Na ANSBERT NGURUMO- BUKOBA
KATIKA miaka mwili ya kwanza ya serikali ya awamu ya nne, wapambe wa Rais Jakaya Kikwete waliunda kikosi cha kumjenga, kumnadi na kumsifu rais hata kwa sifa zisizo zake.
Wapo waliodiriki kusema Kikwete ni Nyerere mpya! Walijua hakuwa Nyerere mpya, lakini walitambua kuwa kumfananisha na Nyerere kungemwongezea mvuto na ushawishi kwa wananchi.
Bahati nzuri kwake, Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 akiwa anapendwa na umma. Alipata kura nyingi za kweli.
Miaka 10 baadaye, wananchi waligundua kuwa kuna mambo kadhaa alifaulu kutenda au kuyasimamia, lakini hakuwa Nyerere, wala hakuwa na unyerere wowote.
Hadi 2015, wapika propaganda wake walishapoteana, na wananchi walishatambua shimo kubwa la sifa kati ya Nyerere na Kikwete.
Propaganda hizo zimeanza tena. Tayari kuna kundi nje na ndani ya chama cha rais wa sasa, kinamsifu kwa kumvisha Unyerere. Hawajifunzi kutokana na makosa yao au ya wenzao.
Ukiondoa ukweli kwamba Rais John Magufuli aliingia kwenye siasa akitokea kwenye ualimu kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yeyote anayemjua vema na kumheshimu Mwalimu Nyerere hawezi kumwona katika nafsi ya Magufuli.
Mwalimu Nyerere alikuwa mmoja wa wasomi wa kizazi chake cha viongozi waliokuwa na upeo wa kuona mbali na kutafakari mambo kwa kina.
Nyerere alikuwa mtu wa misingi – bila shaka kutokana na malezi ya kifalsafa. Aliheshimu wadogo na wakubwa.
Mwalimu Nyerere alijua dunia inakwenda vipi. Kuna wakati alithubutu kuipinga ikamgomea. Hata alipoanzisha sera au programu, alizipima katika msukumo wa kidunia.
Na alipogundua kuwa mawimbi ya kidunia ni mazito kuliko yeye, alibwaga manyanga kistaarabu.
Alitawala kwa mkono wa chuma uliotetewa na katiba na sheria zake, na wakati mwingine alikosana na waliompinga akawaweka kizuizini kwa sheria mbovu za kikoloni, lakini kuna wakati aliheshimu ujuzi wa waliomkosoa.
Edwin Mtei, akiwa waziri wa fedha, alipomshauri Nyerere kuachana na ujamaa au kulegeza masharti akakataa, waziri alijiuzulu.
Rais Nyerere hakuwa na kinyongo naye. Ilipohitajika nafasi ya mkurugenzi katika Shirika la Fedha Duniani, Mwalimu Nyerere alimpendekeza Mtei yule yule aliyemkatalia ujamaa wake.
Licha ya ukali wake na mfumo mbovu kikatiba, Mwalimu Nyerere hakuwahi kuruhusu kashfa ya vyombo vya dola kufyatulia wapinzani wake risasi mchaka kweupe.
Akiwa rais, alikuwa na uwezo wa kuzungumza na kushawishi wananchi wakamwelewa. Hata wakati wa shida, alijijengea sifa ya kuwa mfariji mkuu wa taifa.
Hakuwa kiongozi mwenye kusimanga wananchi wake. Serikali yake haikuwahi kushutumiwa kwa kuchangisha fedha za maafa na “kuzibadilishia matumizi” huku wananchi wakihangaika.
Hakuwa anatoa hotuba za kufokea wananchi wake wenye njaa, na kutisha wakuu wa wilaya waliodiriki kumweleza kuna njaa. Alizungumza nao. Aliwapa matumaini.
Wala hakuwa anatumia muda mrefu kulaumu wakoloni waliomwachia nchi ikiwa duni. Aliweka mipango ya kubadilisha nchi yake, hasa kati ya 1965 na 1977. Baada ya vita ya Uganda, upepo ulibadilika.
Kila mara taifa lilipopigwa na njaa, serikali iliingilia kati na kutoa msaada wa chakula. Rais alijua na kutekeleza wajibu wa serikali.
Mwalimu Nyerere hakukwepa mikutano ya kimataifa. Alitambua kuwa huko ndiko walipokuwa viongozi wa hadhi yake, na kwamba kwa kuchangamana nao angeweza kushawishi na kupenyeza ajenda za Tanzania na Afrika.
Alijiamini na hakuhitaji kukumbusha wananchi kwenye hotuba zake mara kwa mara kwamba yeye ndiye rais. Na kwa wakati wake, wananchi walitambua tu bila kuambiwa, aliamini urais unaendana na uelewa wa mambo, upeo, uvumilivu, wema, busara, na mamlaka yanayoheshimika.
Kwa miaka 24 aliyokuwa rais, Nyerere aliendelea kuwa mwalimu kwa kila mwanachi. Hotuba zake zilikuwa na ujumbe mzito wenye kujenge uelewa au ushawishi wa kimaendeleo.
Hata pale ambapo hakusoma hotuba zake, wasikilizaji wake waligundua kwamba ama zilikuwa zimeandaliwa au alikuwa ameshauriana na wasaidizi waliobobea.
Licha ya ukweli kwamba alipinga ubepari na ubeberu, Mwalimu Nyerere hakushabikia umaskini.
Na ndiyo maana alisisitiza kuwa ujamaa si umaskini wala utajiri, bali imani – kwamba hata tajiri angeweza kuwa mjamaa.
Kwa mfano, alipohutubia watawa wa Maryknoll aliwaeleza kuwa anatambua wito wao na fadhila yao ya umaskini, lakini anatambua pia kuwa Mungu aliumba mtu kwa sura na mfano wake. Akasema ujinga na umaskini si sifa ya Mungu.
Nyerere alikuwa muumini wa kweli wa imani yake katika madhehebu ya kikatoliki. Kwake, kusali ilikuwa zaidi ya kufanya siasa kwenye nyumba za ibada za madhehebu ya kidini.
Alikuwa mkweli. Maisha yake yalifanana na kauli yake. Hata alipofanya makosa, ilikuwa rahisi kumsamehe kwa kuwa wananchi walitambua nia yake njema.
Kwa kiwango chake cha uelewa, akilinganishwa na wananchi wengi wa wakati wake, na marais wa nchi kadhaa za Afrika, kama angekuwa mwizi hata migodi hii ya madini tusingeikuta.
Bila uadilifu, angetumia rasilimali za nchi kujenga viwanja vya ndege na barabara za lami kijijini kwake, kama alivyofanya Rais Mobutu Seseseko wa Zaire.
Waliomwona akiwa mtoto, mwanafunzi, mwalimu, mwanasiasa mchanga, waziri mkuu, rais, na akiwa mstaafu shambani kwake Butiama – wanassema waliona tabia ile ile ya Nyerere mwema, mnyenyekevu, muungwana, mwaminifu, mkali wa haki, na mcha Mungu.
Alipofariki dunia mwaka 1999, katika salaam za rambirambi, Mziwakhe John Tsabedze wa Swaziland alisema: “Julius Nyerere alikuwa kiongozi halisi. Alitufundisha uadilifu na kutumikia raia wenzetu.
“Alitufundisha kuwa kipimo cha kiongozi si idadi ya magari ya kifahari anayomiliki, wala si idadi ya wake alionao. Alitufundisha kuwa kiongozi anaweza kuachia madaraka lakini akabaki na heshima yake, akasikilizwa.”
Efosa Aruede wa Nigeria aliandika: “Maisha ya kawaida na kujinyima aliyoishi Mwalimu Nyerere yalisaidia Watanzania kujitafakari na kufanya rejea juu ya maisha yake binafsi.”
Joshua Odeny wa Kenya aliandika: “Nyerere alikuwa maarufu nchini mwake hata baada ya miaka 14 tangu aondoke madarakani, kwa sababu aliongoza kwa kuonyesha njia. Alikuwa mfano wa wenzake. Alihubiri maji, naye alikunywa maji.”
“Alihubiri Ujamaa, naye akaishi kijamaa. Afrika haijapata kiongozi mwingine mkweli kama Nyerere.”
George Were wa Sudan aliandika: “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atakumbukwa siku zote kama raia wa dunia ambaye kila mmoja anatamani kuwa kama yeye.”
“Pale alipofanya makosa, ni kwa vile tu alikuwa binadamu, si kwa sababu alikusudia kuumiza binadamu wenzake.”
Christian Sorenson wa Denmark alindika: “Nyerere alikuwa na utu, alikuwa mahiri katika kuwasiliana na kuunganisha watu. Ni mwafika mwenye upeo wa hali ya juu. Alifanya makosa. Nani hakosei? Mimi binafsi namkubali.”
Hansel Ramathal wa India na Marekani alisema: “Alionyesha sifa ya uongozi uliotukuka alipostaafu na kumpisha Ali Hassan Mwinyi. Hili lilikuwa tendo moja lililodhihirisha ukomavu katika uongozi, jambo ambalo hatukuwa tumezoea kuliona katika Afrika na Asia.”
Hii ni taswira ndogo tu ya Mwalimu Nyerere tunayemkubuka leo. Kumlinganisha Mwalimu Nyerere na watu kiholela holela ni kumkosea adabu Mwenyezi Mungu.