26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NASSARI AWASILISHA VIELELEZO VINGINE TAKUKURU


Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), amewasilisha vielelezo vya ushahidi wa awamu ya pili kuhusu tuhuma za kununuliwa madiwani mkoani Arusha, zinazowahusu madiwani wanane waliohamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nassari aliwasili makao makuu ya Taasisi hiyo Dar es Salaam jana, saa 7:57 mchana na kutoka saa 11:33 jioni.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi vielelezo hivyo, Nassari alisema kuwa, amepeleka upelelezi mwingine tofauti na tayari jalada limefunguliwa.

Alisema ushahidi huo ameuhifadhi kwenye ‘flash’ na ‘hard disk’ ambapo maofisa wa Taasisi hiyo waliupitia na kuangalia kilichomo ndani.

Alisema katika ‘flash’ na ‘hard disk’ hiyo, ana ushahidi mkubwa kuhusiana na sakata hilo, ambao unahusisha viongozi wakuu wa Serikali na watendaji wengine walioshiriki katika kutoa rushwa.

“Awali niliwaambia nina mambo kibao machafu yanayofanywa na viongozi wa Serikali …baadhi ya mambo hayo nimewasilisha Takukuru kwa ajili ya uchunguzi.

“Mpaka sasa maisha yangu yapo hatarini, kwa sababu nina ushahidi kamili unaohusisha viongozi wakuu wa Serikali, wakisema wanipoteze kwa sababu nimeingilia kazi za Usalama wa Taifa,” alisema Nassari.

Alisema mahojiano yalikuwa marefu kutokana na vielelezo hivyo, lakini alipewa ushirikiano wa kutosha.

Alisema baada ya kuwasilisha ushahidi huo, atawaita waandishi wa habari ili awaelezee kwa kina.

Alisema kutokana na mazingira haya, anatakiwa kuishi kwa ujanja ili kuepuka vitendo vya utekaji au kupigwa risasi kama alivyofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Alisema sasa amebadilishe utaratibu wa kuishi kulingana na mazingira yaliyopo, kwa sababu lolote linaweza kumtokea.

“Vitisho bado vinaendelea hadi sasa, vinatoka kwa baadhi ya viongozi wakuu wa serikali, hivyo basi napaswa kuwa makini ili kutetea roho yangu,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, amefungua jalada kuhusu tuhuma hizo na kwamba anasubiri uamuzi wa Serikali, baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

“Takukuru wamefungua jalada, nimeandika maelezo na wamenipa ushirikiano mzuri kwa sababu tayari na wenyewe wameanza upelelezi,” alisema.

Juzi, Nassari akiongozana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, walifika ofisi za Takukuru na kuonana na Mkurugenzi Mkuu, Valentino Mlowola, ambapo pamoja na mambo mengine, waliwasilisha ushahidi kuhusu madiwani wa chama chao kununuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles