KATIKA lugha ya Kiswahili kuna msemo usemao: ‘‘Ukiona nyumba ya jirani inawaka moto kimbia ukaokoe na ya kwako.’’
Mwezi uliopita afisa mmoja Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema kuwa wafungwa 34 walitoroka baada ya kuuvunja ukuta wa gereza wakati wa mvua kubwa iliyokuwa inanyesha.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Asociated Press (AP) Waziri wa Sheria wa Jimbo la Kivu Kusini, Pasaline Basezage alisema kwamba takribani wafungwa 27 waliotoroka Jumapili ya Septemba 24 jioni walikuwa wenye hatia ya uhalifu wa ngono na vitendo vingine vya ghasia.
Kutoroka kwa wafungwa katika gereza la Mwenga, ni mwendelezo wa vitendo vya utoro katika magereza mbalimbali nchini humo vinavyosababishwa na sababu mbalimbali zikiwamo: ujenzi hafifu wa magereza, msongamano, kuvamiwa, ukosefu wa chakula na matibabu ya uhakika.
Taharuki hii ya kutoroka kwa wafungwa katika nchi jirani hadi kusababisha afisa mmoja wa Serikali aitwaye Masumbuko kuwataka wakazi kuwa katika hali ya tahadhari, inaweza kutokea hata kwetu Tanzania maana hatuko mbinguni/peponi.
Nasema inaweza kutokea kwetu kutokana na mazingira yaliyopo kwa hivi sasa ambayo kwa namna moja au nyingine huenda yanasababishwa na maswala ya kiuchumi na kisiasa kama si ya kiutawala.
Ikumbukwe kuwa Rais John Pombe Magufuli akiwa katika ziara mkoani Mtwara ili kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya umeme, alitoa maagizo kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kukata umeme bila woga kwa wadaiwa sugu.
Mheshimiwa Rais alizungumza huku akisisitiza kuwa hata ikiwa jeshini, polisi au ofisi yoyote ya umma TANESCO wakate umeme tu kwani kila Wizara na Ofisi za umma huwa zinatengewa pesa ya malipo kwa ajili ya umeme.
Ni kweli mheshimiwa Rais mwenye nia ya kuibadilisha nchi kutoka kufanya kazi kwa mazoea hadi kuwajibika hana budi kuchukua hatua kali, lakini hatua hizo zichukuliwe kwa uangalifu mkubwa hasa kwenye maeneo nyeti ya kiusalama.
Fikiria Septemba 25 ambapo gereza kubwa lenye ulinzi mkali Butimba lilipokatiwa umeme kisa ni mdaiwa sugu, unategemea nini hata kama ilikuwa ni siku moja?
Kama wafungwa wenye makosa ya ubakaji na ghasia wametoroka katika gereza la Mwenga na Serikali ya Kongo inahaha kuwasaka, Je Tanzania yenye magereza yaliyosheheni wafungwa na mahabusu wa kutisha?
Nani hajui magereza yetu yana wafungwa wengi wa ujambazi wa kutumia silaha, ubakaji, mauaji, dawa za kulevya, wafungwa wa maisha na wafungwa wa kunyongwa?
Kutokana na utandawazi huku uhalifu ukifanyika kimkakati, nani hajui kuwa siku hizi kuna ugaidi wa kimataifa ambapo watuhumiwa wanaonaswa huletwa magerezani ?
Katika muktadha huu, magereza kukatiwa umeme, hali ambayo inaweza kuchochea wafungwa/mahabusu kutoroka na hatimaye kutishia usalama wa wananchi walioko nje, sina uhakika kama ni sahihi.
Katika nyakati hizi za uhalifu mamboleo ni bora Rais kuongeza umeme wa dharura kwenye magereza badala ya kufikiria kuukata. Ni busara magereza kuboreshewa ulinzi kwa kujengewa mifumo ya kompyuta inayotumia nishati ya uhakika kama ilivyo huko Marekani.
Wahaya wana msemo usemao: ‘‘Ukitaka kumuokoa ndege, muokoe akingali anaruka,’’ Naamini Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye dhamana ya Ulinzi na Usalama wa watu wake, kushauriana na Kamishina Jenerali wa Magereza ili kupata njia bora ya kulipa madeni ya TANESCO, kuliko kutumia njia hatarishi inayoweza kutuzalia majanga kama huko Kongo.