- Ni ukolonimamboleo mlango wa nyuma
Na Lilian Justice,Morogoro.
SERA ya Taifa ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ulianza kabla ya uhuru kutokana na sababu za kihistoria, wananchi hawakushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, kwa kuwa walinyimwa fursa.
Hali hii ilikuwepo wakati wa ukoloni ambapo wananchi wengi waliwekewa vikwazo kushiriki katika uchumi ili watawalike kirahisi ambapo wananchi walilazimika kujishughulisha na uchumi wa sekta isiyo rasmi wakati sehemu kubwa ya sekta rasmi ilishikwa na watawala wa kikoloni na wageni.
Wakoloni walitumia mbinu mahsusi kuwaendeleza wazungu na wananchi wachache huku mbinu hizo ni pamoja na utoaji wa mikopo, utoaji wa elimu, ugawaji wa ardhi na utoaji wa leseni za biashara na baadhi ya mbinu hizo zinaweza kutumika hivi sasa kurekebisha hali hiyo na kuwawezesha wananchi kumiliki sehemu kubwa ya uchumi.
Hata hivyo baada ya Uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961, Wananchi walipata madaraka ya kisiasa  ya bendera lakini sehemu kubwa ya uchumi bado ilibaki mikononi mwa wageni na baadhi  ndogo ya Watanzania viongozi. Hali hiyo  ilileta kero na ni mojawapo ya sababu muhimu ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, mwaka wa 1967 .
Azimio hilo lilikuwa  mkakati muhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi kwa pamoja kupitia dola wanashika  na kumiliki njia kuu za uchumi.
Shughuli zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ziliundiwa mashirika ya umma lakini hata hivyo  mashirika ya umma mengi  yaliendeshwa kwa hasara  kwa kukosa uaminifu, weledi na ujuzi na  hivyo yaliendesha shughuli za kiuchumi kwa kutumia mtaji na ruzuku kutoka Serikalini, ikiwa ni kinyume na mategemeo ya mpango huo.
Katika kushiriki kikamilifu sasa kwenye shughuli za uchumi, wananchi wanakabiliwa na vikwazo  sugu vifuatavyo ambavyo ni upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ujuzi na uzoefu vikichochewa na upungufu katika elimu,  mafunzo, mila na desturi potofu na mtazamo  usio sahihi wa maendeleo.
Ukosefu wa masoko ya uhakika au  uzalishaji duni huleta ugumu wa uwezo wa kuingia katika masoko yenye ushindani.
Vilevile kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya watu au katika vikundi, ushirika hafifu na ukosefu wa sauti ya pamoja ya makundi mbalimbali ya wananchi katika kusimamia maslahi yao  ya Kiuchumi na  kuweza kukabili matatizo yanayowakwaza wasishiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ndani ya sekta zao.
Uwezeshaji uchumi
Aidha, kuna vikwazo katika uchumi  vitokanavyo na udhaifu wa mfumo wa kodi, sheria, kanuni na leseni pamoja na huduma nyingine za Serikali kuunga uchumi huo.
Sera ya Uwezeshaji inalenga kuondoa vikwazo hivi ili kutoa nafasi nzuri zaidi kwa makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu zaidi katika shughuli za uchumi.
Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA ) ambao ulisajiliwa rasmi mnamo mwaka 1995 ukiwa na lengo la kuhakikisha unawaunganisha wakulima ili kuweza kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi yao kama wazalishaji wakuu katika sekta ya uchumi.
Akizungumzia mtandao huo Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Stephen Ruvuga anasema lengo la kuanzishwa mtandao huo ni kuwaunganisha wakulima wadogo nchini ambao ndio wazalishaji wakuu na kuweza kupaza sauti zao ili changamoto zao  serikali iweze kuzitafutia ufumbuzi ili kuleta maendeleo katika Taifa.
Ruvuga anasema kuwa bado wakulima wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika wa mazao yao, ushuru usio na tija na mbegu feki ambazo humsababisha mkulima  hasara na huku migogoro ya ardhi ikiwaathiri kila kukicha .
Anasema licha wakulima kukumbwa na changamoto hizo kwa hivi sasa wakulima wadogo nchini wanahofia endapo serikali itasaini makubaliano ya ubia wa kiuchumi ( EPA)  na Ulaya kwani hauna tija kwao na badala yake utazidi kumdidimiza zaidi.
Anaeleza kuwa MVIWATA  umekuwa ukifuatilia kwa karibu mchakato wa majadiliano kati ya serikali  na EU juu ya makubaliano ya mashirikiano ya kiuchumi (EPA).
Janga la EPA
Ruvuga anaeleza kuwa tangu awali Mviwata imekuwa na mtazamo kwamba misingi ya makubaliano hayo hayana maslahi kwa wazalishaji wadogo wa Tanzania  na uchumi kwa ujumla na hivyo kuishauri serikali kuwa kusaini makubaliano hayo  ni kuweka rehani  maisha ya wakulima wa Tanzania hususani wakulima wadogo.
‘’Endapo Serikali itasaini makubaliano hayo ni kuuza maisha ya wakulima wadogo wa Tanzania ‘’anasema Ruvuga.
Alikomelea kwa kusema kuna athari hasi nyingi.
‘’Kutakuwa na athari katika mfumo wa uzalishaji wa wakulima wadogo na maisha  yao kwa ujumla’’anasema Ruvuga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MVIWATA Veronica Sophu anasema kuwa hofu kubwa ya wakulima  ni kuwa na uwezekano wa nchi kugeuzwa soko la bidhaa kutoka Ulaya na hivyo kuwanufaisha wazalishaji wa Ulaya kuliko wazawa.
Hata Rais wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa aliyaita masharti ya EPA kama ni ukoloni mambo leo na hayajabadilika kwa maana hayajali hisia za watuwetu.
Sophu anabainisha hatari kwa serikali kupoteza mapato yake ya ushuru wa bidhaa zinazoingizwa kutokana na masharti ya makubaliano hayo.
“Endapo nchi itaingia makubaliano hayo (EPAs) yataibana nchi kufanya biashara ya mazao ya kilimo na mengineyo na mataifa mengine kupitia mashirikiano mengine ya kibiashara hususani mashirikiano ya nchi za kusini kwa kusini(South-South Cooperation).
Naye Afisa Ushawishi na Utetezi Thomas Laiser anasema kuwa Mviwata inampongeza Rais Dk John Pombe Magufuli katika kikao cha 17 cha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki  kuacha kusaini makubaliano hayo ya EPA ili kujipa muda wa kutafakari na kujiridhisha iwapo kuna maslahi kwa mataifa ya Afrika Mashariki.
“Sisi kama Mviwata tunaunga mkono kwa asilimia mia moja msimamo huo wa serikali na kuiomba iufanye wa kudumu kwa kuangalia mazingira ya sasa na azma yake ya kujenga uchumi wa viwanda,’’anasema Laiser
Aidha anaeleza kwa hivi sasa nchi bado inapitia kipindi cha kufungua milango zaidi ya kiuchumi , kifedha na kibiashara  hivyo haina budi kuangalia kwa kina  suala hili la makubaliano ya kiuchumi .
Mhadhiri mstaafu kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof Mwesiga Baregu anasema kuwa mkataba wa EPA sio wa kwanza nchi za Afrika na zile za Ulaya kwani kumekuwepo na mikakati  mbalimbali hususan ule wa mji wa Younde wa nchini Cameroon  ambao ulikuwa mwaka 1963-1975.
‘’Pia kulikuwa na mkataba wa Lome kati ya mwaka 1976-1979 na ule wa Cotoneu  wa mwaka 2000 ambao umekuja kuzaa EPA,’’anasema Prof Baregu.
Mikakati hiyo ilikuwa na vipengele viwili ambavyo ni kuongeza biashara kati ya nchi za Kiafrika , Caribbean na Pasifik (ACP) ambapo nchi hizi zilikuwa makoloni ya nchi za Ulaya.
Anasema  muda wote huo haikuleta faida zozote kwa wananchi wa ACP  na badala yake nchi hizo zimebakia kuwa tegemezi.
Aidha anasema kuwa suala la EPA sio kitu kigeni bali kilichobadilika ni nchi za Ulaya badala ya kuchukua nchi za Afrika zote inataka mikataba ya Kikanda  mfano Afrika Mashariki na Afrika  Magharibi . Mtindo huu wa tuwa tugawe unafanywa makusudi ili kunyonya Afrika.
Anasema nchi zilizo katika Kanda zinatakiwa kusaini  ambapo mvutano upo sehemu tatu ambazo ni wasaini au waache, kusaini pamoja au kila mmoja asaini kivyake na pia kuendelea na mazungumzo ili kulinda maslahi binafsi na kusubiri mustakabali wa mbeleni wa kusaini ama kutokuusaini .
Prof Baregu anaeleza kuwa endapo Serikali itasaini mkataba wa EPA ni kujiwekea kitanzi kutokana na sababu mbalimbali .
Sababu hizo ni katika nchi za Afrika Mashariki mkataba huo unataka soko huria ili kubadili bidhaa zinazotoka nje ziingie nchini bila ya kutozwa kodi na nchi pia ipeleke Ulaya  bila ya kutozwa kodi.
“Katika nchi za Afrika Mashiriki, Kenya ni muathirika mkubwa inapambana na kutozwa kodi kwa uchumi wake kwani uko juu  ambapo hutegemea zao la maua kuuza barani Ulaya na kulipishwa kodi hivyo endapo nchi nyingine zitajiunga hawatalipa kodi, ’’anasema Prof Baregu.
Pia anasema kuwa endapo mkataba utasainiwa bidhaa zote za viwanda zilizotengenezwa nje zitaingizwa bila ya kulipilia kodi. Eneo hiloAfrika Mashariki halina ubavu.
Hasara yazidi faida
Baregu anaeleza kuwa endapo nchi ya Tanzania ikijiunga  itapoteza  dola za Kimarekani Mil. 940 kwa mwaka kwenye kodi ya Mapato.
‘’Nchi nyingine  kupata  athari endapo zitasaini mkataba huo ni Uganda  ambapo italazimu kupoteza Dola Mil. 597, Rwanda Dola Mil 241 na Burundi Dola Mil. 242 kwa mwaka,’’anasema Prof Baregu.
“Kutokana na changamoto hiyo nchi zenye lengo la viwanda haiwezi kufikia lengo kutokana na kupoteza mapato mengi ya kodi,’’anasema Prof Baregu, na kuongezea kuwa “kutokana na changamoto hiyo watakaoathirika ni wakulima wadogo, wavuvi, wafugaji wa kuku nk.
Anabainisha kuwa kwa upande wa Kampuni za Ulaya kwa asilimia 90  watatuzidi kwenye ushindani  huku nchi za kiafrika wakishinda ama kupata faida ni kwa asilimia 10% pekee.
Pia anaeleza kuwa viwanda vitakavyoathirika ni mafuta na gesi, mafuta ya kula, viuatilifu , mbolea , madawa na bidhaa zinazotumika kutengeneza vitu.
‘’Kwa sababu hiyo basi hakuna sababu yoyote ya kiuchumi, kisiasa , wala kijamii ambayo italeta hasara endapo hautosainiwa mkataba huo wa EPA,’’anafafanua  Baregu na kuhitimisha.
Anaeleza kuwa nchi za Afrika Mashariki tangu mwaka 2011 waliamua kupitia vikao vyake vya bunge la Afrika Mashariki, Baraza la mawaziri, wakuu wa nchi (summit) kuwa na mpango thabiti wa viwanda kwa  pamoja katika Afrika Mashariki.
Anasema kuwa sera hiyo imetoka kama mchakato lakini utekelezaji wake haujaweza kufanyika hivyo haiwezekani kuanzisha programu nyingine.
Hata hivyo Prof Baregu anasema kuwa endapo serikali ya Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda inapaswa kutekeleza maazimio waliyojiwekea kama serikali  ya mwaka 2012-2032 ambao ni mkakati wa pamoja wa viwanda Afrika Mashariki  uweze kutekelezwa kwanza ili kuweza kutambua kama EPA itaweza kuwa na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ni wakati sasa umefika kwa serikali kuwa makini katika kusaini mkataba huo na kuamua kusimama yenyewe na kuepuka vitisho vya kukosa misaada kutoka nchi za Ulaya na hivyo ni vyema viongozi walioko madarakani  kutokubali kusaini mkataba huo kutokana na visingizio fulani  na badala yake wawe waangalie athari zitakazowapata wananchi endapo serikali itajiingiza katika kuusaini mkataba huo.