahali alikuwa hajaelewa kwa nini asinipigie hata simu kunikuliza. Kwa hili narudia tena watalaamu tuachwe tufanye kazi yetu na si kuingiliwa na watu wanapotosha takwimu huria,” alisema Dk. Chuwa.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, juzi katika mkutano wake na waandishi wa habari alikaririwa kuwa takwimu zilizotolewa na BoT kuhusu pato la taifa zina shaka.

Alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa takwimu hizo zimepikwa ili kuonyesha kuwa hali ya uchumi ni nzuri wakati siyo kweli.

Akindika katika mitandao ya kijamii, Zitto alidai hali ya uchumi ni mbaya, thamani ya shilingi imepoteza uwezo wake, mfumuko wa bei umepanda kwa kasi hasa vyakula na mahitaji muhimu.

Katika andishi lake hilo mitandaoni, alitaja maeneo mengine yanayoporomoka kwa kasi kuwa ni uzalishaji katika kilimo, mikopo kwa sekta binafsi, uzalishaji katika sekta ya viwanda aliodai umeshuka zaidi ya nusu huku mapato ya serikali yakididimia.

Andishi lake hilo lilisomeka kuwa taarifa ya serikali iliyotolewa kipindi cha Juni hadi Julai, mwaka huu kuhusu mikopo katika sekta binafsi inaonyesha ukuaji wa mikopo imeporomoka kutoka asilimia 24 hadi sifuri.

Zitto ambaye kitaaluma ni mchumi, aliandika zaidi kuwa madhara ya kuporomoka kwa mikopo yataathiri viwanda katika uzalishaji wake.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema ripoti hiyo ya robo ya pili ya pato la taifa iliyotolewa na BoT, yaani Juni, Mei na Aprili, mwaka huu imefanyiwa utafiti na chama chake lakini kwa kuwa ni suala la kisera litawasilishwa kwenye Kamati Kuu kujadiliwa.

“Tumegundua kasi ya ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.7 kiuhalisia ni mbaya zaidi, si nne, tatu, mbili wala si moja. Uchambuzi umekamilika na tumewasiliana na wachumi mbalimbali kwa ajili ya kutazama jambo hilo kabla ya kulisema.

“Tutakapoliwasilisha Kamati Kuu mtaweza kulipata na liko katika lugha nyepesi hata mtu wa kawaida atalielewa kwanini tunasema takwimu zimepikwa. Hakuna ukuaji kati ya Aprili hadi Juni, mwaka huu,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alisema moja ya hoja za uchumi atakazowasilisha katika Kamati Kuu ni taarifa za kuchotwa kwa fedha za mashirika ya umma na kutumiwa na serikali bila kufuata sheria.

“Kuna mashirika matano hadi sasa hayana fedha za kujiendesha, tumekubaliana hilo nitaliwasilisha katika Kamati Kuu ya chama na litajadiliwa kisha nikaliwakilishe bungeni,” alisema.

Pia alisema suala hilo linahitaji muda kujadiliwa na kwa kuwa ni jambo linalovunja misingi ya sheria za fedha na linatokana na kuwa na Bunge dhaifu.

“Kamati ya Bunge ya Bajeti ina uwezo wa kudhibiti hilo iwapo Bunge ni imara,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles