27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATOA MAFUNZO KWA WAHASIBU, WAKAGUZI HESABU

Na KOKU DAVID

KATIKA mwaka wa fedha wa 2017/18 Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imejipanga kuhakikisha inashirikiana kwa karibu na  Wahasibu pamoja na Wakaguzi wa Hesabu kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali ili kuweza kukusanya mapato hadi kufikia lengo.

Mamlaka hiyo ambayo ina jukumu la kutoa elimu ya kodi, kukusanya mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi imetakiwa na serikali kukusanya sh. trilioni 17.106 katika mwaka wa fedha wa 2017/18.

Ili kuweza kufanikisha lengo la kukusanya mapato hadi kufikia lengo, mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na maofisa hao ambao ni sehemu ya jeshi la TRA katika kukusanya mapato ili kuwapa elimu ya masuala mbalimbali ya kodi.

Hivi karibuni TRA, imekutana na wahasibu na wakaguzi wa hesabu kutoka katika taasisi mbalimbali za hesabu na kuwapa elimu ya sheria za kodi mbalimbali.

Katika semina hiyo ya mafunzo ya kodi kwa wanataaluma hao ambayo yalifanyika kwa siku mbili, ilihudhuriwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere ambaye anasema kuwa lengo ni kuwafundisha ili wawe na uelewa wa aina ya kodi mbalimbali wanazotakiwa kuwakata watumishi hasa ile kodi ya zuio.

Anasema mafunzo yaliyotolewa kwa wanataaluma hao yalihusu elimu ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kuhusu mfumo mpya wa kukusanya kodi ya zuio hasa kwenye huduma na bidhaa.

Anaongeza kuwa walifundishwa namna ya kutumia mfumo wa malipo (Revenue Gate Way-RGS) ambao hutumika baada ya kodi stahiki ya serikali kukusanywa kwa mfumo wa kodi ya zuio.

Anasema baada ya mkataji wa kodi ya zuio kukata kodi inayotakiwa kuwasilishwa serikalini atatakiwa kuiwasilisha kwa kutumia mfumo wa malipo(RGS).

Anasema kabla ya mafunzo hayo wamekuwa wakikutana na changamoto kutoka kwa baadhi ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu ambao walikuwa hawajui aina ya kodi wanazotakiwa kuwakata watumishi hasa kutokana na mabadiliko ya sheria za kodi yanayokuwa yamefanyika baada ya bunge la bajeti kupitisha.

Anasema ili kuondoa changamoto hiyo, wameweka utaratibu wa kukutana na wanataaluma hao muda mfupi baada ya bunge la bajeti kumalizika ili kuwawezesha kujua mabadiliko yatakayokuwa yamejitokeza mapema wayafanyie kazi.

Anasema wahasibu na wakaguzi wa hesabu ni miongoni mwa jeshi la TRA ambalo kwa pamoja wanatakiwa kushirikiana na mamlaka hiyo ili kuhakikisha mapato ya kutosha yanakusanywa ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi wake.

Kichere anasema mikakati ambayo TRA imejiwekea ili kuweza kufikia malengo ya serikali ni pamoja na kufanya maboresho katika mfumo wa ulipaji wa kodi ya zuio ambao unamrahisishia utendaji mkataji wa kodi hiyo.

Anasema kwa kutumia mfumo huo mkataji wa kodi ya zuio na mkatwaji wataweza kutumia njia moja ambayo ni ya uwazi kwa kila mmoja wao kuhakikisha kodi iliyokatwa inawasilishwa TRA.

Anaongeza kuwa baada ya kodi hiyo kukatwa kwaajili ya kuwasilishwa TRA itapitishiwa kwenye akaunti ya mkatwaji ili kumuhakikishia kodi aliyokatwa imewasilishwa sehemu husika tofauti na awali yalikuwa yakifanyika kupitia akaunti ya mkataji.

Anasema baada ya utaratibu wa makato hayo kukamilika, vyeti vya kodi ya zuio iliyokatwa vitaonekana moja kwa moja kwa mkataji, mkatwaji pamoja na TRA kupitia mtandao wa mamlaka.

Kichere anasema sambamba na elimu ya kodi, pia wamefundishwa kuhusu matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutolea risiti(EFD) na kutakiwa kuhakikisha kila risiti itakayotolewa baada ya kupata huduma wanaikagua iwapo ni sahihi na kiasi cha pesa kilichoandikwa kinaendana na kile kilichotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles