Na MWANDISHI WETU
HATIMA ya maridhiano katika maeneo 14 kati ya Serikali na Kampuni ya Kimataifa ya Uchimbaji wa Madini ya Barrick Gold, yaliyolenga kutatua mzozo wa udanganyifu unaodaiwa kufanywa kwenye mchanga wa madini (makinikia), ipo mikononi mwa wajumbe saba wa Bodi ya Kampuni ya Acacia.
Wiki hii baada ya Serikali ya Tanzania kufikia maridhiano pamoja na mambo mengine kwa kampuni hiyo kukubali masharti yote ya sheria, ikiwa ni pamoja na kutoa asilimia 16 ya hisa zake kwenye kila mgodi wake nchini, asilimia 50 ya faida ya mauzo na zaidi ikitoa Sh bilioni 700, Acacia ilitoa taarifa ikisema kuwa, inahitaji kupelekewa mapendekezo rasmi juu ya kilichoafikiwa ili iyapitie na kutoa uamuzi.
Bodi ya Acacia, ambayo kimsingi ndiyo ina uwezo wa kuamua kupitisha au kutopitisha mapendekezo hayo, inaundwa na Kelvin Dushnisky, Brad Gordon, Andre Falzon, Michael Kenyon, Steve Lucas, Rachel English na Stephen Galbraith.
Acacia jana ililiambia MTANZANIA Jumapili kuwa bado bodi yake haijafanya uamuzi wowote juu Sh. Bilioni 700 wala makubaliano mengine yote yaliyofikiwa kati ya Barrick na Tanzania.
Alipoulizwa na gazeti hili juu ya utata uliojitokeza wa malipo ya Sh bilioni 700 ambazo Barrick imesema itailipa Serikali ya Tanzania, huku Acacia ikigoma kwa maelezo kuwa haina fedha hizo, mshauri mwenza wa Acacia hapa nchini, Dickson Senzi alisema hataki kuamini kama kauli hiyo ni ya kweli.
Juzi, Shirika la Habari la Kimataifa la Reuters, lilimkariri Mkurugenzi wa Fedha wa Acacia, Andrew Wray, akisema Kampuni hiyo haina uwezo wa kulipa fedha hizo.
“Labda walimkariri vibaya, kwa sababu kulipa au kutolipa ni uamuzi wa bodi, kwa sababu yale ni makubaliano ambayo inabidi yapitishwe kwenye bodi ya kampuni hiyo ndipo uamuzi utoke,” alisema Senzi.
“Hadi sasa Acacia hawajapata formal proposal (mapendekezo rasmi), watakapopata, bodi itafanya uamuzi,” alisisitiza Senzi.
Alisema tayari Acacia imekwishapokea muhtasari wa kile ambacho Barrick na Serikali ya Tanzania wamekubaliana na kwamba kinachosubiriwa sasa ni hayo mapendekezo (formal Proposal).
Kuhusu kuwapo kwa hisia kwamba Sh bilioni 700 ambazo Barrick wamesema wanazitoa wakati mazungumzo ya malipo mengine yakiendelea ni danganya toto, Senzi alisema ni mapema mno kutabiri mazungumzo ya kamati ndogo iliyoundwa kwa ajili ya kutatua mzozo wa kiasi cha zaidi ya Sh trilioni 400 ambazo Serikali ya Tanzania inasema iliibiwa kupitiwa mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa nje kwa takribani miaka 20 sasa.
“Ninachojua hizi bilioni 700 zimetolewa kama ‘good faith’, tusubiri kamati ndogo iliyoundwa imalize kazi yake kwanza.” alisema.
Alipoulizwa kuhusu namna faida ya asilimia 50 kwa 50, Barrick pamoja na Acacia watakavyogawana na Serikali ya Tanzania, wakati kukiwa na taarifa zinazodai kwamba kampuni hiyo imekuwa ikitangaza hasara na kwamba wanachofaidika ni kuuza hisa, Senzi alisema hilo watalizungumza watakapopata mapendekezo rasmi.
Pamoja na hilo, Senzi alisema mazungumzo ya kutatua mzozo wa madini kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hizo za madini kwa kiasi kikubwa yamekamilika.
Jana kwa mara nyingine Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alizungumzia suala la makubaliano kati ya Kampuni ya Barrick Gold na Serikali, akisema ni moja kati ya mambo yatakayojadiliwa na Kamati Kuu ya chama chake itakayoketi wiki ijayo.
Zitto, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, akiwa ameongozana na viongozi wenzake, akiwamo Kaimu Mwenyekiti Taifa, Yeremia Maganja, alisema suala la Barrick ni kama kila mmoja alimkuna mwenzake mgongo, kwa kuwa serikali nayo ilikuwa ikitaka ndege yake iliyoshikiliwa nchini Canada kuachiwa.
Aliyaita makubaliano hayo kuwa si makubaliano na kwamba hakukuwa na uwezekano wa kugawana 50 kwa 50 kwa kuwa haikuwekwa wazi suala la gharama ambazo zilipaswa kuondolewa kabla ya kupata faida.
Zitto alisema kuwa, changamoto inayotukabili ni kuzidiwa maarifa katika mfumo wa kodi wa kimataifa na umiliki.
Alisema mfumo wa kodi wa kimataifa unayaruhusu makampuni kufungua makampuni dada kwenye nchi zenye kodi ndogo ambako wanajaza gharama huko na kuonekana kuwa hakuna faida.
Alisema mgodi wa almasi wa Williamson ulikuwa na hisa ya 50 kwa 50 miaka yote tangu utawala wa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na mgodi wa Tanzanite One asilimia 25, lakini haikuwahi kupatikana faida.
Alisema Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, anajua kuwa hilo haliwezekani na yeye (Zitto) aliwahi kumwelewesha kuhusu mfumo huo wa kodi na umiliki.
Alisema hilo linawezekana iwapo mwekezaji atafanywa kuwa kandarasi na kulipwa gharama zake kama inavyofanyika katika sekta ya gesi na mafuta.
Zitto pia alihoji ukimya wa Serikali kuhusu makontena ya makinikia yaliyokuwa yakishikiliwa na kuhoji yatakakopelekwa.
Mbali na hilo la kugawana hisa na faida, makubaliano mengine yaliyoafikiwa kati ya Barrick na Tanzania na ambayo Acacia inayasubiri ili iweze kuyapitia, ni kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini ambayo itakuwa na makao makuu Mwanza na Dar es Salaam, badala ya nchini Uingereza kama ilivyo sasa.
Pia kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg, Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania.
Barrick Gold Corporation imekubali kuwapo kwa wawakilishi wa serikali katika bodi za migodi yake yote nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania.
Pia migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye kambi ya migodi na mashauri yote yafanyikie nchini.
ACACIA NI NANI HASA?
Hatua Acacia, yenye hisa asilimia 36.1, huku kampuni mama ya Barrick ikiwa na 63.9, kuyataka mapendekezo hayo ili yaweze kupitishwa na bodi yake, imezua maswali mengi, baadhi wakihoji wanaounda chombo hicho ni akina nani? Na je, kama kinaweza kuyatupa au kutoyatupa mapendekezo hayo.
MTANZANIA Jumapili limefanya uchambuzi wa aina ya watu wanaounda bodi hiyo ya Acacia ambao unaweza kukupa taswira juu ya uamuzi ambao unaweza kufikiwa pindi mapendekezo rasmi yatakapofika mezani kwao.
Miongoni wa watu wanaounda bodi hiyo ni Kelvin Dushnisky, ambaye amekuwa Rais wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation tangu Agosti, 2015.
Akiwa na uzoefu wa kimataifa wa masuala ya uchimbaji wa madini kwa miaka 25, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Acacia Julai, 2012.
Dushnisky ana wajibu wa juu kabisa wa usimamizi wa mikakati na vipaumbele vya Kampuni ya Barrick, ambako pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Dushnisky ni mwakilishi wa Kampuni ya Barrick kwenye baraza la dunia la madini ya dhahabu.
Kwa upande wake Brad Gordon, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia, Agosti mwaka 2013.
Gordon, ambaye anatajwa kusimamia zaidi maslahi ya Acacia, kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Intrepid Mines, kabla ya hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DRDGold na mwandamizi wa Kampuni ya Placer Dome.
Akitumikia kampuni ya Placer Dome, Gordon aliweza kupata mafanikio makubwa ya uzalishaji kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji kiasi cha kufikia ufanisi wa hali ya juu uliosaidia kurejesha na kuimarisha uhai wa migodi iliyokuwa inamilikiwa na kampuni hiyo.
Andre Falzon kwa upande wake ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni ya Acacia.
Kwa uzoefu, Falzon amekuwa mwandamizi wa masuala ya fedha na uongozi katika sekta ya madini kwa zaidi ya miaka 25, pia amewahi kuwa makamu rais na kiongozi kati ya mwaka 1994 na 2006.
Michael Kenyon naye ni Mkurugenzi Mshauri wa Acacia na ana uzoefu wa miaka 40 katika uchimbaji wa madini na ufundishaji wa masuala ya miamba.
Amewahi kushika nyadhifa za juu katika kampuni za Detour Gold Corporation, Troon Ventures Ltd, Canico Resource Corp na Sutton Resources Ltd na Cumberland Resources Ltd .
Steve Lucas ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni ya Acacia, akiwa amebobea katika masuala ya uhasibu na amekuwa na uzoefu mkubwa katika masuala ya nishati na uziduzi.
Kabla ya nafasi hiyo, kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa kiongozi katika kampuni za National Grid plc, Shell, BG Group, Ferrexpo plc na Tullow Oil plc.
Rachel English naye ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni ya Acacia. Ni mjumbe wa Taasisi ya Chartered Accountants, pia ni mmoja wa watendaji waandamizi wa Kampuni ya BGGroup na Royal Dutch Shell, akiwajibika na masuala ya fedha, mikakati na maendeleo ya biashara.
Amewahi kufanya kazi Benki ya Dunia na Benki ya Ulaya, pia ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni ya Kuwait Energy plc, Adam Smith International na Helios Social Enterprise.
Stephen Galbraith ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni ya Acacia. Ni mwajiriwa wa Kampuni ya Barrick tangu Agosti, 2000, katika kitengo cha mali na fedha na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Barrick International (Barbados) Corporation.