27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CHADEMA AIRARUA SERIKALI MISHAHARA MIPYA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MBUNGE wa Viti Maalumu, Susanne Maselle (Chadema), amesema suala la nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma si hisani ila ni haki yao kwa mujibu wa sheria.

Hayo aliyasema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambapo alisema kauli ya Rais Dk. John Magufuli wakati akifungua  mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (ALAT), kwamba hatapandisha wala hana mpango wa kupandisha mishahara ya watumishi nchini imesababisha mkanganyiko mkubwa kwa Watanzania.

Susanne ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza, alisema kauli hiyo ya mkuu wa nchi ni wazi inaonyesha dharau kwa wabunge licha ya aliyekuwa Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki kulijibu suala hilo mara kadhaa, ikiwamo hatua ya Serikali kupandisha mishahara kwa watumishi nchini.

“Dharau kwa mhimili wa Bunge, dharau kwa watumishi nchini, dharau kwa wananchi. Kwamba nyongeza ya mishahara kwa watumishi inatolewa kwa hisani au kadiri rais anavyojisikia.

“Kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni haikuwa kweli. Hivyo nitoe wito kwa watumishi wote wa mkoani Mwanza wakishirikiana na wenzao wengine nchini kupitia vyama na jumuiya zao mbalimbali, kusimama kidete kupinga kauli na ulaghai wa Serikali kuhusu stahili zao.

“Watetee haki zao, hasa hii ya nyongeza ya mshahara, bila kuogopa! Mapambano ya kupigania haki za wafanyakazi duniani kote ni sehemu ya mapambano ya kitabaka,” alisema Maselle.

Alisema ni muhimu Serikali kama ilivyo sehemu nyingine duniani, itumie lugha ya kistaarabu na staha hasa kupitia njia za majadiliano ya mezani kufikia mwafaka katika kutatua matatizo ya wafanyakazi na kada nyingine katika jamii.

Alisema ni vyema wananchi na makundi mengine katika jamii kusimama pamoja na wafanyakazi dhidi ya unyanyasaji huo ambao ni kinyume na sheria zetu, kwa sababu sasa inazidi kudhihirika kuwa hakuna kundi liko salama au litabaki salama kwenye mikono ya utawala usiozingatia Katiba na kukiuka sheria za nchi.

“Kwa sababu inaonekana kauli iliyotolewa bungeni kuhusu nyongeza ya mishahara haikuwa kauli inayotokana na mipango au uwajibikaji wa pamoja wa Serikali yetu, basi mambo haya yafanyike ikiwemo Bunge letu liitake Serikali iwajibike bungeni kuhusu kauli (commitment) hiyo ambayo sasa ni dhahiri kuwa haikuwa ya kweli,” alisema.

Pia alisema Waziri mwenye dhamana aone umuhimu wa kuwajibika, kwa kutoa kauli isiyokuwa ya kweli bungeni au kwa sababu kauli yake hiyo (iwapo ilikuwa ya kweli) imekanushwa hadharani tena na mkuu wake wa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles