ANTANANARIVO: Madagascar
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeipa Madagascar zaidi ya dozi miliomi moja za chanjo dhidi ya ugonjwa wa tauni katika juhudi za kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo ambao hadi sasa umekwisha kuua watu wapatao 33.
Uongozi nchini humo pia wamepiga marufuku watu kutembelea ndugu zao magerezani katika maeneo mawili yaliyokumbwa zaidi na ugonjwa huo.
Habari zinasema kuna uwezekano mkubwa wa ugonjw3a huo kusambaa haraka katika maeneo ya magerezani ambako kuna watu wengi.
Hivi karibuni serikali ya nchi hiyo ililaumiwa kwa kutochukua hatua za haraka kuukabili ugonjwa huo.
Maofisa wa afya wamesema mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa huo umeathiri watu wasiopungua 230 katika miezi miwili, wakiwamo waliokufa.
Kwa mujibu wa maofisa hao huathiri watu wapatao 400 kila mwaka nchini humo.
Maofisa hao wamesema aina ya ugonjwa wa tauni ulioikumba nchi hiyo mwaka huu ni unaoathiri zaidi mapafu na huenezwa kwa kukohoa.
Aina hiyo ya tauni ndiyo mbaya zaidi na husababisha kifo katika muda wa saa 24 tu.